ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 22, 2016

HOTUBA YA MHE. WAZIRI MKUU MAJALIWA ALIYOITOA LEO TRH 22.04.2016


 HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHE. KASSIM M. MAJALIWA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2016/2017

 

UTANGULIZI


1.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2015/2016 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2016/2017. Vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2016/2017.

2.            Mheshimiwa Spika, huu ni Mkutano wa Bunge wa kujadili Bajeti ya Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2015. Hivyo naomba nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi na hivyo kukiwezesha kushinda na kukipa tena ridhaa ya kuunda Serikali na kuiongoza Nchi yetu. Aidha, kwa njia ya pekee napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano. Pia, nampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nawapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo muhimu.

Nawahakikishia wananchi wote kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia kwa nguvu zake zote bila kujali itikadi zao za kisiasa.

3.            Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kutumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uteuzi huo kuungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge kwa asilimia 73. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwamba sitawaangusha.

4.            Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Pia, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa Wawakilishi wa Wananchi katika Bunge hili. Jukumu lililo mbele yetu sote ni kuwatumikia wananchi waliotuchagua ili kuwaletea maendeleo.

5.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Nchi yetu imekumbwa na majanga mbalimbali yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Nitumie fursa hii kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie wale walioumia kupona haraka na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa. Ninawapa pole wote waliofiwa na ndugu, jamaa na marafiki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.  Amina!


6.            Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kupitia kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie nafasi hii, kuwashukuru  Wajumbe  wa  Kamati  ya  Kudumu  ya  Bunge  ya

Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Hasna Sudi Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, naomba niwapongeze Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia makadirio ya sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana katika kuboresha Makadirio ya bajeti ya Serikali.

7.            Mheshimiwa Spika, makadirio ya bajeti ninayowasilisha leo  ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015. Ilani hiyo, imeainisha ahadi ambazo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itazitekeleza katika miaka  mitano ijayo. Aidha, makadirio ya Bajeti yamezingatia ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati wa Kampeni na katika uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja, tarehe 20 Novemba 2015. Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kujenga Taifa imara kiuchumi na maendeleo ya watu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Barani Afrika kwa ujumla.

MWELEKEO WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO


8.            Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwasilisha mapitio ya kazi za Serikali kwa mwaka 2015/2016 na mwelekeo kwa mwaka 2016/2017, niruhusu kupitia Bunge lako Tukufu niwakumbushe Watanzania wote kuhusu dhima ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye falsafa ya “Hapa Kazi Tu”. Sote tunatambua kwamba ili Tanzania ifikie Nchi yenye Uchumi wa Kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025 ni sharti kila mmoja wetu afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu wa hali ya juu. 

9.            Mheshimiwa Spika, ili yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye uchumi wa kati tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa Viongozi, Watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya Watumishi wasio waadilifu wanaotumia fedha za umma au madaraka yao vibaya na kukwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo tunayojiwekea. Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uzembe, ubadhirifu, uvivu na kukwepa wajibu wetu. Ndiyo maana, tumeanza kwa nguvu kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili zielekezwe kwenye shughuli zenye manufaa kwa Watanzania walio wengi na siyo vinginevyo.

10.         Mheshimiwa Spika, pamoja na kuimarisha ufanisi na tija ndani ya utumishi wa umma, tumebaini kuwa changamoto ya utamaduni usioridhisha wa ufanyaji kazi upo katika sekta zote, za umma na binafsi. Wizi, uzembe, udhuru wa kila siku na huduma mbaya kwa wateja ni baadhi ya malalamiko ya wawekezaji hapa nchini. Tabia hizi ni lazima zikemewe kama tunataka nguvu kazi yetu ipate ajira katika zama hizi tunazohamasisha mapinduzi ya viwanda. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu katika jamii kusimamia maadili na makuzi ya vijana ili nguvu kazi hii iweze kutumika ipasavyo kuchangia ukuaji wa uchumi.

11.         Mheshimiwa Spika, imani yetu ni kwamba tumeanza vizuri kwenye suala la kuongeza uwajibikaji na maadili ndani ya Serikali. Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana na Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano. Jambo la msingi ni kwamba tutachukua hatua kwa kufuata Sheria, Kanuni  na Taratibu za Utumishi wa Umma. Niwahakikishie Watanzania kwamba hakuna mtumishi au mwananchi atakayeonewa au kunyanyaswa katika zoezi hili. Hivyo, wale wote ambao wako safi waendelee kutimiza wajibu wao bila woga. Kazi zifanyike kwa weledi na kwa kasi bila  urasimu.

12.         Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua za kuongeza mapato na kuziba mianya ya ukwepaji kodi ambazo zimeonesha manufaa makubwa. Mathalan, hatua tulizochukua za kubana mianya ya ukwepaji kodi zimeimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 870 mwezi Novemba, 2015 na kufikia Shilingi trilioni 1.3 mwezi Machi, 2016. Tunaendelea kuimarisha ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kila anayetakiwa kulipa kodi alipe na fedha hizo zitumike kutekeleza mipango ya maendeleo. Vilevile, Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali. Fedha zinazopatikana zitaelekezwa kwenye miradi ya kipaumbele yenye kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.

13.         Mheshimiwa Spika, uchumi wa viwanda utajengwa na Sekta Binafsi. Kazi ya Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki kwa sekta hiyo kuwekeza. Hivyo, Serikali itaendelea kubuni na kutekeleza miradi itakayowezesha sekta binafsi kuwekeza bila vikwazo. Miradi hiyo ni pamoja na miundombinu muhimu ya uchukuzi na usafirishaji, umeme, mawasiliano na maji kwa ajili ya uzalishaji na biashara. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia wawekezaji wote nchini na wengine wanaokusudia kuwekeza kwamba Serikali imedhamiria kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi. Hatua zote zinazochukuliwa sasa ni za kuhakikisha kwamba sekta binafsi inawekewa mazingira wezeshi na yenye ushindani wa haki ili iweze kuimarika.

SIASA


14.         Mheshimiwa Spika, mtangamano wa kisiasa ni nguzo muhimu katika kujenga Nchi yenye maendeleo makubwa na ya uhakika. Mtangamano wa kisiasa unajumuisha siasa safi, za kiustaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu. Siasa za aina hii ndiyo chimbuko la mustakabali wa amani na utulivu wa Taifa letu tangu tujipatie uhuru. Ni jambo la faraja na kufurahisha kwamba, pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kujaa tashwishwi na ushindani mkubwa, Taifa letu limeendelea kuwa na amani, utulivu na mshikamano mkubwa Kitaifa kiasi cha kupigiwa mfano Barani Afrika na dunia kwa ujumla. Hali hii inaonesha kukua na kuimarika kwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini ambapo hadi sasa vipo vyama 22 vyenye usajili wa kudumu na vyama vitatu vyenye usajili wa muda na vingine sita vimewasilisha maombi ya usajili wa muda.

15.         Mheshimiwa Spika, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 umesaidia kupima namna demokrasia inavyozidi kukua na kupanuka kwani kwa mara ya kwanza kulikuwa na mwitikio mkubwa wa kujitokeza kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na wananchi wengi kujiandikisha kupiga kura. Vyama nane vilisimamisha wagombea wa nafasi ya Urais na vyama 22 Ubunge na Udiwani. Idadi ya wapiga kura walioandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa 23,161,440, sawa na asilimia 96.9 ya makadirio. Idadi ya watu waliopiga kura ilikuwa ni 15,596,110, sawa na asilimia 67.3 ya waliojiandikisha. Hii ni idadi kubwa ya wapiga kura ikilinganishwa na chaguzi zote zilizopita. Hivyo, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa  kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kuanzia katika uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura, ugawaji wa majimbo mapya ya uchaguzi, kutoa elimu kwa umma, uandikishaji wa wapiga kura na kuusimamia kwa umakini mkubwa uchaguzi wenyewe na kutangaza matokeo. Tume ilifanya kazi yake kwa uhuru na kwa weledi mkubwa. Niwapongeze viongozi na wananchi wote walioshiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

16.         Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Tume na wananchi kuitikia wito wa kujiandikisha na kupiga kura, bado kulikuwa na idadi kubwa ya waliojiandikisha lakini hawakupiga kura. Naiagiza Tume ya Uchaguzi kufanya tathmini ya kina kubaini sababu zilizofanya wapiga kura zaidi ya Milioni saba waliojiandikisha kupiga kura kutoitumia haki yao ya Kikatiba.  Hii itasaidia kuboresha chaguzi zijazo kwani wananchi wana wajibu wa kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka. Aidha, tathmini itasaidia kubaini iwapo kuna vikwazo vinavyowazuia baadhi ya watu kupiga kura ili kwa pamoja tuviondoe. Ndani ya Bunge hili tupo wabunge wa Vyama mbalimbali lakini kwa lengo moja tu la kuwawakilisha wananchi wetu na kuishauri Serikali ili ipange mipango mizuri itakayoharakisha maendeleo yao. Niseme tu kwamba sasa Uchaguzi Mkuu umekwisha na Serikali zetu zipo madarakani kwa mujibu wa Katiba. Hivyo, tuienzi falsafa ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya “Hapa Kazi Tu!” kwa kuchapa kazi na tusitoe nafasi kwa tofauti zetu za kisiasa na kiitikadi kuwa kisingizio cha kukwamisha shughuli za maendeleo ya Nchi yetu.

17.         Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendelea kukuza Demokrasia ili kuwezesha ushiriki mpana wa wananchi katika kufanya maamuzi ya maendeleo yao katika Taifa letu chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hivyo, Serikali inaandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 kwa lengo la kuondoa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake na kuzifanya ziendane na hali halisi ya siasa nchini na kwa mtazamo wa baadaye.

 

UCHUMI


Ukuaji wa Uchumi


18.         Mheshimiwa Spika, malengo yetu ya kufikia Nchi ya kipato cha kati na kufanyika mapinduzi makubwa ya viwanda yanategemea sana utulivu wa uchumi. Kwa ujumla, ukuaji wa uchumi umekuwa wa kuridhisha kwani mwaka 2015, uchumi ulikua kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2014. Sekta zilizochangia katika ukuaji huo ni pamoja na Ujenzi, Mawasiliano, Fedha, Uchukuzi na Nishati. Pamoja na ukuaji huu mzuri wa ujumla, Sekta ya Kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 66.3 ya Watanzania wote wanaofanya kazi ilikua kwa asilimia 3.4 tu mwaka 2014. Ukuaji huo mdogo unamaanisha kwamba juhudi za ziada na kubwa zinahitajika ili sekta hii muhimu iweze kutoa mchango mkubwa zaidi wakati tunapotekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo. Historia ya maendeleo ya uchumi inatuambia kwamba, Sekta ya Kilimo ina mchango mkubwa na muhimu kwenye mapinduzi ya viwanda. Hivyo hatuna uchaguzi mwingine bali kuelekeza nguvu zaidi kwenye sekta hii ya kilimo.

19.         Mheshimiwa Spika, kwa ujumla tutahitajika kuongeza ufanisi na tija katika sekta zote za uzalishaji na utoaji huduma ili malengo yetu ya ukuaji uchumi yafikiwe katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika kufikia azma hiyo, tutatekeleza sera madhubuti za fedha na kodi zitakazowezesha mfumuko wa bei kuendelea kushuka na kubaki katika tarakimu moja kama ilivyo sasa. Mathalan, mfumuko wa bei mwaka 2015 ulifikia wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.1 kwa mwaka 2014. Mwelekeo huu wa utulivu wa uchumi utavutia mitaji mingi kutoka Sekta Binafsi kuwekeza kwenye sekta za kipaumbele, kuwezesha ongezeko la ajira na kupanua wigo wa ulipaji kodi.

Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji


20.         Mheshimiwa Spika, awali nilidokeza kwamba, uwekezaji kwenye viwanda na sekta nyingine za kiuchumi utafanywa na sekta binafsi na jukumu la msingi la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi. Kwa msingi huo, Serikali ya Awamu ya Tano itachukua hatua madhubuti na za haraka kupunguza muda, gharama na idadi ya taratibu za kiutawala ambazo Wafanyabiashara na Wawekezaji hulazimika kuzifuata ili kufanya biashara nchini. Taratibu zinapokuwa ngumu na ndefu husababisha ongezeko la gharama za kufanya biashara na hivyo kuwakatisha tamaa wawekezaji. Taarifa ya Wepesi wa Kufanya Biashara duniani inayotolewa na Benki ya Dunia iliyochapishwa mwezi Novemba, 2015 inaonesha kwamba katika mwaka 2016, Tanzania imeshika nafasi ya 139 kati ya Nchi 189 Duniani. Hali hii haikubaliki kabisa. Hivyo, eneo hilo litafanyiwa kazi haraka ili kuharakisha mapinduzi ya viwanda.

21.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Mpangokazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini. Utekelezaji huo utazingatia maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa mkutano na Wafanyabiashara uliofanyika mwezi Desemba, 2015. Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Mheshima Rais aliwataka watendaji kupunguza urasimu usio wa lazima kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuyatumia mabaraza ya biashara ya Mikoa na Wilaya ili kuhakikisha juhudi shirikishi za uboreshaji wa mazingira ya biashara zinatekelezwa hadi ngazi ya chini. Pia, nawataka watumishi wa umma kuepuka kuwachelewesha kwa uzembe au makusudi wawekezaji wenye nia njema ya kuwekeza nchini ili kuleta maendeleo endelevu kwa wakati. Mtumishi yeyote wa umma atakayeendeleza urasimu usio wa lazima hatavumiliwa.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi


22.         Mheshimiwa Spika, azma ya kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda ni jambo la msingi. Hivyo, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye Taasisi za Fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu. Pamoja na hatua hizo, Mpango Maalum wa Ushiriki wa Watanzania katika miradi mikubwa ya uwekezaji ulioandaliwa utatekelezwa. Mpango huo unalenga kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali za Nchi yao kwa njia ya ubia kwenye miradi ya uwekezaji, ajira na kandarasi mbalimbali zitakazotolewa na kampuni kubwa kwa Wazawa. Wananchi pia wataendelea kuwezeshwa kupitia mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi mbalimbali vya kiuchumi vya wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini inayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Serikali imeruhusu Mifuko hiyo kutoa mikopo nafuu kwa wanachama wa vikundi vinavyojiunga na Mifuko kunufaika na mafao ya afya na pensheni yanayotolewa na mifuko husika.

23.         Mheshimiwa Spika, Serikali imehamasisha uanzishaji na usajili wa Vikundi vya Kiuchumi kama vile Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOs) na Benki za Jamii Vijijini (VICOBA). Serikali pia imesimamia uanzishwaji wa Taasisi Mwavuli ya kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA. Takwimu zilizotolewa mwezi Februari 2016 na Taasisi hiyo zinaonesha kuwa kuna vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama Milioni 2.2 na mtaji wa Shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya wanachama wa VICOBA ni wanawake.

24.         Mheshimiwa Spika, moja ya ahadi muhimu iliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ni kutenga Shilingi Milioni 50 kwa kila kijiji nchini zitakazotumika kwa utaratibu wa mzunguko (Revolving Fund). Lengo ni kuwawezesha wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa na vikundi vingine vya kiuchumi. Uhakiki wa Vyama vya Ushirika wa Kuweka na Kukopa uliofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika unaonesha kwamba idadi ya SACCOs zinazokidhi vigezo vya usajili nchini imepungua kutoka 5,559 mwaka 2013 hadi 3,856 mwaka 2015. Kati ya hizo, SACCOs 2,125 sawa na asilimia 55 zipo Vijijini na 1,740 zipo Mijini. Ni dhahiri kwamba Mpango wa Shilingi Milioni 50 kwa kila Kijiji unahitaji maandalizi mazuri, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji na usajili wa SACCOs na vikundi vya kiuchumi  vinavyokidhi vigezo, ili kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa zinawafikia walengwa na zinatumika kwa shughuli zilizokusudiwa. Ninaziagiza Halmashauri zote nchini ziweke orodha sahihi ya Vyama vya Ushirika wa Kuweka na Kukopa vilivyosajiliwa kwa kila Kijiji na kuchukua hatua za kuwezesha uanzishaji na usajili wa SACCOs zinazokidhi vigezo kulingana na shughuli za uzalishaji katika Halmashauri husika.

25.         Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, maandalizi ya utekelezaji wa Mpango huo yanaendelea vizuri katika kila Halmashauri. Tutatumia uzoefu uliopatikana kwenye utekelezaji wa mifuko mingine, ukiwemo Mfuko wa Kuwawezesha Wananchi na Kuongeza Fursa za Ajira maarufu kama “Mabilioni ya JK”, ili changamoto zilizojitokeza zitusaidie kuboresha Mpango huu mpya.

26.         Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuziwezesha Kaya maskini ili ziweze kupata mahitaji yao ya msingi na kuongeza kipato kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III). Tangu utekelezaji wa Mpango huo uanze kaya maskini 1,099,289 zimepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 164.8 kama ruzuku katika Halmashauri 159 za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.  Aidha, kupitia Mpango wa Ajira za Muda kwa Kaya Maskini, iliandaliwa miradi 1,880 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 42.6 kutoka Halmashauri 40 za Tanzania Bara na Zanzibar. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kufanya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini katika maeneo ambayo hayakufikiwa.

 

Ajira


27.         Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 imeweka umuhimu katika  kupanua fursa za ajira kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie kwenye uchumi na kupata kipato halali. Msisitizo huo wa Ilani ya Uchaguzi unatokana na ukweli kwamba Utafiti wa Hali ya Ajira Nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3 mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira  kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014. Kiwango hicho bado ni kikubwa na tunaweza  kufanya vizuri zaidi.  Jitihada za  Serikali  za kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi zitaendelezwa ili kupunguza zaidi kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.

28.         Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni vijana wetu kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza Programu  ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi  Nchini (2015/2016 – 2019/2020). Programu hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia 3 ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi 54. Utekelezaji wa Programu hiyo utasaidia kupunguza pengo la mahitaji ya rasilimali watu nchini ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya haraka ya uchumi wa viwanda. Serikali itahakikisha kuwa suala la ukuzaji ajira linazingatiwa katika mipango yote ya uwekezaji pamoja na mipango ya maendeleo ya kisekta katika ngazi zote. Hivyo, nazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha ukuzaji wa ajira  unakuwa ni agenda ya msingi ya kudumu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Tayari Mheshimiwa Rais amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kwamba vijana ambao ndiyo nguvu kazi kuu ya Taifa wanatumia fursa itakayopatikana kutokana na Shilingi Milioni 50 zitakazotolewa kwa kila kijiji kuanzisha miradi ya maendeleo ya kujipatia kipato.

VIJANA


29.         Mheshimiwa Spika, vijana ni hazina na rasimali watu  muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha kuwa idadi ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ni takribani Milioni 16.2, sawa na asilimia 35.1 ya Watanzania wote. Aidha, Utafiti wa Nguvu Kazi wa mwaka 2014 unaonesha kuwa vijana ni asilimia 59 ya nguvu kazi ya Taifa. Matokeo ya tafiti hizo yanathibitisha kuwa kuna umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana na ushirikishwaji wao katika mipango ya maendeleo. Katika mwaka 2014/2015 hadi 2015/2016, Serikali imewawezesha vijana kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Hadi kufikia mwezi Machi 2016, mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.6 imetolewa na Mfuko huo kwa vikundi vya vijana 284 na mafunzo yametolewa kwa viongozi wa vikundi 2,552 kutoka Halmashauri 59. Vilevile, Serikali imetenga maeneo maalum ya shughuli za kiuchumi na huduma kwa vijana katika Halmashauri 30 nchini.

30.         Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha dhana ya ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo, Bunge la Kumi lilitunga Sheria Na. 12 ya Baraza la Taifa la Vijana ya mwaka 2015. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sasa Kanuni za utekelezaji wa Sheria hiyo zimekamilika. Hivyo,  katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa na kuhimiza uanzishaji na uimarishaji wa SACCOs za vijana  katika Halmashauri zote nchini na kuziwezesha  kupitia Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana na Taasisi za fedha.

31.         Mheshimiwa Spika, Maadili na Makuzi ya Vijana ni suala linalopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano. Hatuwezi kujenga uchumi imara wa viwanda, kuongeza fursa za ajira na kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali za umma kama jamii yetu, hasa vijana hawatajitambua kwa kuwa waadilifu, wazalendo na wachapakazi. Serikali, itaendelea kuratibu utekelezaji wa Programu ya Stadi za Maisha na Programu ya kujitolea kwa vijana ili kukuza maadili, uzalendo na kujenga utamaduni wa kuchapa kazi kwa vijana.

WATU WENYE ULEMAVU


32.         Mheshimiwa Spika, Serikali inathamini mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo na kwamba wana haki sawa ya kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika kuzingatia azma hiyo, Serikali inatekeleza Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010, ambayo, imewezesha kuundwa kwa Baraza la Kitaifa la Ushauri la Watu wenye Ulemavu ili kuongeza ushiriki wa Watu wenye Ulemavu katika maamuzi. Aidha, Kamati za kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu zimeundwa katika ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata, Mitaa na Vijiji kwa ajili ya kuratibu masuala muhimu kwa watu wenye ulemavu katika maeneo husika.

33.         Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuwalinda na kuwapatia fursa, kumekuwepo na matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu hususan watu wenye ualbino. Ukatili huo umesababisha watu wenye ualbino kupoteza maisha na wengine kupata aina nyingine ya ulemavu wa kudumu. Hali hiyo haikubaliki na haivumiliki katika jamii ya Watanzania. Serikali inafanya jitihada kubwa kukomesha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Aidha, itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kubadili mitazamo na imani potofu kuhusu watu wenye ualbino na ulemavu kwa ujumla. Napenda kusisitiza kwamba watu wenye ulemavu wana haki ya kuthaminiwa utu wao na kulindwa dhidi ya ukatili na aina yoyote ya ubaguzi.

34.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaviboresha Vyuo vya Ufundi na Marekebisho (Vocational and Rehabilitation Training Centres) vya watu wenye ulemavu nchini ili kutoa ujuzi unaoendana na mahitaji yao katika soko la ajira. Serikali pia, itaandaa walimu wa elimu maalum na kutoa vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye ulemavu mashuleni. Kwa sasa Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwahabarisha watu wenye usikivu hafifu kwa kuanzisha tafsiri za matangazo kwa njia za alama. Hivyo, wamiliki wote wa Televisheni wametakiwa kuajiri wakalimani.

 

KAZI NA HIFADHI YA JAMII


Kazi


35.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na viwango vya kazi kwa kufanya kaguzi ili kuhakikisha waajiri wanazingatia mikataba ya ajira, masaa ya kazi, likizo na ujira kwa lengo la kupunguza migogoro na kuongeza tija. Hadi kufikia Machi 2016, jumla ya kaguzi  za kazi 1,305 zilifanyika na migomo 23 katika sekta za usafirishaji, viwanda, ujenzi na kwenye migodi ilisuluhishwa na kupatiwa ufumbuzi. Aidha, kaguzi za kawaida 4,670 na kaguzi maalum 17,005 zilizojumuisha kaguzi za umeme, mitambo na vipimo vya mazingira ili kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na afya njema na usalama mahala pa kazi zilifanyika.

36.         Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kuratibu Ajira ya Wageni Na. 1 ya Mwaka 2015 ilitungwa na kumpa Kamishna wa Kazi mamlaka ya kutoa vibali vya kazi nchini ili kukuza fursa za ajira kwa Watanzania. Tangu Sheria hiyo ianze kutumika rasmi tarehe 15 Septemba 2015 hadi mwezi Machi 2016, mapato yaliyopatikana kutokana na vibali vya kazi vilivyotolewa nchini ni Shilingi Bilioni 21.01, sawa na asilimia 356 ya lengo la makadirio ya Shilingi Bilioni 7.5 kwa mwaka 2015/2016. Serikali pia imefanya kaguzi katika Makampuni na Taasisi 400 zenye jumla ya wageni 3,939 na kubaini wageni 779 hawana vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini. Kati ya hao, wageni 29 waliondolewa nchini, 317 walipewa hati maalum (special pass), 77 walifikishwa mahakamani na 356 walielekezwa kukamilisha taratibu za ukaazi wao kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Sheria ya Uhamiaji. Katika mwaka  2016/2017, Serikali itafanya kaguzi za kazi 56,200 katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini na itaanzisha Bodi mbili za kupanga kima cha chini cha mishahara kwa sekta ya umma na binafsi.

Hifadhi ya Jamii


37.         Mheshimwa Spika, Sekta ya Hifadhi ya Jamii ina mchango mkubwa katika uchumi wa Nchi yetu. Kwa kutambua hilo, Serikali imeifanyia tathmini mifuko sita ambayo ni GEPF, LAPF, NHIF, NSSF, PPF na PSPF kwa lengo la kupima uendelevu wake. Tathmini hiyo imebainisha kuwa mifuko hiyo bado ni endelevu na rasilimali zake zimefikia Shilingi trilioni 8.8. Aidha, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii imetoa miongozo ya kupunguza gharama za uendeshaji wa Mifuko hiyo itakayoanza kutumika Julai, 2016. Serikali imekamilisha uhakiki wa madeni ya PSPF yaliyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo mwaka 1999 yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.9. Hadi sasa,
Serikali imelipa sehemu ya deni la PSPF kiasi cha Shilingi Bilioni 180 ili kuhakikisha kwamba mafao ya wastaafu wa Mfuko huo yanalipwa kwa wakati. Serikali pia itaendelea kulipa deni la Shilingi Bilioni 840.4 linalotokana na miradi ya Serikali iliyogharamiwa na mifuko ya GEPF, LAPF, NHIF, NSSF na PPF.

38.         Mheshimiwa Spika, hadi sasa asilimia 6.5 ya Watanzania wote ndiyo wanaofikiwa na huduma ya Hifadhi ya Jamii. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuongeza wigo wa wanaofikiwa na huduma hiyo. Hii ni pamoja na kujumuisha makundi mengine katika jamii kama vile wazee na watu wenye ulemavu ambapo rasimu ya andiko la mpango wa pensheni kwa makundi hayo imekamilika. Hatua inayoendelea hivi sasa ni ushirikishwaji wa wadau na taasisi zitakazohusika katika kutekeleza mpango huo. Aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha uchangiaji wa hiari na kusimamia uendeshaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora  na kuchangia zaidi katika ukuzaji wa uchumi bila kuathiri mifuko.

SEKTA ZA UZALISHAJI MALI


Uzalishaji wa Mazao na Akiba ya Chakula

 

39.         Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo inayojumuisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu ndio tegemeo la maisha ya watanzania walio wengi. Hata hivyo, ukuaji wa sekta hiyo umekuwa siyo wa kuridhisha kutokana na matumizi ya teknolojia isiyoendana na wakati na pia kutegemea majaliwa ya Mwenyezi Mungu ya hali ya hewa. Pamoja na changamoto hizo, hali ya upatikanaji wa chakula imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi hapa nchini. Katika msimu wa 2014/2015, wakulima walizalisha Tani Milioni 15.5 za mazao ya chakula. Kutokana na uzalishaji huo, Nchi imejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120 kwani mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 ni Tani Milioni 12.95. Hali hii pia imetuwezesha katika msimu huu kutoa chakula cha msaada na cha bei ya chini katika maeneo yaliyopata upungufu wa chakula. Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula - NFRA iliuza jumla ya Tani 239,322 ya akiba yake kwa wafanyabiashara nchini ili kukabiliana na mfumuko wa bei za vyakula hususan unga wa sembe katika masoko ya mijini. Hadi kufikia mwezi Aprili 2016, NFRA ilikuwa na akiba ya Tani 67,895 za chakula. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itanunua Tani 100,000 kwa ajili ya hifadhi ya chakula.

40.         Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kupanua na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha zaidi kwa ajili ya usalama wa chakula, kuuza ziada nje na kupata malighafi za viwandani. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, inalenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka Hekta 461,326 za sasa hadi Hekta Milioni moja ifikapo mwaka 2020. Ili kufikia lengo hilo, Serikali itashirikiana na sekta binafsi katika kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji nchini.

Ruzuku za Pembejeo


41.         Mheshimiwa Spika, ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao unategemea kwa kiasi kikubwa matumizi ya pembejeo zikiwemo mbolea  na mbegu bora zenye ukinzani na ustahimilivu wa magonjwa na ukame; na zenye uwezo mkubwa wa kutoa mavuno. Katika msimu wa 2015/2016, Serikali imetoa vocha milioni tatu za pembejeo za kilimo zikiwemo Tani 10,271 za mbegu bora za mahindi na mpunga na Tani 99,923 za mbolea ambazo zimesambazwa katika mikoa 24 ya Tanzania Bara na kunufaisha kaya 999,926. Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa hiyo kuhakikisha kuwa pembejeo hizo zinawafikia walengwa kwa wakati na zinatumika kama ilivyotarajiwa na kuwachukulia hatua wale wote watakaohujumu mpango huu.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo


42.         Mheshimiwa Spika, mwezi Agosti 2015, Serikali ilizindua Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu. Benki hiyo inatoa mikopo ya muda mfupi na muda mrefu kwa riba kati ya asilimia saba na 12 imeanza na mtaji wa Shilingi Bilioni 60. Mikopo inayotolewa na Benki hiyo inalenga kusaidia kugharamia uandaaji wa mashamba, ununuzi wa pembejeo za kilimo, usindikaji wa mazao pamoja na hifadhi ya mazao. Serikali itaendelea kuiongezea mtaji Benki hiyo ili ikopeshe wakulima wengi zaidi hasa kupitia vikundi vya wanawake na vijana vinavyojihusisha na kilimo. Benki hiyo itasimamia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 25 kwa ajili ya kudhamini mabenki ya biashara ili yaongeze ukopeshaji kwenye miradi ya miundombinu ya masoko na  kuendeleza ubunifu kwenye miradi ya maendeleo vijijini chini ya Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF). Vilevile, Benki hiyo itakuwa  Wakala wa Serikali wa kusimamia fedha za ruzuku ya pembejeo.

Miundombinu ya Masoko


43.         Mheshimiwa Spika, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inayotekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Programu hiyo inasaidia kuboresha miundombinu ya masoko, zikiwemo barabara na maghala ya kuhifadhia mazao; kuwawezesha wananchi waishio vijijini kuongeza thamani ya mazao ya kilimo; kuwajengea wananchi uwezo wa kuyafikia masoko na kupanua wigo wa huduma za kifedha vijijini.

44.         Mheshimiwa Spika, chini ya Programu hiyo katika mwaka 2015/2016, Serikali imekarabati barabara za vijijini zenye urefu wa kilomita 180 kwa kiwango cha changarawe zikiwemo kilomita 63.6 za Zanzibar. Aidha, imejenga maghala matano yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 1,000 za mazao kila moja na kuvijengea uwezo wa kufikia masoko vikundi 780, vikiwemo vikundi 101 vya Tanzania Zanzibar. Vilevile, imezijengea uwezo Asasi ndogo za Kifedha, zikiwemo SACCOs 291 na Benki tisa za Wananchi ili ziweze kutoa huduma endelevu za kifedha. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya masoko katika Halmashauri 38 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar. Aidha, itaendelea kuwajengea wazalishaji wadogo uwezo wa kuhifadhi na kusindika mazao, mbinu za kufikia masoko na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Mifugo


45.         Mheshimiwa Spika, tunayo fursa ya kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo kama tutawekeza kwenye viwanda vya kusindika nyama ili kuongeza thamani na kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali kutokana na mifugo iliyopo nchini.  Hali ilivyo sasa siyo nzuri kwani tunauza mifugo mingi nje ya nchi ikilinganishwa na nyama. Mathalan, katika mwaka 2015/2016 hadi kufikia mwezi Machi 2016, ng’ombe milioni 1.5, mbuzi milioni 1.2 na kondoo 253,243 wenye thamani ya Shilingi  Bilioni 976.5 waliuzwa nje ya nchi. Hii ina maana kuwa mazao kama ngozi, kwato na damu za wanyama hao, ambazo zingeweza kutumika kuzalisha bidhaa nyingine za viwandani, yamekwenda nje badala ya kutumika hapa nchini. Tunaweza kabisa kugeuza hali hii haraka kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani mifugo.  Nashauri wawekezaji binafsi kwenye sekta ya mifugo kuchangamkia fursa ya kufufua viwanda vya nyama vilivyopo  na kujenga vingine vipya ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, ni lazima tuanze kubadili fikra za wafugaji wetu ili ufugaji uwe na tija kwa kuwa na idadi ndogo ya mifugo yenye ubora wa kisasa na inayoendana na uwezo wa eneo la malisho. Serikali itaweka msisitizo wa kipekee katika kuboresha kosaafu za mifugo ili kuzalisha mifugo yenye tija kwa kusambaza ng’ombe bora kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa na nyama kutoka katika mashamba ya kuzalisha mifugo na kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo. Vilevile, juhudi za kudhibiti magonjwa ya mifugo yasiyokuwa na mipaka na yenye athari kubwa katika uchumi wa Taifa zitaongezwa. Serikali itaendelea kufanya tathmini ya uendeshaji wa ranchi za Taifa zilizobinafsishwa ili kuhakikisha kwamba wale waliopewa vitalu vya mifugo wanavitumia kwa mujibu wa mikataba ya mauzo au vinginevyo kuwanyang’anya na kuwapa wengine wenye uwezo.

Viwanda 


46.         Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuweka nguvu kubwa katika sekta ya viwanda ili kufikia lengo la kuwa Nchi ya uchumi wa viwanda. Azma hiyo imesisitizwa sana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Ili kufikia uchumi wa viwanda, kuanzia mwaka 2016/2017 jitihada kubwa itawekwa katika kutenga na kuendeleza maeneo maalum ya viwanda; kuweka miundombinu muhimu ya nishati, usafirishaji, maji na maghala. Aidha, tutaweka utaratibu  endelevu wa upatikanaji mitaji na teknolojia ikiwemo kuanzisha dirisha maalum katika Benki ya Maendeleo TIB na  Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Serikali pia itapitia mifumo ya kodi, tozo na taratibu mbalimbali kwa lengo la kuzipunguza na kuondoa urasimu ili kupunguza gharama za uzalishaji wa ndani na kuwezesha bidhaa zetu kushindana katika soko la ndani na kimataifa. Aidha, Serikali itaifanyia mapitio ya Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na Sheria yake ya mwaka 1997 ili kuendana na wakati.

Masoko


47.         Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa masoko ya uhakika unategemea mambo makuu manne. Ubora wa bidhaa au mazao; uhakika wa kupatikana kwa mazao au bidhaa wakati wote;  unafuu wa bei dhidi ya washindani wengine katika soko; na ufungashaji na ujenzi wa jina la bidhaa (branding). Hivyo, ni lazima mlolongo wote wa uzalishaji, uongezaji thamani na usafirishaji uwe mzuri kuwezesha uwepo wa soko la uhakika. Mtiririko huo katika mnyororo wa thamani wa bidhaa zenye uhakika wa soko ndio msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano na msingi wa kuhamasisha mapinduzi ya viwanda kwa lengo la kuongeza thamani bidhaa zetu kabla ya kuuzwa.  Msukumo mkubwa utawekwa katika uendelezaji na upatikanaji wa soko la ndani na nje kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan katika masoko ya upendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na masoko mengine ya kimkakati ya Kikanda na Kimataifa. Vivyo hivyo, uondoaji wa vikwazo vya kibiashara pamoja na kusimamia viwango na ubora wa bidhaa za ndani na nje ya nchi utaendelezwa. 

48.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2015/2016, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania zimekamilisha mkataba mwingine wa kutumia Soko la Marekani  bila ushuru chini ya Mpango wa AGOA, kwa kipindi kingine cha  miaka 10 kuanzia tarehe 30 Septemba, 2015 hadi 30 Septemba, 2025. Ni muhimu sana kutumia fursa hii mpya ya AGOA kufanya biashara na Marekani katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Vyama vya wafanyabiashara ni lazima viwaandae wanachama wao kupata taarifa kamili kuhusu bidhaa zinazohitajika na ubora unaotakiwa.  Aidha, Serikali itasimamia uzalishaji wa bidhaa bora kulingana na ubora unaotakiwa na masoko.

Madini


49.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uchimbaji madini mdogo kama kichocheo cha kuongeza ajira na kukuza kipato cha wachimbaji wadogo wa madini na wananchi wanaozunguka maeneo husika ya madini. Aidha, uchimbaji mdogo wa madini unachangia kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo, kuwapatia ruzuku na kutoa mafunzo ya kuwawezesha kutekeleza kazi zao kwa ufanisi na tija. Katika mwaka 2015/2016, Serikali ilitenga Hekta 7,731 kwa ajili ya uchimbaji madini mdogo katika maeneo ya Nyamongo (Tarime) na Muhintiri (Singida). Aidha, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB imetoa mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.2 kwa ajili ya kukuza mitaji ya wachimbaji wadogo. Pia mafunzo yametolewa kwa wachimbaji wadogo 1,520. Mikoo hiyo pia inaweza kutolewa kupitia benki ya TIB Corporate.

50.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itatenga zaidi maeneo tengefu kwa ajili ya uchimbaji madini mdogo na kuongeza kiasi cha ruzuku inayotolewa kwa Wachimbaji Wadogo. Serikali imetenga Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya ruzuku na Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni Tatu kuchangia kwenye ruzuku hiyo. Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi katika biashara ya madini ya Tanzanite na kutoa mwongozo mpya wa namna ya kuendesha uchimbaji madini mdogo kwa tija.  Mafunzo kuhusu namna ya kufanya utafiti wa awali wa madini na uchenjuaji bora wa madini yataendelezwa ili kazi za wachimbaji madini wadogo zifanyike kwa ufanisi na tija.

 

Utalii


51.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii ni moja ya sekta muhimu ambazo fursa zilizopo zikitumika vizuri zitasaidia sana kukuza ajira na kupunguza umaskini. Juhudi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali katika kuboresha huduma na miundombinu ya kitalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii zimeiwezesha Sekta ya Utalii  kuchangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 25 ya mapato yanayotokana na mauzo ya nje mwaka 2015. Aidha, mwezi Julai 2015 Serikali ilizindua Kampeni Maalum ya Kukuza Utalii wa Ndani ili kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo katika Hifadhi zetu. Kampeni hiyo imeongeza idadi ya watalii wa ndani kutoka watalii 115,913 mwezi Septemba 2014 hadi 148,406 Septemba 2015. Mafanikio hayo yanadhihirisha kwamba Sekta ya Utalii ikiboreshwa ina fursa nyingi za kuchangia Pato la Taifa na kuongeza ajira na kipato cha wananchi. Hata hivyo, unahitajika uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo hoteli, usafirishaji na rasilimali watu imara na yenye weledi katika kuwahudumia watalii wa ndani na nje.

52.         Mheshimiwa Spika, tunahitaji kufanya vizuri zaidi kwa kupanua vyanzo vya utalii na kuhakikisha fedha nyingi wanazotumia watalii kuja Tanzania zinalipwa hapa nchini badala ya utaratibu wa sasa wa malipo hayo kufanyika Nchi wanazotoka watalii. Tunahitaji pia kupanua na kuvutia utalii wa kihistoria na malikale kama vile miji mikongwe ya Kilwa, Mikindani, Bagamoyo na Mjimkongwe Zanzibar na vivutio vingine visivyo na mfano  Barani Afrika; kuliko kuegemea tu utalii wa wanyamapori na maliasili nyingine.  Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Utalii Nchini pamoja na kuendelea kutangaza vivutio maafufu kama Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Serengeti na Mapango ya Olduvai.

Kudhibiti Ujangili


53.         Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inakabiliwa na tatizo la ujangili hasa wa tembo, faru na biashara haramu ya nyara za Serikali. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilizindua Mkakati wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya Nyara za Serikali ulioanza kutekelezwa mwaka 2015, kwa kuchukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kutumia vifaa na teknolojia ya kisasa kama vile “Geographical Information System - GIS” na “Global Positioning System - GPS”; kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya radio kutoka mfumo wa analogia kwenda kidigitali; na kuanza kutekeleza Mpango wa Kikanda wa kukusanya taarifa za kiintelijensia zinazoongoza doria katika kukamata watuhumiwa na wahalifu.

54.         Mheshimiwa Spika, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Mkakati huo hususan kwa kuzingatia ukubwa wa changamoto ya vitendo vya uwindaji haramu vinavyofanywa na majangili kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa Idara ya Wanyamapori wasio waaminifu na baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mapori. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba ujangili huu unakomeshwa haraka. Nichukue fursa hii kuziomba jamii zinazozunguka hifadhi zetu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali katika vita hii.

HUDUMA ZA KIUCHUMI


Ardhi


55.         Mheshimiwa Spika, ili azma yetu ya kufanya mapinduzi ya viwanda ifanikiwe, inahitajika ardhi iliyopimwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Changamoto tuliyonayo hivi sasa ni kwamba sehemu kubwa ya ardhi yetu haijapimwa na kupatiwa hatimiliki. Hivyo, tumeanza kuchukua hatua za haraka zitakazowezesha kupatikana kwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa walishaagizwa kutenga maeneo ya viwanda na biashara katika Mipango Miji. Napenda kutumia fursa hii kuitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutopitisha maombi yoyote ya Mipango Miji yasiyokuwa na maeneo ya Viwanda na Biashara. Nimefarijika kuona kwamba chini ya Mpango wa Maeneo Huru ya Biashara, baadhi ya mikoa imeshatenga ardhi ambayo itaweza kuanza kutumika mara moja kutekeleza Mpango huo kwa kuwekewa miundombinu muhimu na kukamilisha upimaji. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji zishirikiane kufanya uhakiki wa haraka wa maeneo hayo ili wawekezaji watakaoonesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda wapatiwe maeneo yenye hatimiliki kwa haraka.

56.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba kuna migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo nchini.  Migogoro hiyo, wakati mwingine imesababisha uharibifu wa mali, majeruhi na mauaji ya binadamu na mifugo. Njia muafaka ya kudhibiti migogoro hiyo ni kupima kila kipande cha ardhi, kukimilikisha kwa mtumiaji kwa kumpatia hatimiliki na kusimamia matumizi yake. Kwa kutambua hilo, mwezi Februari 2016, Serikali ilizindua Programu ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi (Land Tenure Support Programme) ambayo imeanza kutekelezwa kwa majaribio katika Wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi mkoani Morogoro. Programu hiyo imelenga kuongeza kasi ya kupima ardhi na kutoa hakimiliki za kimila ambazo zinaweza kutumika kama dhamana kwa wakulima na wafugaji kupata mikopo; kupunguza au kuondoa migogoro ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi; na kuhifadhi kumbukumbu za ardhi kwa matumizi sahihi ya rasilimali hiyo.  Programu hiyo itatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu kwa gharama Dola za Marekani Milioni 15.2. Baada ya majaribio hayo, na mafanikio kuonekana katika wilaya hizo, Programu itatekelezwa katika wilaya zote nchini. Ninawaagiza viongozi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya zinazohusika, kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Programu hiyo kwani matokeo yake ni ya muhimu sana kwenye mustakabali wa upimaji na matumizi endelevu ya ardhi yetu.

57.         Mheshimiwa Spika, mwaka 2015, Serikali iliwaomba Waheshimiwa Wabunge kuainisha na kuwasilisha Serikalini migogoro ya ardhi iliyopo kwenye majimbo yao. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge walioitikia wito huo. Mchango wao katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, umewezesha jumla ya migogoro 1,130 ya ardhi kupokelewa Serikalini kutoka katika Halmashauri zote nchini. Uchambuzi wa migogoro hiyo unaendelea ambapo taarifa za awali zinaonesha kwamba migogoro mingi iliyopo ni kati ya wakulima na wafugaji, uvamizi wa mashamba na viwanja, migogoro kati ya Mamlaka za Hifadhi za Taifa na wananchi na kati ya wawekezaji na wananchi.

58.         Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, tayari Serikali imechukua hatua kali dhidi ya maafisa ardhi waliokiuka sheria na taratibu za usimamizi wa ardhi nchini. Hii ni pamoja na kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Kwa mfano, hatua kali zimechukuliwa katika Halmashauri za Majiji ya Mwanza na Arusha, Manispaa za Bukoba na Kahama na kutengua madaraka kwa afisa ardhi mteule wa Manispaa ya Temeke.  Ninaendelea kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kushirikiana na Halmashauri zao hususan Maafisa Ardhi na kutumia Dawati Maalum la Kuratibu Migogoro ya Ardhi lililoanzishwa katika kila Halmashauri nchini ili kuendelea kubaini migogoro iliyopo na kuitafutia ufumbuzi.

59.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaifanyia mapitio Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ili kuweka vipengele muhimu vya kudhibiti migogoro baina ya watumiaji wa ardhi na kuunda na kuzipa nguvu zaidi Ofisi za Ardhi za Kanda zitakazosaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kupima na kupanga matumizi ya ardhi na kutoa hati karibu zaidi na wananchi. Aidha, Serikali itapitia upya Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 ili kuzifanyia marekebisho muhimu kuendana na wakati.

 

Barabara


60.         Mheshimiwa Spika, miundombinu imara ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta nyingine zote, ikiwemo Sekta ya Viwanda na Biashara. Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara nchini. Mathalan katika mwaka 2015/2016, Serikali  ililenga kujenga kilometa 523 za barabara kuu kwa kiwango cha lami. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016, jumla ya kilometa 414.3 za barabara zilikuwa zimekamilishwa kwa kiwango cha lami, sawa na asilimia 79 ya lengo lililowekwa. Aidha, jumla ya kilometa 82.4 za barabara kuu zilikarabatiwa kwa kiwango cha lami, ikiwa ni sawa na asilimia 73 ya lengo la kilometa 113. Kwa upande wa barabara za mikoa, jumla ya kilometa 52.19 zilijengwa kwa kiwango cha lami, sawa na asilimia 68 ya lengo la kilometa 77 na jumla ya kilometa 676 za barabara za mikoa zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe, sawa na asilimia 54 ya lengo la kilometa 1,252. Ujenzi wa madaraja makubwa 11 uliendelea ambapo Daraja la Kigamboni limekamilika na kufunguliwa rasmi.

Reli


61.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu na Huduma za Reli ya Kati, lengo likiwa ni kuboresha reli iliyopo kwa kutandika reli mpya na nzito zaidi; kuimarisha matuta, mifereji na tabaka la kokoto. Aidha, tunaendelea na  utekelezaji wa makubaliano baina ya Serikali yetu na Serikali za Rwanda na Burundi kuhusu ujenzi wa reli ya Dar es Salaam – Isaka – Keza - Kigali (Km. 1,464); na Keza – Musongati (Km. 197) kwa kiwango cha Standard Gauge. Mkakati wa ndani ni pamoja na kujenga reli ya Standard Gauge kuanzia Dar es Salaam –Kigoma yenye matawi mawili ya Kaliua-Mpanda-Karema na …..(Haijamalizika NB Nasubiri HANSARD)

Bandari


62.         Mheshimiwa Spika, katika  mwaka 2015/2016, Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha ufanisi wa bandari zetu kwa kuanzia na Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu la biashara katika Afrika Mashariki na Kati na kufuatiwa na Bandari za Mtwara na Tanga. Tumeanza kwa kuondoa watumishi wote wasio waaminifu ambao wanachangia kupoteza mapato ya Serikali yanayohitajika sana katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi wetu. Vilevile, tumefanya kazi kubwa ya kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa kuhakikisha  kwamba malipo yote yanafanyika benki na kuoanisha mifumo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania.  Niwahakikishie wananchi na wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma katika bandari zetu na hususan Bandari ya Dar es Salaam kwa kupunguza idadi ya siku za kutoa mizigo bandarini li tufikie siku mbili au chini ya siku hizo. Aidha, tutaziondoa kero zote zilizoainishwa na Mawakala wa Forodha nilipokutana nao tarehe 21 Machi, 2016 Jijini Dar es Salaam. Vilevile, Serikali itaziba mianya yote ya upotevu wa mapato bandarini na wale wote watakaobainika kushiriki kwenye wizi wa aina yoyote wataondolewa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

Mawasiliano


63.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukamilisha mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchini ikiwemo ujenzi wa Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu katika Jiji la  Dar es Salaam. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ambapo hadi sasa tumefanikisha ujenzi wa kilometa 18,000 kati ya kilometa 20,000 za miundombinu ya mkongo katika wilaya zote nchini. Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika vijiji 4,000 visivyokuwa na mawasiliano, kuunganisha Ofisi zote za Wakuu wa Wilaya, Hospitali za Wilaya, Mahakama, Vituo vya Polisi vya Wilaya, Ofisi za Posta na kuziwesha shule 431 kupata huduma ya intaneti bila malipo.

Nishati

(a)Umeme


64.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika, unaokidhi mahitaji na wenye gharama nafuu ili kusukuma mapinduzi ya viwanda kwa kasi zaidi. Ili kutekeleza azma hiyo, katika mwaka 2015/2016, Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme kutoka Megawati (MW) 1,226.24 mwaka 2015 hadi kufikia MW 1,516.24 mwezi Januari 2016, sawa na ongezeko la Asilimia 24.  Ongezeko hilo limetokana na uamuzi sahihi wa Serikali wa kutekeleza mradi mkubwa wa  ujenzi wa Bomba la Gesi pamoja na mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi-I wenye uwezo wa kuzalisha MW 150.  Mradi huo baadaye utapanuliwa na kuweza kufikia MW 335 ifikapo mwaka 2017/2018. Sambamba na hatua hiyo, tarehe 16 Machi 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo kingine cha Kinyerezi-II cha kufua umeme kutokana na gesi asilia ambao utakapokamilika utazalisha MW 240. Lengo la Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme hadi kufikia MW 4,915 na hivyo, kuwezesha asilimia 60 ya watanzania kupata umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2020 na kutekeleza ipasavyo azma ya kuongeza uwekezaji mkubwa kwenye viwanda.

65.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2015/2016, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kusambaza na kuunganisha umeme kwa wananchi waishio vijijini.

Katika kipindi hicho, idadi ya wananchi waliopata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Pili ni 71,724 katika vijiji 1,669. Aidha, hadi mwezi Januari, 2016 Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 12,193 za njia za msongo wa kati na kilometa 1,830 za msongo mdogo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Usambazaji wa Umeme Vijijini. Vilevile, umeme umefikishwa kwenye Makao Makuu ya Wilaya mpya 12 za Buhigwe, Busega, Chemba, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Mkalama, Mlele, Nyasa, Nanyumbu na Uvinza. Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza kiwango cha wananchi wanaopata huduma ya umeme kufikia asilimia 40.

66.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Kinyerezi-II pamoja na  kuimarisha na kujenga njia za usafirishaji umeme katika Gridi ya Taifa za Msongo mkubwa wa kiloVolts 400 kutoka Iringa kupitia Dodoma na Singida hadi Shinyanga na kutoka Dar-es-Salaam kupitia Chalinze na Tanga hadi Arusha pamoja na mradi wa kiloVolts 220 kutoka Makambako hadi Songea. Aidha, Serikali itakamilisha Awamu ya Pili ya mradi wa usambazaji umeme vijijini na kuanza utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya miradi ya REA.

(b) Gesi Asilia na Mafuta


67.         Mheshimiwa Spika, baada ya ugunduzi mkubwa wa Gesi Asilia nchini, mikakati ya Serikali inayoendelea ni kubuni miradi mbalimbali hasa ile itakayoendeshwa na wafanyabiashara wazawa ili rasilimali hiyo iweze kuwanufaisha Watanzania na kuwawezesha kumiliki uchumi wa Taifa lao. Serikali imetenga eneo la ardhi huko Likongo Mkoani Lindi kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kuchakata Gesi Asilia ikiwa ni sehemu ya kutekeleza azma hiyo ya kuwawezesha wazawa. Serikali itaanza utekelezaji wa mradi huo katika mwaka 2016/2017.

68.         Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba Nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta kwa ushindani na gharama nafuu, Serikali imeanzisha Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja yaani Petroleum Bulk Procurement Agency, ulioanza kazi rasmi mwezi Januari, 2016. Utaratibu huo utaiwezesha Serikali kusimamia vizuri udhibiti wa uagizaji wa mafuta nchini na kuwawezesha Wananchi kuwa na uhakika wa kupata mafuta bora yenye viwango vinavyokubalika kimataifa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na kijamii.

HUDUMA ZA JAMII


Elimu


69.         Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa elimu kama nyenzo imara ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuboresha na kuimarisha elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu  ya juu. Hatua zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha kwamba  elimu ya Tanzania ni ya viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana wetu kukabiliana na changamoto za maisha kwa kujiari wenyewe na kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani, kikanda na kimataifa. Aidha, hatua hizo zitatuwezesha kuwa na rasilimali watu yenye weledi wa kutosha kujenga uchumi wa viwanda nchini. Moja ya hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ni utekelezaji wa ahadi ya utoaji wa elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kwa shule za umma kuanzia mwezi Januari 2016. Ahadi hiyo ilitolewa na mgombea Urais kupitia CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2015 ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, ni matakwa ya Kifungu cha 52(a) cha Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 ambacho kinasisitiza kwamba Serikali itaandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na elimumsingi bila malipo ili kila Mtanzania apate fursa sawa ya kupata elimu.

70.         Mheshimiwa Spika, naamini kabisa kuwa hatua hiyo nzuri iliyochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, itawapunguzia wazazi na walezi hasa wananchi maskini mzigo wa kugharamia elimu ya vijana wao. Kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015, Serikali imefuta michango ya maji, umeme, ulinzi, mitihani na ada iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa idhini ya Kamati na Bodi za Shule.  Hata hivyo, yapo majukumu yanayohusu mahitaji ya msingi ya mtoto ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi kama ilivyokuwa inafanyika awali. Majukumu hayo ni  pamoja na kumnunulia mtoto sare za shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa kwa utaratibu utakaowekwa na wazazi na walezi wenyewe. Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule mwanafunzi na mahitaji mengine kama vile kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Vilevile, mzazi au mlezi ana wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake. 

71.         Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo, kumejitokeza changamoto kadhaa. Baadhi ya changamoto hizo ni uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa kuweka utaratibu muafaka wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa mabweni ambayo wazazi na walezi au jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula. Changamoto nyingine ni pamoja na upungufu wa miundombinu kama madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na vyoo. Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo na jitihada kubwa zimewekwa katika kuielimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mpango mzima wa utoaji elimu bila malipo.

72.         Mheshimiwa Spika, tunayo changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule bila malipo. Hili ni jambo kubwa na tulishatoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha kuwa kila Halmashauri inatumia rasilimali zake kutengeneza madawati kwa kila shule. Nitumie nafasi hii kuwashukuru wadau walioanza kuchangia madawati katika maeneo mbalimbali na ninawasihi wengine waendelee kuunga mkono jitihada hizi za Serikali. Kuanzia leo hii, nawaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waliokamata mbao ndani ya Halmashauri zao kuzitumia kutengenezea madawati na siyo kuzipiga mnada. Natumia nafasi hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Watendaji wa Bunge kwa Mkakati wa kubana matumizi uliowezesha kupata Shilingi Bilioni sita zitakazotumika kutengeneza madawati. SUMA JKT na Magereza wameanza kazi ya kutengeneza madawati hayo. Tunatarajia kupata madawati 80,000 ambayo tutawagawia Wabunge wa Majimbo yote na kwa wastani kila Jimbo litaweza kupata madawati 300.

73.         Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika juhudi za kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila malipo.  Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu kushirikiana katika kuwaelimisha wananchi kuhusu mpango huu na wajibu wa kila mmoja wetu katika kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata fursa za kupata elimu bora. Tukifanya hivyo, tutaweza kufikia lengo letu la kuwa Nchi yenye uchumi wa kipato cha kati kwa haraka zaidi.

74.         Mheshimiwa Spika, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu ya kuwapatia ujuzi na kuwajengea uwezo na uzoefu wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari. Uzoefu wa Nchi za Asia zilizowekeza katika elimu ya ufundi na ufundi stadi unaonesha kwamba maendeleo ya haraka waliyoyapata na hususan kufikia uchumi wa kati na wa viwanda umechangiwa sana na elimu ya ufundi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali itaelekeza nguvu zake katika kujenga na kuimarisha miundombinu ya elimu ya ufundi na kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya sasa ya uchumi wa viwanda. Kwa kuanzia, Serikali imeridhia vyuo vya maendeleo ya wananchi kuhamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na kufanyiwa ukarabati kwa ushirikiano na Sekta Binafsi ili viweze kutoa mafunzo ya ufundi. Hatua hiyo itaharakisha kufikiwa kwa lengo la Serikali la kuwa na chuo cha ufundi kwa kila Wilaya.

75.         Mheshimiwa Spika, udahili katika vyuo vya elimu ya juu umeongezeka kutoka wanafunzi 214,722 mwaka 2014 hadi kufikia wanafunzi 220,531 mwaka 2015.  Aidha, hadi kufikia Februari 2016, idadi ya wanafunzi waliopewa mikopo ya elimu ya juu ilifikia 122,886.  Kiasi cha fedha za mikopo kilichotolewa kwa wanafunzi hao ni Shilingi Bilioni 207. Hata hivyo, hali ya urejeshaji wa mikopo iliyotolewa hairidhishi. Hivyo, naiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kufuatilia urejeshaji wa mikopo hiyo ili fedha hizo zitumike kuwakopesha wanafunzi wengine.

 

Afya


76.         Mheshimiwa Spika, uimarishaji wa huduma za afya nchini, kwa maana ya kinga na tiba ni muhimu sana. Nguvukazi yenye afya njema hutoa mchango mkubwa kwenye uchumi ikilinganishwa na nguvukazi dhaifu kiafya. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za kinga, uchunguzi na upatikanaji wa dawa na vifaa-tiba katika  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalum, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati. Aidha, Serikali imetoa maelekezo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kufungua na kuendesha maduka ya dawa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Wilaya ili kuhakikisha kwamba dawa za kutosha zinapatikana wakati wote na kwa bei nafuu.

77.         Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Bohari Kuu ya Dawa imefungua na inaendesha maduka ya dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu ndani ya maeneo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Sekou Toure (Mwanza), Mawenzi (Kilimanjaro) na Mount Meru (Arusha). Pamoja na juhudi hizo za Serikali za kuimarisha huduma za afya nchini, milango ipo wazi kwa sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya afya.

78.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za Bima ya Afya ili kuongeza na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya afya kwa watu wote. Idadi ya wanufaika wa Bima ya Afya tangu kuanzishwa kwake ni 11,729,281, sawa na asilimia 27 ya watanzania wote kulingana na Sensa ya mwaka 2012. Kati ya hao, wanufaika 8,390,550 wako katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na 3,338,755 ni wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hata hivyo,  idadi ya wanufaika wa Bima bado ni ndogo, hivyo naagiza viongozi wa Mifuko hiyo kushirikiana pamoja kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na Mifuko hiyo. Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili Katibu Tawala wa Mkoa aratibu maendeleo ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati.

Maji


79.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya maji safi, salama na ya kutosha. Hadi kufikia Desemba 2015, Serikali imefikisha huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 72 katika maeneo ya vijijini, asilimia 86 miji mikuu ya mikoa na asilimia 60 katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo. Mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa miradi ya maji 1,143 kati ya miradi 1,855 ya maji mijini na vijijini ambayo imetekelezwa chini ya Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha, huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na miji ya Bagamoyo na Kibaha imeongezeka na kufikia asilimia 68, lengo likiwa kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itatekeleza Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji pamoja na kukamilisha miradi 712 ambayo haikutekelezwa katika Awamu ya Kwanza. Natoa wito kwa wananchi wote kutunza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yake ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji vijijini na mijini.

80.         Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba maji ni moja ya vigezo muhimu katika kuanzisha na kuendeleza viwanda. Hivyo hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji nchini, pamoja na kuongeza huduma ya maji safi na taka, ina lengo la kuongeza mchango wa Sekta ya Maji katika Sekta ya Viwanda. Mathalan, ongezeko la maji kutokana na utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya maji ya  Ruvu Juu na Ruvu Chini umesaidia kupunguza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam. Serikali itahakikisha kuwa maeneo yenye viwanda na yanayotegemewa kuwa na viwanda yanaunganishwa na miradi mikubwa ya maji ili kuongeza kasi ya uzalishaji.

SHERIA, ULINZI NA USALAMA


Sheria


81.         Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuona kwamba kero ya mlundikano wa mashauri Mahakamani inakuwa historia na kwamba wananchi wanapata haki kwa wakati. Katika kufanikisha dhamira hiyo, Serikali imeimarisha utendaji wa Mhimili wa Mahakama kwa kuongeza rasilimali watu na fedha. Aidha, Serikali imeboresha na kuongeza ufanisi katika upelelezi na uendeshaji wa mashauri kwa kutenganisha jukumu la upelelezi na uendeshaji wa mashauri. Vilevile, uongozi wa Mahakama umejiwekea utaratibu wa Majaji na Mahakimu kuwa na malengo ya idadi ya mashauri ambayo wanapaswa kuyasikiliza kila mwaka. 

82.         Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa majengo ya Mahakama na vitendea kazi katika ngazi zote, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametekeleza ahadi yake aliyoitoa tarehe 4 Februari 2016 ya kutoa fedha zote za maendeleo za Mahakama kiasi cha Shilingi Bilioni 12.3 kwa mwaka 2015/2016.  Hatua hiyo imeiwezesha Mahakama kuendelea na ukarabati na ujenzi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali na pia ununuzi wa vitendea kazi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huo.

83.         Mheshimiwa Spika, wakati akihutubia Bunge lako Tukufu mwezi Novemba, 2015 Mheshimiwa Rais aliahidi kuwa katika mwaka 2016/2017, Serikali itaanzisha Mahakama Maalum ya Ufisadi. Napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai 2016. Aidha, Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki.

Ulinzi na Usalama


84.         Mheshimiwa Spika, vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea na jukumu la kulinda mipaka, raia na mali zao. Kwa jumla, hali ya ulinzi na usalama wa Nchi yetu ipo shwari. Napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi yao nzuri, weledi na uzalendo wa hali ya juu katika kuhakikisha Taifa letu lina usalama wa kutosha pia kuchangia usalama wa mataifa mengine duniani yenye migogoro ya kisiasa. Mambo yote haya yanatokana na ukweli kwamba Serikali imekuwa ikiviwezesha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuwa na uwezo wa kulinda mipaka ya Nchi, raia na mali zao. Katika kujenga utayari wa Majeshi wakati wote, askari wetu wameshiriki kwa ufanisi katika majukumu ya kimataifa ya kulinda amani katika Nchi zenye migogoro duniani, hususan Darfur, Sudan, Lebanon na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

85.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, jumla ya vijana 27,463 walipatiwa mafunzo ya kujenga uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa pamoja na stadi za kazi na za kimaisha. Kati yao, vijana 7,517 ni wa kujitolea na 19,946 ni wa mujibu wa sheria. Ni jambo la kutia moyo kwamba vijana 5,453 waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa wamenufaika na utaratibu wa kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya hao, Vijana 3,521 wameajiriwa na JWTZ; Polisi 1,185; Usalama wa Taifa 106, Takukuru vijana 24 na Jeshi la Zimamoto vijana 617.

Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kuishi kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama ambapo ujenzi wa nyumba 4,744 za makazi zimekamilishwa kati ya nyumba 6,064 za awamu ya kwanza kwenye mradi wa nyumba 10,000 zinazotarajiwa kujengwa Nchi nzima.

86.         Mheshimiwa Spika, Serikali italiimarisha Jeshi letu kwa kulipatia mafunzo, zana bora na za kisasa zaidi; kuboresha mazingira ya kufanyia kazi; na maslahi. Aidha, itaimarisha uwezo wa Jeshi katika utafiti na kuendeleza teknolojia kwa madhumuni ya kuongeza ubunifu katika kuzalisha bidhaa bora zaidi na huduma kwa ajili ya matumizi ya jeshi na raia nchini na nje ya nchi. 

Udhibiti wa Uhalifu Nchini


87.         Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kulinda usalama wa raia na mali zao na kudumisha amani na utulivu nchini. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2015, jumla ya makosa makubwa ya jinai 68,814 yaliripotiwa katika Vituo vya Polisi kote nchini ikilinganishwa na makosa 70,153 yaliyoripotiwa katika  kipindi kama hicho mwaka 2014, sawa na upungufu wa asilimia 1.9. Upungufu huo wa makosa umetokana na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wananchi katika vita dhidi ya uhalifu na kuongezeka kwa taarifa za kiintelijensia. Aidha, Jeshi limeimarisha doria za Nchi kavu na majini pamoja na kufanya misako na operesheni maalum kwa ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata na Shehia. Katika mwaka 2016/2017, Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu ya Ulinzi Shirikishi kwa wananchi ili waweze kuongeza ushirikiano na Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa jukumu la kupambana na uhalifu. 

MICHEZO


88.         Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa michezo katika kuimarisha  afya, kuongeza ajira, kujenga udugu na mshikamano miongoni mwa jamii na mataifa mbalimbali duniani, Serikali itaendelea kuimarisha michezo nchini ili wanamichezo wetu waweze kufanya vizuri katika medani za michezo ndani na kimataifa. Katika kufikia azma hiyo, mwaka 2016/2017, Serikali  itakamilisha mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 na kuendelea kutoa mafunzo ya michezo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari ili kuibua vipaji. Serikali pia itaendelea kusimamia maendeleo ya michezo katika shule, vyuo, taasisi na vilabu. Lengo ni kuhakikisha kuwa michezo inatoa fursa kwa vijana kupata ajira na kuendeleza vipaji vyao.

HABARI


89.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba Sekta ya Habari ni nguzo muhimu katika kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha umma. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kusimamia Sekta ya Habari kikamilifu na kuhakikisha vyombo vya habari vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili na Weledi. Uhuru wa vyombo vya habari ni mkubwa na wigo wa  ushiriki wa Sekta Binafsi umeongezeka sana. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016 Serikali ilikuwa imesajili Vituo vya Televisheni 26, Vituo vya Redio 126 na Magazeti 833. Muhimu hapa ni matumizi mazuri ya kalamu na kuweka uzalendo wa Nchi mbele.

90.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa vyombo vya Habari. Aidha, itaboresha Idara ya Habari- Maelezo ili itimize jukumu lake kama Msemaji Mkuu na Mratibu wa Mawasiliano Serikalini. Vilevile, itaendelea kufuatilia kwa karibu maudhui ya vituo vyote vya utangazaji kupitia mtambo maalum wa ufuatiliaji wa maudhui na kuhakikisha vituo vya utangazaji vinakuwa na wakalimani wa lugha ya alama. Napenda nitumie fursa hii kuvitaka vyombo ya habari nchini, kufanya kazi zake kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo, mambo ambayo ni muhimu sana katika tasnia ya habari kama wafanyavyo wenzao katika Nchi zote duniani yaani uzingatiaji wa maadili katika tasnia ya habari. Aidha, niwaombe wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari kutanguliza uzalendo wa Nchi yao mbele.

MASUALA MTAMBUKA


Lishe


91.         Mheshimiwa Spika, lishe bora ni nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye rasilimali watu wenye afya bora na uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya kazi. Ukosefu wa lishe bora husababisha utapiamlo ambao una madhara makubwa kiuchumi na kijamii kwa kaya, jamii na Taifa kwa ujumla. Hali hiyo ikitokea ndani ya kipindi cha siku 1,000 kuanzia ujauzito hadi miaka miwili ya ukuaji wa mtoto husababisha udumavu ambao madhara yake hayawezi kurekebishwa katika maisha yake yote. Udumavu unaathiri mwili na akili ya mtoto na hivyo hawezi kujifunza vizuri darasani na pia hupunguza uwezo wake katika kuchangia maendeleo ya Taifa lake hapo baadaye.
92.         Mheshimiwa Spika, athari nyingine za utapiamlo ni pamoja na watoto kuugua mara kwa mara, hali inayochangia ongezeko la gharama za matibabu kwa familia, jamii na Taifa; na wazazi kutumia muda mwingi kuuguza watoto badala ya kufanya shughuli za kukuza uchumi. Hali hiyo inatutaka sote tuwe mabalozi wa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa lishe bora. Vilevile, ni muhimu kwa wajawazito kuhudhuria kliniki ili kuchunguzwa afya zao na pia kupata ushauri wa kitaalam utakaowawezesha  kupata watoto wenye afya njema. Wakina mama waelimishwe kunyonyesha watoto wao kwa kipindi kisichopungua miezi sita mfululizo na kuwapatia vyakula vyenye viini lishe vya kutosha baada ya hapo. Masuala haya yanahitaji elimu zaidi kwa sababu vyakula hivyo vinapatikana kwenye jamii na kaya zetu na siyo ghali kuvipata.

Vita Dhidi ya Rushwa


93.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupambana na rushwa kwa kuchunguza tuhuma za rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria. Katika mwaka 2015/2016, Serikali imeshughulikia tuhuma 3,911 ambapo uchunguzi wa tuhuma 324 ulikamilika. Kati ya tuhuma hizo, majalada 252 yaliombewa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 156 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani. Aidha, Majalada 329 yaliyotokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yalichunguzwa. Majalada 19 yalikamilika na kuombewa kibali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 12 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Vilevile, majalada nane yaliyohusu tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Kati ya hayo, majalada mawili yamepata kibali na watuhumiwa wamefikishwa Mahakamani.

94.         Mheshimiwa Spika, Miradi ya Maendeleo 284 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 41.63 ilikaguliwa kupitia ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo katika Serikali za Mitaa. Miradi 69 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 8.32 ilibainika kuwa na kasoro ambapo miradi 10 wahusika walishauriwa namna ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati miradi 59 uchunguzi wa kina umeanzishwa ili wahusika wachukuliwe hatua. Aidha, ufuatiliaji maalum wa miradi ya afya inayofadhiliwa na Benki ya Dunia unaendelea kufanyika ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na kasoro, ikiwemo kuanzisha uchunguzi wa awali ambapo majalada 85 yamefunguliwa.

95.         Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa. Aidha, itawajengea uelewa wa masuala ya rushwa makundi mbalimbali katika jamii na hususan Asasi za Kiraia, madhehebu ya dini na wanahabari ili washiriki kikamilifu kuwaelimisha wananchi kuhusu kudhibiti rushwa na kuendelea kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuendelea kujenga jamii inayochukia rushwa.

Kudhibiti UKIMWI


96.         Mheshimiwa Spika, maambukizo mapya ya Virusi vya UKIMWI yanaendelea kupungua kutoka asilimia 5.7 mwaka 2008 hadi 5.1 kwa takwimu za 2011/2012. Vifo vitokanavyo na UKIMWI navyo vimeendelea kupungua kutoka wastani wa vifo 79,338 mwaka 2012/2013 hadi vifo 50,219 mwaka 2014/2015. Maambukizi mapya ya UKIMWI nayo yamepungua kutoka wastani wa 78,843 mwaka 2012/2013 hadi 69,000 mwaka 2014/2015. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI inakadiriwa kuwa milioni 1.4 kwa mwaka 2012/2013 na watu milioni 1.5 mwaka 2014/2015.

97.         Mheshimiwa Spika, pamoja na kupungua kwa kasi ya maambukizi, UKIMWI bado ni tishio linaloathiri maendeleo na maisha ya wananchi. Hatuna budi kuendelea kuchukua hatua za dhati na madhubuti za kudhibiti maambukizi mapya, kutoa huduma za afya na matibabu kwa wale walioambukizwa na kuwahudumia wale wenye mahitaji kutokana na vifo vya wazazi hususan watoto yatima. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018 unaolenga kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 50, kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI na kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI  ifikapo 2018.

98.         Mheshimiwa Spika, huduma za upimaji wa virusi vya UKIMWI  na uingizwaji  kwenye mpango wa matunzo na matibabu kwa wale wanaogundulika na  maambukizi ya VVU zinaendelea kutolewa. Jumla ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanaopata dawa za ARV ni 640,084, sawa na asilimia 43 ya watu wote wenye maambukizi. Kati yao, asilimia 69 ni wanawake na watoto. Serikali imeanza utaratibu mpya wa kutoa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa yeyote atakayepimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI tofauti na utaratibu wa awali ambao mwathirika alianzishiwa dawa kutegemea idadi ya CD4. Utaratibu huo umeanza katika Halmashauri 48 zenye kiwango kikubwa cha maambukizi na hatimaye kueneza huduma hii Nchi nzima. Katika juhudi za kupunguza maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Serikali imeendelea kutoa huduma katika vituo 5,361 kati ya 5,863 vinavyotoa huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini. Vilevile, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma katika masuala ya VVU, UKIMWI, Afya ya Uzazi na Ujinsia. Kuanzia mwezi Julai 2016, Serikali itaanza zoezi la kupima kiwango cha maambukizi kwa Nchi nzima, kila Mkoa, ikiwa ni mara ya nne zoezi hili kufanyika nchini.

Hifadhi ya Mazingira


99.        nbsp; Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka na kutekeleza mipango na mikakati thabiti ya kutunza mazingira kwa lengo la kutunza vyanzo vya maji, Bioanuai, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na uharibifu wa misitu. Aidha, Serikali imeandaa Kanuni mpya ya Mifuko ya Plastiki ya mwaka 2015 inayokataza kuzalishwa na kuingizwa nchini matumizi ya mifuko ya plastiki yenye unene chini ya mikroni 50. Vilevile, Serikali imeendelea kufanya kaguzi katika maeneo mbalimbali ili kubaini iwapo sheria za mazingira zinazingatiwa na kuchukua hatua za kuvifungia viwanda tisa na kutoa onyo kwa viwanda 63. Taasisi zinazohusika na usimamizi wa Sheria ya Mazingira  hazina budi kuvisaidia kiufundi viwanda husika ili visifungwe kwa muda mrefu kwani ni hasara kwa Taifa.

100.       Mheshimiwa Spika, wakati wa maadhimisho ya 54 ya Uhuru, tarehe 9 Desemba, 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alifanya uamuzi wa busara wa kuwataka wananchi wote kuyatumia maadhimisho hayo kwa kufanya usafi  wa mazingira katika maeneo yao yanayowazunguka na maeneo  ya Taasisi za Umma.  Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati wananchi wote, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi na Asasi za kiraia kwa mwitikio mkubwa waliouonesha katika kushiriki na kufanikisha zoezi hilo la usafi.

101.              Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa usafi wa mazingira, Serikali imeamua kwamba zoezi la usafi wa mazingira litakuwa endelevu. Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, tayari zimetoa Waraka maalum wa kuifanya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku maalum ya wananchi wote kufanya usafi wa mazingira nchini kote. Napenda kuwahimiza Viongozi na Watendaji wote wa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma na Sekta Binafsi,  Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini pamoja na Watendaji wa Mitaa, Kata na Vijiji na Vitongoji na Wakuu wa Kaya kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao. Aidha, nawasihi Wananchi wote kudumisha utamaduni na tabia nzuri ya kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa safi wakati wote ili kuboresha afya zao na kuleta maendeleo endelevu nchini.

Menejimenti ya Maafa

           
102.              Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza jukumu la kuwalinda na kuwasaidia wananchi dhidi ya maafa yaletwayo na matukio mbalimbali ya kiasili. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Serikali kutoa Tani 31,184 za chakula kwa halmashuri 69 zilizokumbwa na tatizo la upungufu wa chakula katika mwaka 2015/2016. Kati ya hizo, Tani 7,727 zilitolewa bure kwa kaya zisizo na uwezo na Tani 23,457 zilitolewa kwa bei nafuu ya Shilingi 50 kwa Kilo.

103.              Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa misaada mbalimbali ya kibinadamu yenye thamani ya Shilingi Milioni 42.5  na kiasi cha Shilingi Milioni 143.5 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu za mihogo na mtama kwa waathirika wa maafa ya mafuriko, mvua ya mawe na upepo mkali. Mikoa iliyopata misaada hiyo ni Mtwara, Mara, Dodoma, Shinyanga, Iringa, Tanga, Pwani, Lindi na Tabora. Pia Shilingi Milioni 516 zilitolewa kama fidia kwa watu waliotakiwa kupisha ujenzi wa upanuzi wa mtaro katika eneo la Buguruni - Mnyamani.  Serikali imeimarisha Mfumo wa Upatikanaji wa Taarifa za Tahadhari za majanga kwa haraka kwa kujenga vituo 16 vya upimaji wa hali ya hewa na kuweka vifaa vya kupima wingi na kasi ya maji katika vituo 10 vilivyopo katika mabonde ya mto Pangani na mto Ruvuma. Aidha, Serikali imetoa mafunzo kwa Kamati za Maafa katika wilaya 14 za mikoa mitano nchini. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kuimarisha uratibu na menejimenti ya maafa nchini kwa kuanzisha Wakala wa Usimamizi wa Maafa, kuzijengea uwezo Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya na kuendelea kuimarisha Mfumo wa Taarifa za Tahadhari ya Awali.

Kudhibiti Dawa za Kulevya


104.              Mheshimiwa Spika, dawa za kulevya ni changamoto kubwa kwani huwaathiri watu wengi hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilifanya marekebisho ya Sera ya Kupambana na Dawa za Kulevya na kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria Mpya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kupitishwa na Bunge lako Tukufu na kuanza kutumika tarehe 15 Septemba 2015. Sheria hiyo inaipa Tume nguvu zaidi ya kudhibiti na kupambana na tatizo hilo.

105.              Mheshimiwa Spika, Tume imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kutoa huduma za matibabu kwa waathirika. Hadi kufika mwezi Februari 2016, zaidi ya watumiaji 2,223 wamepata huduma katika Hospitali za Muhimbili, Temeke na Mwananyamala. Tume kwa kushirikia na Jeshi la Polisi wameendesha misako, doria na operesheni nchini kwa lengo la kudhibiti uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, ambapo wamefanikiwa kuteketeza mashamba ya bangi na mirungi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mara. Katika mwaka 2015/2016, jumla ya watuhumiwa 43 walikamatwa na kiasi cha kilo 37.2 na kete 156 za dawa aina ya heroin na bangi. Pamoja na ukamataji huo, Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa hukumu kwa kesi kubwa nne za dawa za kulevya. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itakamilisha utaratibu wa kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza ufanisi. Mamlaka itashirikiana na Jeshi la Polisi kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini na kuwafikisha wahusika Mahakamani.

USTAWISHAJI MAKAO MAKUU DODOMA


106.              Mheshimiwa Spika, mwaka 2015/2016, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu imepima viwanja 957 katika maeneo ya Mkalama, Nkuhungu Kusini na Mahungu. Vilevile, jumla ya viwanja 6,599 vilisanifiwa katika eneo la ukubwa wa Hekta 493 na kutoa vibali 275 vya ujenzi. Katika mwaka 2016/2017, Mamlaka inatarajia kuandaa ramani za jumla na ramani za kina katika maeneo ya Ihumwa na Hombolo pamoja na kupima viwanja vipya 4,000 katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Dodoma na kujenga kwa kiwango cha lami barabara zenye urefu wa kilometa 23.

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


107.              Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushiriki kwenye utengamano wa kikanda na kimataifa na kuendeleza Diplomasia  ya Uchumi na Siasa kwa kuzingatia maslahi muhimu ya Nchi yetu. Mathalani, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Miaka Mitatu (2016-2018) wa Ushirikiano kati ya Tanzania na China. Mpango huo umeainisha miradi ya kipaumbele ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali nchini. Ushirikiano huo umelenga kutumia fursa ya Dola za Marekani Bilioni 10 zitakazotolewa na Serikali ya China chini ya Mpango wa kuzisaidia Nchi nne za Afrika, ikiwemo Tanzania. Makubaliano hayo yalifikiwa katika Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Johannesburg, Afrika Kusini tarehe 5 Desemba 2015. Nchi nyingine zitakazofaidika na Mpango huo ni Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya.  Serikali pia imesaini Mkataba wa ushirikiano na Serikali ya Japan kwa ajili ya ujenzi wa Gridi ya umeme na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kusaidia mpango wa maboresho ya Terminal Two  ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

108.              Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, Serikali itaendelea kusimamia na kutekeleza diplomasia thabiti ambayo itachangia katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu ya Tanzania. Aidha, itakuza ubia wa kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Barani Afrika na wadau wengine wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata manufaa ya fursa za utandawazi.

 

URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI


109.              Mheshimiwa Spika, ili kazi zote zilizopangwa kutekelezwa zifanyike kwa ufanisi, tunahitaji uratibu mzuri wa sekta zote ili kila mmoja atekeleze wajibu wake kikamilifu. Hivyo, kuanzia mwezi Julai, 2016 Serikali itaanza kutumia mfumo wa wazi wa kielektroniki wa kufuatilia uwajibikaji na utendaji kazi kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mfumo huo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa utendaji kazi unaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kufikia malengo yaliyopangwa. Mfumo huo utarahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kulingana na Ilani ya Chama Mapinduzi ya mwaka 2015, Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, Ahadi na Maagizo ya Viongozi Wakuu. Aidha, Mfumo huo utapunguza ucheleweshaji wa utekelezaji, mwingiliano wa majukumu na gharama zisizo za lazima katika utendaji kazi.

HITIMISHO


110.              Mheshimiwa Spika, nimetumia muda mrefu kuelezea baadhi ya shughuli ambazo Serikali ya Awamu ya Tano itazipatia kipaumbele.  Kabla ya kuhitimisha Hotuba yangu, napenda kusisitiza masuala machache yafuatayo:-

(i)          Tunayo changamoto kubwa ya kutumia rasilimali fedha kidogo tuliyonayo kukidhi mahitaji makubwa ya kutoa huduma bora kwa wananchi.  Mathalani, upo upotevu wa mapato kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma.  Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika kulingana na sheria na kanuni za matumizi ya fedha za Serikali;

(ii)        Tumedhamiria kufanya mapinduzi ya viwanda ili kujenga uchumi imara kwa faida ya wananchi.  Hata hivyo, tunalo jukumu kwa kila mmoja wetu kuunga mkono dhamira ya kweli ya Serikali ili kufikia lengo hili. Tuungane na Mheshimiwa Rais kuondoa kasoro zilizopo kwa kupunguza urasimu katika kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje; kuimarisha huduma na miundombinu ya kiuchumi kama vile umeme, barabara, reli, maji na rasilimali watu yenye ujuzi kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa na ambavyo havifanyi kazi vianze kufanya kazi. Ni muhimu kuhimiza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vyenye kutumia malighafi iliyopo nchini kwa faida na maendeleo ya wananchi wetu. Watanzania na wawekezaji kutoka nje mnakaribishwa kuwekeza;

(iii)       Tunahitaji kuboresha Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na bidhaa za masoko kama njia ya kujenga muunganisho wa sekta hizi na viwanda ili kuongeza thamani kwa lengo la  kuondoa umaskini kwa wananchi wetu ambao wengi wao ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Tutumie akili, maarifa na nguvu zetu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata nyenzo na pembejeo za kuwaongezea uwezo wa uzalishaji wenye tija kwa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu. Tumedhamiria kuupitia mfumo wa masoko ya mazao yetu ili wakulima wauze kwa faida mazao yao;

(iv)       Tunalo jukumu kubwa la kuboresha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama na miundombinu ya umeme hasa vijijini.  Tumeanza utaratibu wa kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi, kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne;

(v)        Bado tunalo tatizo kubwa la biashara na matumizi ya Dawa za Kulevya.  Tuunge mkono juhudi za Serikali katika vita hii kubwa ya kupambana na tatizo la Dawa za Kulevya ambazo zinaleta athari kubwa kwa wananchi hususan vijana;

(vi)       Umuhimu wa kurejesha maadili katika utumishi wa umma ni suala la kipaumbele. Ni vyema kila mtumishi wa umma kuzingatia sera, sheria na kanuni kuhusu Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma. Aidha, ni vyema viongozi na watumishi wa umma kila mmoja kwa nafasi yake, awajibike kwa cheo na dhamana aliyopewa katika kuwatumikia wananchi. Dhana ya “Kutumbua Majipu” iwe kichocheo cha kuwabaini na kuwarekebisha wale wote wenye dhamira ya kukiuka maadili kwenye nyadhifa zao na katika kuwatumikia wananchi;

(vii)      Tunayo changamoto ya ukuaji wa uchumi ambao hauendi sambamba na kasi ya upatikanaji wa ajira.  Aidha, zipo dalili kwamba vijana wetu wamekuwa wakitumia muda mwingi kufanya shughuli ambazo hazichangii sana katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Tuendelee kuwahimiza vijana na kujenga utamaduni kwa kila mwananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi kwa maendeleo yetu.  Tuunge mkono falsafa ya “Hapa Kazi Tu” na kwamba Asiyefanya kazi na Asile; na

(viii)    Mwisho, niwaombe Watanzania wote kuendelea kuishi kwa amani na utulivu. Tunayo Nchi nzuri na Watanzania wote ni watu wenye upendo. Tudumishe amani, umoja na mshikamano kwa kuwaunga mkono viongozi wetu ili tuongeze kasi ya kuleta maendeleo katika Nchi yetu kwa maana Umoja ni Nguvu. Sekta Binafsi, ambayo ndiyo Injini ya Ukuzaji Uchumi wa Taifa letu, isiwe na tashwishwi hata kidogo. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuienzi na kuisaidia Sekta Binafsi katika kuchangia maendeleo ya Taifa letu.

SHUKRANI


111.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano walionipa tangu wateuliwe. Aidha, nawashukuru Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017. Nawashukuru Watanzania wote kwa kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

112.        Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu); Mheshimiwa Dkt. Abdallah Saleh Possi, Mbunge, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) kwa msaada na  ushirikiano  wao mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Uledi A. Mussa na Bwana Eric F. Shitindi kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha kwa wakati maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/2017.

113.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Nchi yetu imepata misaada na mikopo kutoka kwa Wahisani wetu mbalimbali. Misaada na mikopo hiyo imetoka kwa Nchi rafiki, Nchi fadhili, Taasisi za Fedha duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mifuko mbalimbali ya Fedha duniani, madhehebu ya dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali. Misaada na mikopo hiyo imechangia sana katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini misaada na mikopo waliyotupatia na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za kuleta maendeleo ya Taifa letu.

114.                 Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wapiga kura wangu wa Jimbo la Ruangwa kwa imani na heshima kubwa waliyonipa ya kunikubali na kunichagua kuwa Mbunge wao. Napenda kuwaahidi kuwa sitawaangusha. Ninawashukuru viongozi wenzangu wote wa  Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwao ambao umeniwezesha kutekeleza jukumu hili kubwa la kusimamia utendaji wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Asanteni sana!

115.                 Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuishukuru familia yangu hususan mke wangu Mary Majaliwa na watoto wangu wote kwa kuniombea na kunipa moyo mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huu. Maombi yao yamenipa nguvu ya kutekeleza majukumu yangu.

 

MAKADIRIO YA  MAPATO NA MATUMIZI  YA  FEDHA  ZA OFISI  YA  WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2016/2017


116.        Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/2017, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili Thelathini na Sita, Milioni  Mia Saba Hamsini na Tisa, Mia Nane Sabini na Nne Elfu, Mia Saba na Sita (236,759,874,706). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na Moja, Milioni Mia Tano Sitini na Nne, Mia Mbili Tisini na Tatu Elfu, Mia Saba Sabini na Tatu (71,564,293,773) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Moja Sitini na Tano, Milioni Mia Moja Tisini na Tano, Mia Tano Themanini Elfu, Mia Tisa Thelathini na Tatu (165,195,580,933)  ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

117.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: