Dar es Salaam
TANZANIA
13 Oktoba, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
PROGRAMU YA BAHATI NASIBU YA VIZA YA UKAAZI
WA KUDUMU MAREKANI IMEANZA
Ubalozi
wa Marekani jijini Dar es Salaam unatangaza kuanza kwa programu ya Bahati
Nasibu ya Viza ya Ukaazi wa kudumu Marekani (Diversity Visa Program) kwa mwaka
2018 (DV-2018). Kila mwaka, kupitia
programu hii, Marekani hutoa viza za ukaazi wa kudumu (immigrant visas) zipatazo
55,000 kwa raia wa nchi ambazo kihistoria zina idadi ndogo ya watu wanaohamia
Marekani. Mwaliko unatolewa kwa Watanzania wenye sifa kutuma maombi yao katika
programu hii ya uhamiaji kabla ya tarehe 7 Novemba 2016.
Tafadhali
soma kwa makini na kwa ukamilifu maelekezo ya namna ya kutuma maombi yako
katika tovuti maalumu ya Masuala ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya Nje ya
Marekani inayopatikana katika anuani ifuatayo; www.dvlottery.state.gov.
Maombi ya kupata viza hiyo katika kipindi cha mwaka 2018 (DV-2018) yanapokelewa
hivi sasa hadi tarehe 7 Novemba 2016 saa. Unaweza kutuma ombi lako
mara moja tu na kwa njia ya mtandao pekee. Maombi hayatapokelewa kwa njia ya barua wala
kuletwa kwa mkono.
Tafadhali zingatia taarifa muhimu zifuatazo:
·
Hakuna ada yoyote inayotozwa kwa kutuma maombi yako kupitia
mtandao. Tafadhali usitume, usilipe wala kuhamishia fedha kwa taasisi au mtu
yeyote anayedai anaweza kukusaidia kupata viza hii au kuongeza nafasi yako ya
kushinda Bahati nasibu hii.
·
Iwapo utashinda bahati nasibu, utatakiwa tu kulipia ada ya
maombi ya viza katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam wakati
utakapoitwa kwa ajili ya usaili wa viza. Iwapo kuna mtu yeyote atakayekudai
fedha kwa ajili ya kukusaidia kuingia katika Bahati nasibu hii, tafadhali
wasiliana na Ubalozi wa Marekani.
·
Kushinda bahati nasibu hii hakukuhakikishii moja kwa moja kupata
visa. Iwapo utashinda bahati nasibu bado utahitajika kusailiwa ili kuona kama
unakidhi matakwa ya sheria ya Uhamiaji ya Marekani.
·
Unaweza kuwajumuisha watu wa familia yako (mke/mume na watoto wako
wa kuwazaa ambao bado hawajaoa au kuolewa walio chini ya miaka 21) katika
maombi yako ya Viza hii. Iwapo utaongeza watu wengine (mbali na hao
waliotajwa) maombi yako ya Viza yatakataliwa. Iwapo mtu yeyote atakuomba
ujumuishe watu wengine katika maombi yako ya visa, tafadhali wasiliana na
Ubalozi wa Marekani – si lazima utaje jina lako utakapotupatia taarifa hiyo.
·
Orodhesha watu wote wa familia yako (immediate
family) katika maombi yako hata kama watu hao wasingependa kuhamia
Marekani pamoja nawe. Kushindwa kufanya hivyo kutasababisha wewe kukosa sifa na
maombi yako kukataliwa wakati wa usaili wa viza.
Iwapo una maswali zaidi, tafadhali tuma maswali hayo kwa barua
pepe ifuatayo; DRSIV@state.gov. Kwa
taarifa za jumla kuhusu viza na masuala mengine ya uhamiaji, tafadhali tembelea
tovuti ya Ubalozi inayopatika katika anuani: http://tanzania.usembassy.gov.
No comments:
Post a Comment