Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge akizungumza na wawakilishi kutoka Kampuni ya TING(hawapo pichani) kuhusu kushirikiana na Serikali kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo.
Afisa Mtendaji Mkuu kutoka TING Mch. Dkt. Veron Fernandos akifafnua jambo katika kikao kati ya kampuni yake na Serikali kilicholenga kushirikiana katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo.
Mkuu wa Masoko kutoka TING Bi. Bernice Hannah akionesha jinsi kampuni yake itakavyoweka miundombinu ya kuweka matangazo ndani ya uwanja wa taifa katika kikao baina ya Serikali na kampuni ya TING kushirikiana katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo.
Baadhi ya maafisa wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wakifatilia kikao baina ya Serikali na kampuni ya TING kushirikiana katika kuboresha mapato ya Uwanja wa taifa kupitia matangazo. (Picha na Raymond Mushumbusi WHUSM)
Serikali imeanza majadiliano na kampuni ya TING katika kuboresha mapato ya uwanja wa Taifa kupitia matangazo uwanjani hapo.
Akizungumza hapo jana wakati wa kikao kati ya Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na kampuni hiyo, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge amesema kuwa Serikali imefarijika kupata maombi hayo kutoka kampuni ya TING ya kuboresha mapato ya uwanja wa Taifa kupitia matangazo ambayo yatawekwa katika maeneo ya uwanja huo.
“Ndugu zetu TING wamekuja na wazo zuri sana na tumelipokea na tunaahidi kuliangalia kwa jicho la tatu kwani ni fursa ya pekee kwetu, sio kuboresha mapato tu bali kutangaza uwanja wetu na kuendeleza michezo kwa ujumla” alisema Bw. Nkenyenge.
Aliongeza kuwa ni wakati sasa wa Serikali pamoja na Wananchi kufaidika na uwanja wao ambao ni wa kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwani fursa hiyo itasaidia pia kuendeleza Kijiji cha Michezo Changamani ambao pia ni mpango wa Serikali katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu kutoka TING Mch. Dkt. Veron Fernandos amesema kuwa kampuni yake itatoa ushirikiano kwa Serikali kupitia Wizara na ni azma yao kuona wananchi wanaona faida ya kuwa na uwanja wa kisasa ambao utawaletea mafanikio katika maendeleo ya michezo nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Esther Yonael ameipongeza kampuni ya TING kwa kuona fursa na kuitumia kwani kuna kampuni nyingi zinaweza kuwa ziliona hiyo fursa hii lakini sikakosa uthubutu wa kuleta maombi Wizarani kushirikiana katika suala hilo ambalo linafaida kwa pande zote mbili.
Aidha, Mkuu wa Masoko kutoka TING Bi. Bernice Hannah ameihakikishia Serikali kuwa wamejipanga vizuri na wamefanya utafiti wa kina wa mradi huo na kuona kuwa unawezeka ukafanyika na kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo nchini.
Kampuni ya TING imedhamiria kushirikiana na Serikali katika kuboresha mapato ya uwanja wa Taifa na imejipanga kuwekeza Shilingi Billioni moja kwa miaka minne katika miundombinu na wataalam.
No comments:
Post a Comment