Saturday, April 23, 2016

SHAHIDI AMKAANGA MTUHUMIWA KESI YA MENO YA TEMBO

Shahidi wa nne katika kesi ya kukutwa na vipande 14 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 21 milioni bila kuwa na kibali inayomkabili mshtakiwa Said Shomaria, ameileza mahakama kuwa alimkuta mshtakiwa akiuza vipande hivyo chumbani.
Shahidi huyo ambaye ni Askari Polisi namba F 8165 Jackson kutoka Kituo cha Polisi Buguruni , ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa alishiriki katika ukamataji wa mshitakiwa Said Shomari ambaye anakabiliwa na mashitaka ya kukutwa na vipande 14 vya meno ya tembo.
Jackson, ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Hassan, wakati kesi hiyo iliposikilizwa.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Florida Wenslaus, shahidi huyo amedai kuwa walifika eneo la tukio na walimtafuta mjumbe wa eneo hilo ambapo walizingira nyumba kwa ajili ya ukaguzi.
Jakson amedai kuwa walipata taarifa kutoka kwa ofisa wa wanyamapori ambaye aliwataarifu kuwa kuna mtu anauza meno ya tembo maeneo ya Vingunguti Force.
Alidai askari walikuwa watatu na walipofika katika eneo hilo waliingia chumbani alipokuwa mshitakiwa, walikuta watu wanne ambao ni maofisa wanyamapori waliojifanya wanunuzi wa meno hayo.
‘’Tulikuta watu wanne ndani watatu kutoka wanyamapori na mmoja ambaye ni msiri aliyetoa taarifa hiyo kwa maofisa hao, Pia tulimkuta mshitakiwa akiwa amewafunguliwa kasha lenye meno ya tembo maofisa wa wanyamapori,’’ alidai Jackson.
Akiendelea kutoa ushahidi huo, shahidi huyo alisema kuwa walikuta vipande 14 vya meno ya Tembo na kwamba katika nyumba waliyomkuta hakuwa mpangaji bali alikaribishwa na Ally Hussein aliyekuwa mwenye chumba.
Katika mashtaka yake, ilidaiwa kuwa Juni 3,2013 maeneo ya Vingunguti Force wilayani Ilala, mshtakiwa alikutwa na vipande 14 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 21 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake