ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 15, 2016

Vyama nane vyaiandikia rasmi ZEC kujitoa uchaguzi Zanzibar

Vyama nane ambavyo vimeungana na Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar, vimeiandikia rasmi Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kuwa havitashiriki uchaguzi huo. Vyama vilivyochukua uamuzi huo ni Chauma, DP, Demokrasia Makini, SAU, Jahazi Asilia, NRA, UPDP na UMD.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chauma, Mohamed Massod Rashid, alisema uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, una viashiria kuwa ushindi utakuwa ni wa kulazimisha na kwamba marudio hayo ni batili kisheria.

“Vyama vyetu vinajiondoa rasmi kwa kuthibitisha wagombea wetu hawatashiriki katika ngazi zote za uchaguzi wa marudio, pia hatutohusika kuwamo kwenye karatasi za kura pamoja na kupokea machapisho yoyote na matokeo ya uchaguzi,” alisema.

“Taarifa ya kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu iliyochapishwa katika gazeti la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Novemba 6, mwaka jana chini ya kifungu cha 119 (10) cha Katiba na vifungu 3(1) na 5 (a) vya sheria havikufuatwa na vilikiukwa na kuvunjwa na Mwenyekiti wa Tume,” alisema.

Alisema kuharibu uchaguzi ni kosa la jinai na inapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwafikisha mahakamani wahusika ili sheria ichukue mkondo wake, lakini inashangaza kuona watu waliohusika bado wanapewa nafasi ya kuandaa uchaguzi wa marudio.

“Ni wajibu wa tume ya uchaguzi kuzingatia matakwa ya sheria zinazosimamia uchaguzi, na haiwezekani kuepuka misingi na matakwa ya wananchi katika kuchagua viongozi wanaowataka, tume haina mamlaka na uwezo wa kutengua au kufuta uchaguzi na matokeo ambayo yameshakamilika na kutangazwa, chombo chenye mamlaka ya kutengua na kufuta matokeo ni Mahakama Kuu Zanzibar,” aliongeza kusema.

Naye, Mwenyekiti wa Jahazi Asilia na mgombea urais Zanzibar, Kassim Bakar Ali, alisema Rais Dk. John Magufuli hana namna ya kukwepa suala la Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama anajitenga nalo, anapaswa kuondoa majeshi na polisi visiwani humo.

Aidha, alisema pia hawatashiriki uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Kijitoupele unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi (Nec) hadi watakapopewa vitambulisho vya kupigia kura vinavyotolewa na tume hiyo na siyo vilivyotolewa na ZEC.

Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, kwa kueleza kuwa uligubikwa na kasoro mbalimbali ikiwamo wapigakura kuzidi.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Huu ni uzembe uliosababishwa na maamuzinpejee ya Jecha. Hili ninjipu limekaa pabaya nimi kinachosubiriwa muda wote lisitumbuliwe!? Jecha anatakiwa ajiuzulu mara moja kwa kuingiza Zanzibar kwenye mtafaruki mkubwa na kuingia gharama lukuki zenye kupoteza fedha. Tunashauri kwa aondolewe kwenye nafasi hiyo sivyo ataendelea kuleta shubiri Visiwani hata mara baada ya tarehe hiyo mbaya ya kufanya uchaguzinwa CCM pekee. Hata wabunge wawakilishinwalioko bungeni sio halali. !! Ninapita.

Anonymous said...

kwa maoni yangu hili tukio la kufuta uchaguzi linatufunza mengi sisi Wazanzibari kama tutazingatia. huyu Jecha ndio alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi kwa mujibu wa katiba, na baada ya kufanyika uchaguzi kaona kuna kasoro na kaamua kuufuta uchaguzi. mimi naona alichofanya ni sawa kwa nafasi yake aliyokuwa nayo. cha msingi ni kujifunza hili ndio limeshatokea na kama hatutaki in the future mkurugenzi wa uchaguzi aeleze kasoro zozote au asifute uchaguzi kwa sababu ya kasoro zozote no matter what basi turekebishe katiba na kuweka wazi hayo. kwa hatua aliyoichukua wale wasioridhika nayo ni kwa nini wasiende mahakamani. inasikitisha sana tena sana wanasheria wetu wanapenda kukaa kwenye vyombo vya habari zaidi na kutoa maoni yao badala ya kuchukua hatua za kufungua kesi za pingamizi mahakamani. nilisikitika sana siku moja nilipomwona mwanasheria Fatma Karume-Barrister at law alipoulizwa kwa nini asifungue kesi dhidi ya uamuzi wa kuufuta uchaguzi wa Zanzibar, alijibu hana imani na majaji kama watatoa haki kwani jaji mstaafu mheshimiwa Agostino Ramadhani aligombea urais kwa kupitia CCM. huyu Karume amechanganyikiwa Agostino amegombea urais akiwa sio Chief Justice ni raia wa kawaida alietumia haki yake ya kikatiba. Mwanasheria mwengine Tundu Lisu alitetea kitendo cha Maalim Seif cha kuvunja sheria kwa kujitangazia ushindi kinyume na sheria. Lisu alisema hata yeye alifanya hivyo na haoni kosa. Lisu kama ulivunja sheria na ukanusurika kukamatwa na kushtakiwa haimaanishi kwamba ulichofanya hakikuwa kosa. Wazanzibari tunapenda kulaumiana lakini ukweli ni kwamba asilimia kubwa hatutaki kufuata sheria, tunafuata mapenzi na maslahi yetu tu na hata kama sheria tulizozitung zina mapungufu hatukai na kuzirekebisha bali tunapiga kelele tu za kisiasa -SIASA INATUMALIZA ZANZIBAR Mungu tuokoe!!!!!

Anonymous said...

Hiyo mahakama unayoiongelea wewe mdau wa pili ya kupeleka kesi inasimamiwa na nani? Si ndio hao hao. Sasa toka lini ukapeleka kesi ya kima kwa ngedere na haki itendeke? Tafakari!