ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 1, 2016

RAIS MAGUFULI AWATANGAZIA VITA WAFANYABIASHARA ‘WAJANJA’

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wadau mbalimbali wa CTI na kutoka Sekta ya Viwanda nchini kabla ya kutoa Tuzo za Rais kwa viwanda vilivyofanya vizuri kwa mwaka 2015 katika Ukumbi wa Serena Jijini Dar es Salaam.

Rais John Magufuli amesema Serikali yake itaendelea kupambana na wanaoingiza bidhaa zilizochini ya kiwango na wale wanaokwepa kodi.
Amesema kwa kufanya hivyo, wanachangia kuviua viwanda vya ndani ya nchi.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Wenye Viwanda Nchini (CTI).
Rais amesema pia hatawavumilia watendaji wote watakao wakwamisha wafanyabiashara wenye nia ya kuanzisha viwanda nchini kwa sababu zisizo za msingi na kuwaahidi kuwasaidia waweze kufanikisha ndoto zao.
Pia, amesema ni vizuri wafanyabiashara wote nchini wakatumia fursa zipatikanazo katika awamu hii ya uongozi wake, ili wasije kuzijutia baadaye.
“Nasema kwa dhati kutoka moyoni, you have my support, mkishindwa katika kipindi cha awamu ya tano basi hamtaweza tena,” alisema.
Rais Magufuli alisema nchi inapokuwa na viwanda vingi vitatoa ajira kwa Watanzania, vitaongeza mapato kwa Serikali na kuingiza fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.
“Nina dhamira ya dhati ndani ya moyo wangu kuwasaidia wenye nia ya kuanzisha ya viwanda, siwachukii matajiri nawapenda matajiri,” alisema.
Rais Magufuli aliwapa moyo wafanyabiashara wenye viwanda kuanzisha vingine ili Serikali iweze kunufaika zaidi.
Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi kama maliasili na madini na akawahakikishia wawekezaji kuwa lipo soko kubwa la bidhaa watakazozitengeza lenye watu milioni 160 katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Magufuli alisema sekta ya viwanda ni muhimili mkubwa wa uchumi katika nchi huku akitolea mfano wa nchi za China, India, Korea Kusini, Malaysia, Thailand na Vietnam ambazo zimekuwa kwa kasi kwa sababu ya uwepo wa viwanda.
Alisema viwanda vinapoanzishwa nchini badala ya kuuza mali ghafi kwa bei ndogo zitatengenezwa bidhaa ambazo zitauzwa nje ya nchi na kutoa ajira kwa Watanzania.
“Badala ya kuuza ngozi tutengeneze viatu hapa hapa nchini au badala ya kuuza ng’ombe Comoro tumepeke nyama iliyosindikwa,” alisema.
Alisema nchi kama ya Sudan Kusini ina mahitaji makubwa ya unga wa mahindi.
“Lakini wanaofaidika na soko hilo ni Wakenya ambao wanakuja nchini wananunua mahindi, wanasaga na kuyapeleka huko,hivi wafanyabiashara tunashindwa hata kuanzisha viwanda vya kusaga mahindi,” alisema
Alisema Mkoa wa Arusha una ng’ombe wa maziwa lakini yananunuliwa na Wakenya ambao wanayasindika kwenye viwanda vyao na kuja kuyauza hapa nchini.
Hata hivyo, alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha benki ya maendeleo ya viwanda kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo.
Kuhusu kuondoa kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya viwanda nchini, Magufuli alisema Serikali imeshatenga Sh1trilioni katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Pia, Serikali imeunda kamati maalumu itakayoangalia mazingira ya ufanyaji biashara nchini ikiwamo kodi na tozo mbalimbali.
“Nchi yetu inakuwa na kodi za ajabu ajabu, mfano zao la kahawa kulikua na zaidi ya kodi 30. Haya ndiyo tunayoyaangalia,” alisema.
Kuhusu upatikanaji wa mitaji na riba kubwa zinazotozwa na benki, alisema katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali inajiandaa kuanzisha benki ya viwanda itakayowasaidia wenye wawekezaji.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali imejikita katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingi zaidi nchini.
“Tumeandaa mkakati wa pamba hadi inakuwa nguo, alizeti hadi mafuta na tunaendelea kufufua viwanda vilivyokufa,” alisema.
Akizungumzia changamoto zinazowabiri wenye viwanda nchini, mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Samuel Nyantahe alisema uchakavu wa miundombinu ya umeme na miundombinu ya barabara imekuwa ikiongeza gharama za uzalishaji.
Pia, alilalamikia uwapo wa utitiri wa kodi, mamlaka za usimamiaji biashara na uwapo wa bidhaa bandia zinazotishia bidhaa za ndani.

No comments: