ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 24, 2016

K AANDALIWA MAPOKEZI MAKUBWA BAGAMOYO


Na Richard Mwaikenda, Dodoma

MWENYEKITI mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Jakaya Kikwete ameandaliwa mapokezi makubwa na wanaCCM wilayani Bagamoyo kesho baada ya kung'atuka wadhifa huo, kwenye Mkutano Mkuu Maalum Dodoma.

Akielezea kuhusu mapokezi hayo mjini Dodoma jana, Katibu Mwenezi wa CCM, Wilaya ya Bagamoyo,Kassim Gogo alisema kuwa mapokezi hayo yataanzia Chalinze hadi Bagamoyo.

Alisema kuwa wanaCCM wa wilaya hiyo wanajisikia furaha sana kuona Jakaya Kikwete ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Msoga, wilayani humo, ameng'atuka salama baada ya kukitumia chama na serikali kwa miaka kumi.

Alisema kuwa jambo lingine linalowapa faraja ya kuandaa mapokezi hayo ni kwamba Jakaya Kikwete ameng'atuka uongozi kwa kukiacha chama salama na nchi ikiwa salama pia.

Gogo, alisema kuwa katika mapokezi hayo watakuwepo madiwani wote wa wilaya hiyo, viongozi wa CCM, wabunge wote wa Mkoa wa Pwani na wananchi. 


Alisema kuwa wakati wa hafla hiyo pia Mwenyekiti mstaafu, Kikwete atakabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo kumvisha gwanda ili awe mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani.

Katika sherehe za mapokezi zitakazofanyika mbele ya Makao Makuu ya Ofisi za CCM za wilaya hiyo zilizopo Bagamoyo Mjini, patakuwepo ngoma za asili ya makabila ya Wakwere, Wazaramo na Wazigua pamoja na wasanii mbalimbali pia watatumbuiza.

Alisema kuwa Kikwete akiwa amepumzika baada ya kung'atuka, watapata wasaa wa kuchota hekima na burasa zake ya jinsi ya kukiongoza chama hicho na serikali pia. 

No comments: