ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 18, 2016

LIPUMBA AZIDI KUITESA CUF

Wanachama  wa Chama cha Wananchi (CUF), wameanza kushikana uchawi, huku viongozi wakitakiwa kutoa maelezo ya kwanini wameshindwa kujadili hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Pamoja na hali hiyo, wanachama hao wamemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kutambua kuwa ana wajibu wa kuwasiliana na Profesa Lipumba ili arejee katika nafasi yake ya zamani kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam jana, wakati wa  kongamano lililoandaliwa na Kata ya Makurumla Manispaa ya Kinondoni, ambapo mmoja wa wana CUF Mohamed Mgomvi, alisema anashangazwa na hatua ya kikao cha Baraza Kuu kushindwa kujadili barua ya kujiuzulu Profesa Lipumba.
Alisema CUF kwa upande wa Bara, imebaki haina mtu madhubuti ambaye anaweza kukiendesha kama alivyokuwa kiongozi huyo.

“Ninashangaa hapa mzee Wandwi (Mustafa), kama Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama unashindwa kusema ukweli. Leo hii (jana) CUF imebaki yatima tangu alipoondoka Profesa Lipumba halafu mnasema tupo naye pamoja.

“Haiingii akilini hata kidogo, ni unafiki umetawala kwa baadhi ya viongozi ambao kila kukicha wanakutana na Lipumba wanamuonyesha wanamhitaji, akitoka mnamsema vibaya.

“…napenda kukuambia leo CUF hakuna mwenye uwezo wa kuvaa viatu vya Profesa Lipumba tunamhitaji kiongozi wetu, tumechoka kuburuzwa na unafiki unaoendelea ndani ya chama,” alisema Mgomvi.

Naye Mangaa Dachi, alisema  kwa mujibu wa katiba ya CUF barua ya kujiuzulu Profesa Lipumba inatakiwa iwasilishwe katika kikao cha mkutano mkuu uliomchagua kuliko ilivyo sasa.

“Hivi mnajua kama chama tunavunja Katiba? Kama ndivyo hivyo bado suala la Profesa Lipumba linatakiwa kuwasilishwa kwenye mkutano mkuu, nasi tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake,” alisema Dachi.

Pamoja na hali hiyo wanachama hao walilalamikia mfumo wa upatikaji wa wabunge wa viti maalumu ndani ya chama hicho kuwa umekuwa ukihusishwa na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wakurugenzi.

“Hatuwezi kuvumilia hali hii hata mfumo wa upatikaji wa wabunge wa viti maalumu hivi sasa watu wanafanya wanavyojisikia, leo kuondoka kwa Lipumba wapo baadhi ya wakurugenzi wanatajwa kuchukua fedha kutoka kwa baadhi ya wabunge waliopo sasa ili wawape ubunge,” alisema.

Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF, Mustafa Wandwi, alisema pamoja na yanayoendelea bado wako pamoja na Profesa Lipumba kwa kila jambo linaloendelea ndani ya chama hicho.

Alisema kutokana na hoja ya washiriki wa kongamano hilo, bado kuna kila sababu ya kutafakari kwa kina suala la Profesa Lipumba lakini hata katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kilichofanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar, suala hilo lilijadili kwa kina.

No comments: