TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara
ya Mfalme wa Morocco nchini Tanzania
Mfalme
Mohammed wa VI wa Morocco anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini kuanzia tarehe
19 hadi 23 Oktoba, 2016.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kukuza zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Morocco hususan katika
masuala ya kiuchumi na kibiashara kwa
faida ya nchi hizi mbili na watu wake.
Vilevile,
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco atatumia fursa ya ziara hiyo kutembelea
Zanzibar na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kujionea vivutio vya
utalii vilivyopo nchini.
Hata
hivyo, ziara hiyo ambayo imejikita zaidi katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi
na kibiashara haitaathiri msimamo wa Tanzania katika mgogoro unaoendelea kati
ya Morocco na Sahara Magharibi.
Msimamo
wa Tanzania ambao umekuwa ukisimamiwa na Awamu zote za uongozi zilizopita na
Awamu hii, upo sambasamba na ule wa Umoja wa Afrika (AU) unaoutaka Umoja wa
Mataifa (UN) ambao ndio wamepewa jukumu la kusimamia mgogoro huo, kuongeza kasi
katika kuutatua na kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.
Tarehe 20 Oktoba, 2016
Mhe. Mfalme Mohammed wa VI atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Mhe. Rais Magufuli
Ikulu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi
kati yao na wajumbe waliofuatana nao.
Mhe.
Mfalme Mohammed VI pamoja na kutembelea Tanzania, pia atatembelea Rwanda,
Ethiopia na Kenya.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
13 Oktoba, 2016.
No comments:
Post a Comment