Hai. Miaka 30 waliyokaa uraiani vijana wawili wakazi wa Machane Shari imekoma leo baada ya Mahakama ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kuamuru wamalizie muda uliosalia wa maisha yao wakiwa jela.
Vijana hao, Obadia Daniel Mkulima (30) na Jubiliti Mushi (30) wamehukumia kifungo hicho cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kubaka kwa zamu mwanamke anayewazidi umri kwa miaka 10, ambaye pia ni mkazi wa Machame Shari.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Arnold Kirekiano amesema anatoa hukumu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi usioacha shaka yoyote uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watatu akiwamo Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Hai na Dawati la Jinsia na Watoto wilayani hapa.
“Kosa walilotenda watuhumiwa hawa ni kinyume na mwenendo wa makosa ya jinai kifungu 131A(1) sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 202,” amefafanua.
Awali, Mwendesha Mashtaka, Elisha Molile alidai kuwa watuhumiwa hao alitenda kosa hilo Machi 11, 2014 saa 3 usiku.
Amesema vijana hao walimbaka kwa genge mwanamke huyo ambaye ni mke wa mtu, kitendo ambacho kimemsababishia madhara ya kisaikolojia katika maisha yake, hivyo wanastahili adhabu kali.
Watuhumiwa hao walipopewa nafasi ya kujitetea waliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu kutokana na umri wao na kwamba wana watoto wanaotegemea, maombi ambayo mahakama hiyo iliyatupilia mbali.
No comments:
Post a Comment