Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kupitia timu yake maalumu, limepanga kukutana na viongozi wa Bunge Mei 10, kujadiliana kuhusu hatua ya chombo hicho cha kutunga sheria kuweka mfumo wake wa ‘feed maalumu’, uliogundulika kuchuja habari za vikao vya mkutano wa Bunge linaloendelea.
TEF imechukua hatua hiyo siku ya 16, tangu kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mjini Dodoma huku waandishi wa habari wakizuiwa kupiga picha au kurekodi na badala yake kutakiwa kuchukua matukio hayo kupitia matangazo yanayorekodiwa na Bunge.
Uamuzi huo uliibua mpasuko ndani ya Bunge hilo na kusababisha wabunge wa upinzani wanaounda Ukawa kususia vikao hivyo.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema jana kwamba hatua ya kwanza kabla ya kwenda bungeni itakuwa ni kupeleka barua ya kueleza kutokubaliana na mfumo huo ambao tokea vikao vya Bunge vinavyoendelea vianze jukwaa lake limeona hauna tija.
“Tumebaini habari kutoka ndani ya Bunge hilo kwa sasa zinachujwa mno. Pili, ubora wa picha kupitia ‘feed’ hiyo una kiwango cha chini ndiyo sababu tunapeleka barua ya kulitaka Bunge lifikirie upya, liruhusu chombo chochote kianze kurusha moja kwa moja bila kulazimika kujiunga na ‘feed’ maalumu iliyoanzishwa,” alisema Makunga.
Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema hata Waziri wa Habari, Nape Nnauye alikiri kuwapo kwa dosari katika mfumo huo. Alisema Bunge hilo linaingilia majukumu yasiyokuwa yake.
“Lakini pia, naamini tunaangalia Bunge la Afrika Kusini, anayoyafanya Julius Malema wanataka yasionekane kwenye Bunge letu. Lakini siyo kazi ya polisi kupiga wabunge, kama hawatawapiga wabunge hatutapata hizo picha za udhalilishaji, wafanye kazi zao ‘professionaly’ … kwa hiyo tutaenda kuzungumza nao ili kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru,” alisema Balile.
Januari 28, mwaka huu polisi 35 walitumika kuwatoa ukumbini wabunge kutoka vyama vya upinzani baada ya vurugu kutokea ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na uamuzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge.
Baadhi ya wabunge walitolewa ukumbini wakiwa wamebebwa mzobemzobe, wengine wakiwa wamechaniwa nguo na wengine kurushiana makonde na polisi katika tukio la aina yake tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake