Shughuli nyingi mjini Unguja jana zilisimama wakati Jeshi la Polisi Zanzibar lilipomhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa takribani saa tatu.
Wakati polisi wakimhoji makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Serikali iliyopita, Baraza la Wawakilishi limepitisha kwa kauli moja hoja binafsi ya kutaka dola imdhibiti kiongozi huyo wa upinzani, kwa kile kilichoelezwa kuwa anafanya uchochezi na kutishia amani ya nchi.
Maalim Seif alifika polisi jana saa 3.30 asubuhi kwa mahojiano ambayo yalidumu hadi saa 6.35 mchana.
Muda wote aliokuwa akihojiwa, wafuasi wake walikuwa wamesimamisha shughuli zao ikiwamo kufunga maduka na shughuli nyingine.
Barabara nyingi za kuelekea mjini, hasa za kupitia maeneo ya jirani na sehemu za mahojiano hayo kutokea Jang’ombe na Kidongochekundu, ziliwekewa vizuizi vya polisi, lakini mitaa mingi ilikuwa tulivu. Hali ya hofu na ukimya vilitawala
kutokana na wingi wa askari waliokuwa doria, wengine kwa miguu na baadhi wakitumia magari, wakilizungukia eneo la mji na ng’ambo. Mahojiano hayo yalifanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar yaliyopo Ziwani mjini hapa yakiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Salum Msangi.
“Ni kweli mahojiano na Maalim Seif yamefanyika na tumefikia pazuri. Tumemhoji kutokana na kauli zake alizozitoa hivi karibuni kisiwani Pemba na katika baadhi ya mikoa ya hapa,” alisema kwa kifupi.
Katika mahojiano hayo, upande wa polisi ulikuwa na jopo la watu kumi na moja, wakati Maalim Seif aliambatana na wanasheria wake wawili, Abubakar Khamis Bakar na Awadh Ali Said.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa mengi yaliyozungumzwa hayana tofauti na yaliyokuwamo kwenye barua ya wito.
Miongoni mwa mambo hayo ni madai ya kauli za uchochezi na kufanya maandamano bila ya kibali, hasa katika ziara yake ya hivi karibuni alipotembelea wilaya nne za kisiwani Pemba.
Taarifa zilibainisha kuwa Maalim Seif alikana tuhuma zote hizo, akisema ni uzushi na pia lawama zisizokuwa na msingi zinazomchonganisha yeye na vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Maalim Seif alitumia fursa hiyo kuwataka polisi wasikubali kutumika kisiasa, bali wabaki katika misingi ya sheria na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Ilielezwa kwamba baada ya mahojiano hayo, Jeshi la Polisi Zanzibar lilimtaka Maalim Seif ajidhamini mwenyewe, kabla ya ya kudhaminiwa na mawakili wake hao wawili na kisha walikubaliana kuwasiliana na kiongozi huyo watakapomhitaji.
Maalim Seif baadaye alirudi kwa muda mfupi katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF, Mtendeni kabla ya kuendelea na ziara yake ya kuzitembelea wilaya zote za Unguja.
Katika ziara ya jana, Maalim Seif alifika Wilaya ya Kusini, katika majimbo ya Makunduchi na Paje, alikozungumza na viongozi wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment