Jana, tarehe 03 Novemba, 2016, Nchi Wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zimemchagua kwa mara ya pili mtanzania Prof. Chris Maina Peter, Mhadhiri wa sheria katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuwa Mjumbe wa Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (the International Law Commission (ILC) yenye jumla ya Wajumbe 34.
Kwa mara ya kwanza Prof. Peter alichaguliwa Mwaka 2001, kuwa Mjumbe kwenye Kamati hiyo kwa kipindi cha miaka mitano (5), hivyo ushindi huo utamfanya kuwa Mjumbe kwenye Kamati hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 5 kuanzia 2017-2021. Kwa upande wa Afrika, uchaguzi huo ulijumuisha wagombea 16 kuwania nafasi nane za Bara hilo, ambapo wagombea kutoka nchi za Algeria, Misri, Kenya, Moroko, Afrika Kusini na Tanzania waliibuka kidedea kwenye uchaguzi huo.
Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (Iternationa Law Commission (ILC) ilianzishwa mwaka 1948 kwa madhumuni ya kufanya tafiti, kuendeleza na kutunga sheria za Kimataifa (promotion/research, development and codification of international law). Sambamba na majukumu hayo, ILC inao wajibu wa kuushauri Umoja wa Mataifa kuhusu masulaa yote yanayohusu sheria za kimataifa.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kumpongeza Prof. Chris Maina Peter kwa ushindi huo ambao si kwamba umemjengea heshima kubwa yeye peke yake bali Tanzania kwa ujumla. Wizara itaendelea kutoa msaada na ushauri kwa Prof. Peter na Watanzania wengine wenye nafasi kama hizo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuongeza na kuimarisha nguvu na ushawishi wa Tanzania katika Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia kwa ujumla. Aidha, Wizara inapenda kuwakumbusha Watanzania wote wenye sifa za kitaaluma kuchangamkia nafasi mbalimbali za ajira zinazotolewa na Umoja wa Mataifa na Jumuiya nyingine za Kikanda pamoja na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kiutendaji zinazojitokeza.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake