ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 21, 2016

SERIKALI YAVUNJA BODI YA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA KCU NA KUMFUTA KAZI MENEJA MKUU

Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera, Kagera Co operative Union 1990 LTD (KCU) pamoja na Meneja Mkuu wa Chama hicho na Mrajisi Masidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera wamesimamishwa kazi kuanzia leo tarehe 21.07.2016 kwa tuhuma za ubadhilifu zaidi ya shilingi milioni 900 pamoja na kuingia mikataba yenye harufu ya rushwa iliyopelekea hasara kubwa kwa Chama hicho Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera.

Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Nchini Dkt. Audax Peter Rutabanzibwa akitangza rasmi kusimamishwa kwa Bodi ya KCU pamoja na Meneja Mkuu wa Chama hicho cha Ushirika alisema kuwa Bodi hiyo ikishirikiana na Meneja Mkuu Bw. Vedastus Ngaiza walitoa taarifa za uongo katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho wa mwezi Mei 2016 kuhusu deni wanalodaiwa na Benki ya CRDB.

Dkt. Rutabanzibwa alisema baada ya kutuma wakaguzi kutoka ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Wakaguzi hao walibaini kuwa taarifa waliyosomewa wananchama katika mkutano ilitaja kuwa deni lilikuwa Shilingi bilioni 2.8 kumbe haikuwa kweli kwani deni lilikuwa limepanda hadi shilinngi bilioni 3.15 Bodi na Meneja Mkuu walikuwa wamewadanganya wanachama wa chama hicho.

Pili, Wakaguzi hao waligundua kuwa shilingi Milioni 124 zilitumika katika malipo na hakukuwa na maelezo ya kutosheleza kuhusu malipo ya fedha hizo. Tatu, KCU iliingia mikataba ya kukodisha majengo yake amabayo haikufuata bei ya soko kwa sasa, na mikataba hiyo ilifungwa kwa makubaliano ya miaka 10 jambo ambalo linapelekea Chama hicho kulipwa pango kwa bei ya chini kabisa isiyoendana na soko.

Nne, Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera KCU kimekuwa kikinunua kahawa ya kiwango cha chini kabisa na kusababisha hasara kubwa. Tano, Chama cha KCU kilijiingiza kataika miradi isiyokuwa na tija kama mradi wa kununua maharage ambao ulikisababishia hasara kubwa Chama hicho.

Dkt. Rutabanzibwa alisema kuwa kutokana na sheria Na. 6 ya mwaka 2003 inayohusu usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini Bodi ya KCU hakufanya kazi yake ipasavyo ya kukisimamia vizuri chama hicho Aidha, Bodi hiyo ilifanya vikao 12 kwa mwaka jana 2015 vikao ambavyo vinaonekana havikuwa na tija kwani pamoja na vikao hivyo vya Bodi kufanyika bado kulikuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha.

No comments: