BAADA ya kushikiliwa katika Gereza la Makala mjini Kishansa kwa zaidi ya siku saba, mkongwe wa muziki wa Kilingala, Koffi Olomide ‘Grand Mopao’ hatimaye ameachiwa huru na anatarajiwa kupiga bonge moja la shoo ya bure leo mjini Kinshasa.
Kwa mujibu wa chanzo, Koffi aliyewekwa ndani baada ya kusambaa kipande cha video akimpiga teke moja kati ya madensa wake aliyetambulika kama Pamela, leo atafanya shoo ya bure katika Uwanja wa Veledrome uliopo Kinshasa.
“Atafanya shoo ya bure kabisa bila kiingilio katika uwanja wa siku nyingi wa Veledrome kisha kesho atafanya shoo nyingine ndani ya Invest Hotel mjini Kinshasa ambapo shoo hii ya pili ambayo ni kesho itakuwa kwa kiingilio na siyo bure,” kilisema chanzo hicho.
Mara ya mwisho kabla ya kuachiwa huru, mwanasheria wa Koffi alisema;
“Ni aibu. Ni lazima afurahie haki zake. Mahakama zetu zina kasoro kwa makosa yaliyofanyika nje ya nchi, hasa kwenye kesi hii. Koffi anajua ukubwa wa matendo yake na aliomba msamaha na ataachiwa huru hivi karibuni,” alisema mwanasheria huyo anayetambulika kama Master Lukoo Ruffin.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Koffi alijikuta matatani baada ya kumpiga teke Pamela muda mfupi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Polisi wa Kenya walimkamata usiku huo na kumrudisha kwao Kinshasa hali iliyopelekea kuvunjika kwa shoo aliyokuwa amepanga kufanya.
Alipofika nchini kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mji wa Kinshasa, akiwa nyumbani kwake, polisi walimvamia na kumpeleka mahakamani.
Imeandaliwa na Andrew Carlos/GPL
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake