Sunday, April 24, 2016

TUME YA MIPANGO YAZINDUA MWONGOZO WA MWINGOZO WA USIMAMIZI NA UTAYARISHAJI WA MIRADI YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UMMA




Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma (Public Investment Management Operational Manual), kulia ni Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri na kushoto ni katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma Bibi Rehema Madenge.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akitoa hotuba katika mkutano wa uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma kilichofanyika mjini Dodoma.
Wajumbe wa mkutano.

Na Adili Mhina, Dodoma

Tume ya mipango imezindua kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma (Public Investment Management Operational Manual) kwa lengo la kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuleta ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Akizindua mwongozo huo katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa juma mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wataalamu wa uchumi, sera na mipango kutoka wizara, halmashauri na taasisi mbalimbali za serikali, Waziri wa fedha na mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alieleza kuwa shabaha ya mwongozo huo ni kutoa maelekezo ya mchakato na hatua zinazohitajika kufuatwa katika kutayarisha na kutekeleza miradi yote inayotumia fedha za umma au kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Waziri mpango aliwataka viongozi wote wenye dhamana ya kusimamia miradi kusoma mwongozo huo na kuuelewa ili kuepuka makosa yaliyokuwa yakijitokeza huko nyuma huku akisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano haitamvumilia wala kumonea huruma mtendaji yeyote atakayeshindwa kuwajibika ipasavyo.

“Kuanzia sasa watu ambao wamepewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo, miradi itakaposhindwa kuna mambo mawili tu yakufanya; ama waachie ngazi mapema wao wenyewe au basi wasubiri tuwatumbue. Kwahiyo nawaombeni sana hiki kitabu ambacho kimeandaliwa kuanzia leo kila mmoja akisome vizuri ili kusiwe na miradi tena ambayo ni ya ovyo ovyo,” alisisitiza waziri mpango.

Mwongozo huo unazielekeza Wizara, Idarana Wakala wa Serikali,Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa jinsi ya kufanya uchambuzi unaozingatia vigezo vya kiuchumi na kifedha na kufafanua mbinu, hatua, taratibu, na kuweka viwango vinavyohitajika katika kuandaa na kuwekeza miradi.

Waziri Mpango alieleza kuwa maelekezo ya mwongozo huo yanafafanua vigezo muhimu vya uchambuzi wa kiuchumi na kifedha ili kufikia uamuzi wa miradi ipi ina manufaa na inaweza kupata mikopo katika soko la mitaji la ndani au la kimataifa.

“Mwongozo huu umeanisha vigezo kama mzunguko wa mradi (project cycle) ikiwa ni pamoja na andiko la awali (concept note), mchanganuo wa faida na hasara (cost-benefit analysis) vigezo vya kuchanganua mradi kama vile uwezo wa uzalishaji (internal rate of return) na thamani halisi ya uwekezaji (Net Present Value), na vinginevyo”Alieleza Dr. Mpango.

Kuzinduliwa kwa mwongozo huo kunatoa tafsiri kuwa miradi yote itakayohitaji fedha za Serikali katika Bajeti italazimu kufuata utaratibu uliobainishwa katika kitabu hicho ili kuweza kuimarisha ufanisi na kupata thamani ya fedha. Hivyo, Mwongozo ni chombo muhimu katika michakato mbalimbali ya kupanga bajeti kama vile Mwongozo wa Mpango na Bajeti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka Mmoja na kadhalika.

Kwa upande wake Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwandri alieleza kuwa mwongozo huo unategemewa kuwa mwanzo wa kujenga uwezo katika usimamizi wa uwekezaji wa umma na utakuwa ni msingi wa kuwaimarisha maafisa wa serikali kinyenzo katika kuchambua, kuchagua, kuwasilisha miradi ya uwekezaji kiuchumi na kifedha, pia kijamii kwa kukidhi taratibu na sheria zinazoendesha uwekezaji katika sekta ya umma.

“Katika kufanikisha utekelezaji wa Mwongozo huu na kujenga uwezo wa kutosha, Serikali imedhamiria kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa walengwa wakuu katika ngazi za mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ili kuongeza utaalam na kuwekeza miradi michache kwa mwaka wa bajeti lakini kwa ufanisi zaidi”, alisema bibi Mwanri.

Mwongozo huo pia unatoa taratibu kwa miradi ambayo haitapata fedha kwa mwaka husika itawekwa katika kanzi-data (Database) ambayo itaanzishwa chini ya Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa ajili ya kufikia malengo ya utekelezaji wa usimamizi wa uwekezaji katika sekta ya umma.

Kukamilika kwa kanzi-data kutasaidia wadau mbalimbali wanaohusika na maamuzi ya uwekezaji katika sekta ya umma kuwa na uelewa mmoja kuhusu miradi yenye kipaumbele. Kanzi-data itaonesha miradi gani ya umma, inategemewa kutekelezwa, itaanza lini, na kumalizika lini na ina fedha kiasi gani.
Kaimu naibu katibu mtendaji kutoka Tume ya Mipango anayesimamia klasta ya uchumi jumla, dkt. Lorah Madete akijibu hoja zilizotolewa na wajumbe katika kipindi cha majadiliano. 
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma, kushoto ni Katibu tawala wa mkoa wa Dodoma bibi. Rehema Madenge na kulia ni bi Anna Kimwela kutoka Tume ya Mipango.
Moja ya wajumbe wa mkutano akichangia mada wakati wa mkutano.
Wataalamu wa uchumi, sera na mipango wakiwa katika hali ya umakini wakati wakifuatilia kinachoendelea wakati wa mkutano.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa tano kutoka kushoto kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano mara baada ya uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma.


No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake