Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba
IKIWA leo saa sita usiku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kuzima simu feki za mkononi, mafundi wa simu nchini wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu kutoka mamlaka hiyo.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa uamuzi wa kuzima simu feki.
Alisema mafundi wa simu, wanatakiwa kuomba leseni ya kutengeneza simu na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu.
Akizungumzia simu feki, Kilaba alisema idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango, zimebaki kuwa ni asilimia 2.96 huku namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zimefika 0.09.
Kilaba alisema idadi ya namba tambulishi, ambazo hazina kiwango zimepungua kutoka asilimia 3 kwa mwezi Mei hadi kufikia asilimia 2.96 huku namba tambulishi zilizonakiliwa zimepungua kutoka asilimia 2 hadi 0.09.
Alisema idadi ya namba tambulishi za simu halisi, imeongezeka kutoka asilimia 85 mwezi Mei mwaka huu hadi kufikia asilimia 96.95 ilipofika juzi.
Wakati TCRA inazindua mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi Desemba mwaka 2015, idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zilikuwa sawa na asilimia 4 na zile ambazo zilikuwa zimenakiliwa zilikuwa ni sawa na asilimia 30.
“Pamoja na kuwapo idadi ndogo ya watu ambao wanatumia simu feki, msimamo wetu bado uko palepale ifikapo kesho (leo) saa sita usiku, maana suala la usalama halitegemei idadi ndogo ya simu hizo,” alisema.
Aliwakumbusha Watanzania wote kuwa ni jukumu la kila mmoja, kuhakikisha kuwa simu yake ni halisi na sio bandia, kwani kuanzia leo, hakuna simu bandia itakayoweza kufanya kazi nchini.
“Nawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi kutambua kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi, kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka kumi (10) au faini isiyopungua Sh millioni 30 au vyote kwa pamoja."
Kilaba aliwataka wanaofanya biashara za kuingiza simu hapa nchini kutoka nje, wahakikishe kuwa simu wanazoleta zinakidhi viwango, zimehakikiwa kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment