MKUU wa Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora Gabriel Simon Mnyele ametangaza rasmi kuruhusu vikao na mikutano ya kisiasa katika vijiji, kata na majimbo yote ya ubunge wilayani humo ili kuhamasisha shughuli za maendeleo
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Mnyele amesema kwa kuwa hizi ni zama za hapa KAZI TU Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji wameruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara yenye agenda ya kuhamasisha maendeleo.
Alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli iliyobeba kauli mbiu ya HAPA KAZI TU inataka watu wafanye kazi na sio kuendekeza bla bla za kisiasa kwa kufanya maandamano na mikutano isiyo na tija ya kimaendeleo.
Mnyele alifafanua kuwa serikali imeruhusu viongozi wa kisiasa waliochaguliwa na wananchi kukutana na wapiga kura wao, kusikiliza kero na kupanga mikakati ya kutatua kero hizo ikiwemo kusimamia utekelezaji shughuli za maendeleo.
Aliwataka Wabunge na madiwani wote wilayani humo kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha shughuli za utekelezaji miradi ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Aidha alifafanua kuwa mwongozo uliotolewa na serikali unapaswa kuzingatiwa na wanasiasa wote wanaotakiwa kuendesha mikutano hiyo ni viongozi wa wananchi wa maeneo husika tu yaani Wabunge, Madiwani na si wageni.
‘Wabunge na madiwani wote katika wilaya yangu wanapaswa kuzingatia agizo hilo, atakayekiua hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake’, aliongeza.
Aliwataka viongozi wote wa umma kujikita zaidi kuhimiza wananchi kufanya kazi na sikufanya mikutano ya kisiasa tu.
Aidha Mnyele alionya vikali wote wanaojihusisha na vitendo vya mauaji wilayani humo kwa imani za kishirikina, ugomvi wa mali,wivu wa mapenzi huku akiahidi kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao. Alifafanua kuwa mauaji haya yanatokea sana kwa kukosa msaada kwa Jeshi la Polisi kwani vituo vinakuwa mbali na eneo la tukio hivyo wananchi wanakosa msaada na kusababisha mauaji ya mara kwa mara,
Aidha aliwata wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake waende katika vyombo husika kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni kwa mujibu wa serikali.
No comments:
Post a Comment