Na Woinde Shizza,Arusha
Waziri wa Habari,Utamaduni,sanaa na michezo nchini,Nape Nnauye ametaja mambo manne ambayo ni vikwazo ndani ya sekta ya sanaa ya filamu nchini na kuyaita kwamba ni majipu huku akisisistiza kwamba serikali
itakwenda kutunga sera ya sekta hiyo katika mwaka wa fedha 2016/17.
Nape,aliyataja mambo hayo na kuyafananisha na majipu kuwa ni uporaji wa kazi za wasanii nchini,ujenzi duni wa miundombinu ya kazi za wasanii nchini,usimamizi mbovu wa bodi ya filamu nchini sanjari na tatizo la mfumo mbovu wa usambazaji wa kazi za wasanii nchini.
Akizindua tamasha la filamu la Tanzanite International Film
Festival(TIFF) jijini Arusha juzi ambao ulihudhuriwa na wasanii maarufu wa filamu nchini waziri huyo alisema kwamba jipu la kwanza ambalo atakwenda kulitumbua ni uporaji wa kazi za wasanii nchini.
“Jipu la kwanza tutalitumbua kwenye bajeti yetu ya mwaka 2016/17 ni uporaji wa kazi za wasanii nchini wengi wananyonywa jasho lao”alisema Nape
Hatahivyo,alisema kwamba jipu la pili ni ujenzi duni wa miundombinu ya kazi za wasanii za filamu nchini na kudai kwamba chini ya uongozi wake atahakikisha anaimarisha miundombinu bora kwa lengo la kuwasaidia
wasanii hao pamoja na kulinda haki zao.
Alisema ya kwamba mfumo wa kazi za usambazaji wa kazi za wasanii nchini pamoja na hakimiliki ni wa kinyonyaji huku akitolea mfano wa kazi za msanii maarufu wa sanaa hiyo nchini marehemu Stephen Kanumba na kusema kwamba familia yake hainufaiki na matunda ya kazi zake hadi
sasa kutokana na mfumo mbovu wa usimamizi wa kazi za wasanii nchini.
Alitaja takwimu kwamba mwaka 2011/12 jumla ya filamu 218
zilitengenezwa nchini na mwaka 2014/15 kazi hizo ziliongezeka hadi kufikia 14,00 huku akidai hilo linadhihirisha kwamba sekta hiyo inakua
kwa kasi nchini na kuongeza ajira .
Hatahivyo,Rais wa shirikisho la wasanii wa filamu nchini(TAFF),Simon Mwakifamba aliwataka wasanii wa filamu nchini kujiandaa kisaikolojia kukabiliana na soko la ushindani wa filamu duniani kwa kuwa wabunifu.
“Serikali tunaiomba iandae sera itakayoandaa mazingira mazuri kwa wasanii nchini kuhusu usalama wa kazi zao”alisema Mwakifamba
Naye, muaandaji wa tamasha hilo,Said Sassi alisema kwamba tatizo la uharamia wa kazi za wasanii nchini limetanda na kuwaomba wafanyabiashara na makampuni kujitokeza kudhamini vipindi mbalimbali vya luninga kwa lengo la kuinua sekta hiyo.
Mkurugenzi wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya vito ya Tanzanite One Mining Ltd ambao ni miongoni mwa wafadhili wa tamasha hilo,Feisal Shabhai alisema lengo la kampuni yao kujitosa kufadhili tamasha hilo ni kutoa mchango wao katika kusaidia jamii kupitia faida wanayoipata ili kuinua sekta ya ajira nchini.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake