Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimewasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi
7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na
kuwataka waondoke chuoni hapo mara moja.
Jana, lilitolewa
tangazo chuoni hapo likiwataka wanafunzi hao kuondoka kati ya jana hadi
leo saa 12 jioni. Tangazo hilo lilieleza kuwa kutokana na matatizo
yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo, Serikali kupitia Wizara
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imeamua wanafunzi hao
kurejea majumbani na wataelezwa mustakabali wao “mapema iwezekanavyo”.
Makamu
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alipotakiwa kufafanua suala
hilo, alisema kwa ufupi kuwa suala hilo lipo lakini akaelekeza apigiwe
simu Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Beatrice Baltazal kwa maelezo zaidi.
Baltazal alipotafutwa alisema kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la Serikali na wametakiwa kulitekeleza.
Kuhusu lini na nini hatima ya wanafunzi hao, alisema bado hawajui hadi hapo watakapoelekezwa vinginevyo.
Hata
hivyo, kulikuwa na malalamiko kwa wanafunzi hao juu ya namna
walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao kwa ghafla na kutakiwa
kuondoka.
Kozi ya stashahada ya ualimu wa sayansi, ilianzishwa
maalumu kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuziba pengo la
walimu wa sayansi na ilikuwa inatolewa UDOM pekee.
Waliokuwa na
sifa za kujiunga na kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza kidato cha
nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao waliokuwa
wamekopeshwa na Serikali wamesimamishwa siku mbili baada ya wenzao zaidi
ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya kubainika
hawakuwa na sifa za kudahiliwa.
No comments:
Post a Comment