Dar/Arusha. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameanza kuikaba koo Serikali ya Awamu ya Tano akisema ataifikisha Mahakamani ili chombo hicho cha kusimamia sheria kitoe tafsiri ya kuhusu vitendo alivyosema ni kwa ukandamizaji wa demokrasia vinavyofanywa na viongozi wake hasa mkoani Arusha.
Amelaani kitendo cha mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuwasweka ndani madiwani wanne wa chama hicho akisema hiyo ni ishara ya kwamba utawala wa awamu ya tano hauheshimu sheria na kwamba amewaagiza wanasheria wake kwenda mahakama kupata tafsiri kuhusu vitendo hivyo.
Mbowe amesema viongozi hao wamekuwa wakifanya vitendo vya udhalilishaji kwa baadhi ya wabunge, madiwani, mameya na wenyeviti wa halmashauri kinyume na sheria.
“Wakuu hao wa wilaya pamoja na mkuu wa mkoa wamekuwa wakiwadhalilisha wawakilishi wa wananchi ilhali wao ni waajiriwa na hawajaomba kura kwa wananchi,” alisema.
“Nawashangaa sana wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao jambo hili limeanza mwaka huu, hii ni nafasi mbaya sana kwa Rais Magufuli kuchagua makada badala ya watumishi,” amesema Mbowe.
Kuhusu posho za madiwani
Mbowe, alizungumzia msuguano wa posho za madiwani katika Jiji la Arusha, alisema suala hilo lina upotoshaji mkubwa kwa kuwa zilipitishwa na madiwani wa CCM miaka ya nyuma hata kabla Chadema hawajashika halmashauri hiyo.
Alisema ni ajabu kuona baadhi ya viongozi akiwamo mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kufuta posho hizo na kudai kwamba endapo hali hiyo itaendelea, jambo hilo huenda likazusha vurugu na tafrani mkoani humo.
No comments:
Post a Comment