Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa
mkoa wa Mbeya baada ya kupokea taarifa ya mkoa Agosti 7, 2016 kwenye
Ikulu ndogo ya mbeya. (Picha na Ofisi ya Wairi Mkuu)
*Awataka wafanyabiashara kuwaripoti watendaji wanaoongeza kiwango kikubwa cha kodi kuliko inavyostahili kulipwa.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa imeitaka
Mamlaka ya Mapato Tanzania kuimarisha kitengo cha tathmini ili kuweka viwango
halali ambavyo havitawagandamiza wafanyabiashara na uwepo uwazi kuhusu viwango
stahili vya kodi wanavyotakiwa kulipa.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana
jioni (Jumapili, Agosti 07, 2016) wakati alipozungumza na viongozi wa mikoa ya
Mbeya, Katavi, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na Njombe mara baada ya kuwasili
mkoani Mbeya kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya maonyesho ya nane nane kwa
mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika mkoani Mbeya.
‘‘TRA waendelee kukusanya mapato
vizuri ila kuna wakusanya kodi wanaotaka kuharibu mkakati wa Serikali kwa kufanya
mambo ya hovyo kwa kuwaongezea viwango vikubwa vya kodi kuliko kodi stahili
wanavyotakiwa kulipa na kufanya suala hili liwe kama tatizo au adhabu kwao jambo
ambalo si sahihi. Naagiza watendaji wa TRA wanaofanya hivyo wasakwe na
wachukuliwe hatua“, alisema.
‘‘Wafanyabiashara mnaoonewa kwa
chuki binafsi na watendaji wa TRA toeni taarifa ili muweze kufanya biashara
zenu kwa uhakika bila ya wasiwasi lengo ni kuwafanya muweze kulipa kodi sahihi kwa
mujibu wa sheria“, alisema.
Ili kufanikisha mpango huo Waziri
Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwasikiliza wafanyabiashara ambao
wana malalamiko ya kweli ya kutotendewa haki katika kutozwa kodi kwa sababu
mchango kupitia kodi ni kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine ameitaka idara
ya Uhamiaji ijikite katika kudhibiti watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa
wakichukua rushwa kutoka kwa wageni
wanaotoka nje ya nchi na kuwaingiza nchini bila ya kuwa na vibali maalumu.
‘‘Ni lazima tuhakikishe hakuna
uingiaji holela ndani ya nchi na hasa kwa wanaoingia bila vibali maalumu kwani bila ya
kudhibiti suala hilo tunaacha mianya ya kuingia watu wasiokuwa na nia njema na
Taifa letu. Watu watakaobainika wameingia nchini bila ya vibali wakamatwe na
kufikishwa katika vyombo vya sheria,“ alisema.
Alisema kitendo cha mipaka kushindwa
kudhibitiwa na kuruhusu uingiaji holela wa watu wasiokuwa na vibali chini kunasababisha
Serikali kushindwa kuteleza ipasavyo mipango yake ya kuwahudumia wananchi kulingana
na idadi halisi.
Mbali na kuiagiza Idara ya Uhamiaji
pia Waziri Mkuu alisema wakuu wa mikoa ya mipakani wana jukumu la ziada la kuhakikisha
wanadhibiti mipaka yote na kuhakikisha hakuna watu wanaoingia nchini bila ya
kuwa na vibali.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka
wakuu wa mikoa kote nchini kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama
katika maeneo yao na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu ili
Watanzania waweze kutekeleza shughuli zao za maendeleo kama walivyojipangia.
“Natambua kuwa wakuu wa mikoa na
wakuu wa wilaya ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo
yenu, endeleeni kuimarisha hali ya ulinzi na usalama. Nchi hii tunahitaji iwe tulivu na salama na ni wajibu wenu
kuhakikisha kwamba lolote linalotokea mnalikabili vilivyo“, alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe.
Makalla alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa huo kwa Waziri Mkuu alisema mkoa huo
una jumla ya viwanda 1,653 kati yake vikubwa ni tisa, vya kati 19 na vidogo
1,625 na bado wanaendelea kuzisimamia
halmashauri kutenga maeneo zaidi kwa ajili ya kuongeza na kupanua viwanda.
Mhe. Makalla alisema katika eneo
hilo la viwanda mkoa una kiwanda kimoja cha kusindika nyama cha Tanganyika
Pachers kilichopo wilayani Mbeya ambacho hakijawahi kufanya kazi tangu
kilipojengwa na kufungwa mitambo mwaka 1975.
Mkuu huyo wa mkoa alisema usimamizi
wa kiwanda hicho uko chini ya Masajili wa Hazina na kwamba tayari kuna
muwekezaji amepatikana kwa ajili ya kukiendesha hivyo ameiomba Serikali
kuharakisha taratibu za mikataba ili kiweze kuanza kufanya kazi.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
AGOSTI 08, 2016.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake