Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema walipokea taarifa kwamba raia huyo wa China alitekwa nyara na watu wasiofahamika.
Alisema taarifa hizo zilieleza kwamba Liu alitekwa nyara Oktoba 23, mwaka huu saa moja asubuhi na ndipo polisi wakaunda kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini watekaji walikuwa wakidai Yen 100,000 (fedha za China) ambazo ni sawa na Dola za Marekani 19,000.
“Oktoba 24, mwaka huu saa 11 jioni kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha Polisi Kanda Maalumu walibaini kuwa wateka nyara hao wapo katika Hoteli ya Palm Beach Upanga na walipofika hapo wakaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema polisi walipofika chumba namba tisa na kugonga wahusika waligoma kufungua mlango ndipo polisi waligundua wateka nyara hao kuwepo katika chumba hicho.
Alisema wakiwa wanajiandaa kuvunja mlango, mara mtuhumiwa mmoja Wang Young Jing (37) raia wa China aliamua kufungua mlango na kumkamata akiwa na Liu ambaye ni mtekwa nyara.
“Askari walipoingia ndani walimkuta aliyetekwa nyara akiwa hajitambui akiwa na majeraha usoni. Pia katika tukio hili, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine aitwaye Chen Chung Bao (35) raia wa China ambaye ndiye aliyekodi chumba hicho,” alieleza kamanda.
Alisema ndani ya chumba hicho kulikutwa vipande viwili vya taulo walivyotumia kumfunga mikono, kamba za plastiki na bomba la sindano. Alisema majeruhi alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu na watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa. Upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, Polisi ilifanya operesheni katika maeneo ya katikati na pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam na kuwakamata watuhumiwa 57 kwa makosa mbalimbali ya uhalifu.
Kamanda Sirro alisema Mkoa wa Temeke walikamatwa watuhumiwa 21, Ilala watuhumiwa 19 na Kinondoni watuhumiwa 17.
“Baadhi ya watuhumiwa hao ni vikundi mbalimbali wanaojiita majina tofauti ikiwemo ‘Panya road’, ‘Black American’, Taifa jipya na Kumi ndani na kumi nje,” alieleza na kuongeza kuwa watuhumiwa walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kivule, Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana, Kunduchi, Kawe na Keko.
Alisema watuhumiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuvuta na kuuza bangi, kuuza na kunywa gongo na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Katika tukio jingine, watu wawili wamekamatwa katika maeneo ya Karakata Relini kwa tuhuma za kukamatwa wakiwa na gari lenye namba T 550 CWG Toyota Carina likiwa na viroba 11 vya bhangi, gongo lita 80, mitambo 10 ya kutengeneza pombe ya gongo, mirungi kilo mbili na vifaa vya kuvunjia na funguo za vitasa mbalimbali.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment