ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 28, 2016

Shigongo: Hivi Ndivyo Nilivyomalizana na CCM

Image result for eric shigongo
INAHITAJI mtu jasiri sana kuzungumza ukweli, kwani ukweli umewagharimu watu wengi, ukweli unaweza kugharimu maisha, unaweza kukupeleka gerezani, unaweza kukufukuzisha kazi, unaweza kugharimu biashara yako! Mambo haya na mengine mengi huwafanya watu kuchagua kubaki kimya, hata kama walitakiwa kufungua midomo yao na kuzungumza ukweli dhidi ya uovu au ubaya fulani.
Mimi si mtu wa kukaa kimya ninapoona jambo fulani haliendi sawa, ndivyo nilivyoumbwa, huyo ndiye mimi, kukaa na maneno kifuani au kumwambia mtu maneno ya kumpamba wakati hakustahili siyo desturi yangu, nikifanya hivyo hujisikia kama nataka kufa wakati wowote, ndivyo nilivyoumbwa.
Nilipokuwa mdogo baba yangu (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) alizoea kuniambia “Mwanangu Shigongo unaongea sana, maneno mengine uwe unaweka akiba, utaongea kesho” kwa maneno mengine alichokuwa akinieleza baba yangu ni sawa na msemo wa Kiingereza usemao “SILENCE IS WISDOM” yaani kubaki kimya ni busara.

Tangu siku hiyo na kwa muda mrefu nilijitahidi kuwa ninakaa kimya ili nionekane mwenye busara, yalikuwa ni maisha ya mateso yasiyo na uhalisia, siku moja nikamsikia mtu aitwaye Martin Luther King akisema: “SOMETIMES SILENCE IS BETRAYAL” maneno ya Kingereza yanayomaanisha wakati mwingine kukaa kimya ni usaliti.
Nikaja kumsikia tena wakati mwingine mtu huyohuyo Martin Luther akisema: “THE HOTTEST PLACES IN HELL ARE RESERVED FOR PEOPLE WHOM DURING THE TIMES OF MORAL CRISIS MAINTAINED THEIR NEUTRALITY!” Maneno yaliyomaanisha maeneo yenye joto kabisa huko ahera, yameandaliwa kwa ajili ya watu ambao katika kipindi ambacho maadili yaliporomoka, wao waliamua kutokusema chochote.
Tangu siku hiyo nikatamka: “NITASEMA UKWELI DAIMA FITINA KWANGU MWIKO” na hayo ndiyo yamekuwa maisha yangu, kuzungumza ukweli wakati wote,  badala ya kubaki kimya nikiumia kwa sababu tu nataka kuonekana nina busara, mwema, mzuri au nina hofu kwamba nikizungumza ukweli nitapata matatizo.
Hicho ndicho nilichokifanya wiki iliyopita kwenye ukurasa huu, niliamua kufunguka na kuzungumza ukweli tena kwa unyenyekevu, bila kumtukana mtu wala kumkebehi yeyote, ili kuondoa mambo mengi yaliyokuwa yamejaa kifuani kwangu, kufuatia deni kubwa ambalo ninakidai chama changu cha Mapinduzi (CCM) ambalo linatokana na kazi niliyopewa ya kuchapisha vifaa vya Uchaguzi Mkuu 2015.
Yawezekana kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama nilikosea kueleza hisia zangu hapa, lakini kama nilivyosema wiki iliyopita, kwa mazingira niliyokuwemo ndani yake, sikuwa na jinsi, kama kuna mtu yeyote nimemkwaza kwa uamuzi wangu wa kuzungumza ukweli, basi atanisamehe, halikuwa lengo langu kabisa kumuumiza yeyote bali kumwaga mambo yaliyokuwa yamejaa kifuani mwangu, ili nipate kuwa huru, kweli niko huru.
Niliandika waraka ule kwa hisia nyingi, nikielezea maumivu niliyokuwa nayo na namna ambavyo nilikuwa naelekea kufilisika kama chama changu cha Mapinduzi kisingenilipa deni ninalodai, hapa naomba nieleweke vizuri, sikusema “CCM IMENIFILISI” nilichosema ni kwamba wanaonidai wanatishia kuuza dhamana nilizoweka kama nisingelipa deni lao, maneno mengine tofauti na  hayo ni uchonganishi wenye lengo la kufitinisha na chama changu.
Nimelazimika kuandika tena leo kama nilivyoahidi wiki iliyopita, ili kuwaziba midomo wale wanaojiandaa kusema “AMEPIGWA MKWARA,UNACHEZA NA CCM WEWE?” CCM haiko hivyo, hayo mambo yanaweza kuwa kwenye vyama vingine vya siasa lakini si chama kilichokomaa kama CCM.
Wakati ninaandika kumbukumbu ile sikutegemea kabisa habari ile ingebadilika kuwa kubwa kiasi  ilivyofikia na kusababisha mjadala mrefu mitandaoni na kwenye vyombo mbalimbali vya habari, hicho ndicho kilichotokea. Baada tu ya kutoka siku ya Jumatatu, nilianza kupokea simu kutoka sehemu mbalimbali watu wakiulizia juu ya tukio hilo, wengine wakitaka kufahamu kiasi cha fedha nilichokuwa ninadai na nilifanya biashara gani na chama.
Wapo waliokwenda mbali zaidi na kuniuliza maswali kama “Shigongo huogopi?” “CCM wanaweza kukufanya chochote.” Hakika ilikuwa vurugu, watu wakijaribu kunipandikizia hofu na kunifanya niamini kwamba nilichokifanya, cha kufungua mdomo wangu na kuzungumza ukweli, pengine lilikuwa ni kosa kubwa lililostahili adhabu kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi, niliwaeleza wazi kwamba “Niko tayari.”
Mtandaoni watu waligawanyika makundi mawili, wapo walioniunga mkono lakini pia wapo walioniponda hasa vikundi vya propaganda ambavyo vilijaribu kunipaka matope ili kuonesha kwamba nilikuwa sifai, fisadi ambaye nilitumiwa na baadhi ya watu ndani ya CCM kupitishia ‘dili’ zao.
Eti tisheti moja niliiuzia CCM kwa bei ya shilingi elfu 95 na kofia kwa bei ya shilingi elfu 50, nikisema maneno haya hayakuniumiza nitakuwa muongo, hakika nilivunjika moyo sana pale mtu ninayemheshimu ambaye ni mwandishi mkongwe (sitamtaja jina), lakini  anayeheshimika katika jamii, ambaye siku zote nimemchukulia kama rafiki, ndugu, anaposema mimi nilifanya udanganyifu katika tisheti nilizoiuzia CCM.
Kitu ambacho wengi hawafahamu ni kwamba, kazi hii niliyoifanya kwa chama changu ilikuwa ni kazi halali kimaandishi, tena chama chenyewe ndicho kilichopanga bei ya shilingi 5,650 kwa tisheti moja na shilingi 4,400 kwa kofia moja, siyo shilingi 95, 000 kwa tisheti na 50,000 kwa kofia.
Wote mnaufahamu uchaguzi wa mwaka jana ulivyokuwa mgumu, wa kupata au kukosa! Hakuna aliyekuwa na uhakika wa ushindi, iwe CCM au Ukawa na kuna wakati dalili zilianza kuonesha kama mgombea wa Ukawa alikuwa  na nafasi, wakati mwingine wa CCM ana nafasi, katika mazingira kama hayo mtu unaelezwa tu “Nenda katengeneze, ulete halafu tutakulipa” bila hata fedha za utangulizi!
Mfanyabiashara yeyote angejiuliza “Mh! Wakishindwa je? Nitalipwaje?” Mara moja angeachana  kabisa na biashara hiyo, lakini mimi niliamua kuchukua ‘risk’ na kuifanya kazi hiyo, nikiwa nimemtanguliza Mungu mbele, hebu jiulize leo hii Chama Cha Mapinduzi kiko madarakani, sijalipwa, je, kingeshindwa ingekuwaje?
Najua mtu au kundi lililoanzisha propaganda kuwa niliuza tisheti moja kwa bei ya shilingi 95,000 na kofia kwa shilingi 50,000 lilikuwa na lengo tu la kutaka nichafuke, bila kufahamu kuwa wakati ninapewa kazi hiyo na chama mwaka 2015, mwezi Mei, bei ya dola ilikuwa shilingi 1,700, leo hii nikiwa bado sijalipwa dola moja ni shilingi 2,200!
Thamani ya shilingi imeshuka, kwa kubadilisha shilingi nitakazolipwa kama ningelipwa leo kuwa dola, ninapoteza shilingi mia tano kwa kila dola moja, wafanyabiashara watakuwa wamenielewa kwamba kazi hii, ukiongeza na riba za benki tayari ina hasara kubwa! Labda nitoe mfano kidogo ili nieleweke;
Wakati huo kama nilihitaji dola 10,000 kwenda kufanya kazi hii ya kutengeneza kofia na tisheti ilikuwa ni lazima nitumie shilingi 17, 000,000 kuzinunua, leo hii CCM wakinilipa fedha zangu nikahitaji kununua tena kiasi kilekile cha  dola 10,000 wakati bei ya dola moja ni shilingi 2,200, sitahitaji tena 17,000,000 bali nitahitaji 22,000,000! Kwa hesabu hii rahisi tu, kwa sababu ya thamani ya shilingi kushuka, nitakuwa nimepoteza 5,000,000!
Pamoja na yote hayo mtu anakwenda mtandaoni na kusema eti niliiuzia CCM tisheti moja kwa bei ya shilingi 95,000, huu ni uongo wenye lengo moja tu la kunichafua ili nionekane sifai, lakini uongo huo haondoi ukweli kwamba ninakidai chama na ingekuwa vyema nikalipwa, hata wao wanafahamu mimi si msumbufu, kama hali imefikia hapa tulipo basi kuna tatizo ambalo ni vyema kulishughulikia badala ya kuendelea kunitengenezea timu za propaganda kunishambulia.
Nimetukanwa sana, nimeshambuliwa sana, lakini nataka tu kuutangazia umma kwamba haijalishi nitatukanwa kiasi gani, ilimradi nafsi yangu ni safi, kwamba nilichokisema ni kweli na tena ni haki yangu, sitanyoosha mikono, nitakipigania mpaka dakika ya mwisho ya uhai wangu.
Ukiwa na dawa ya meno mkono wa kushoto, mswaki mkono wa kulia na unataka kusafisha meno yako, hata ungefunga na kuomba siku arobaini ili dawa itoke kwenye chupa yake na kwenda kwenye mswaki, utasali mpaka Yesu anarudi hutashuhudia huo muujiza, atakuja mtu ambaye hata kanisani huwa haendi, atachukua chupa ya dawa na kuikamua, dawa itatoka na kuiweka kwenye mswaki kisha kusafisha meno yake.
Nilichokifanya wiki iliyopita ndicho hichohicho, kukamua ili nipate haki yangu, kuna mambo hapa duniani hayahitaji kufunga na kuomba ni kuchukua hatua tu, ukifunga na kuomba peke yake kwenye suala linalohitaji kuchukua hatua, mbele za Mungu unaonekana huna akili timamu.
Jioni ya siku hiyo ya Novemba 21, 2016, saa 3:30 usiku baada ya gazeti kutoka, nikiwa nyumbani mtu mmoja ambaye nisingependa kumtaja hapa, alinipigia simu na kuniambia “Eric, mzee Kinana anakutafuta, tafadhali mpigie muongee” baada ya kuzungumza naye nilianza juhudi za kumtafuta Katibu Mkuu bila mafanikio, mpaka nikaamua kulala matumaini yangu ni kwamba ningempigia siku iliyofuata.
Saa moja asubuhi niliondoka nyumbani kuwapeleka watoto shule ambako niliwashusha na kuelekea ofisini kichwa kikiwa kimejawa na mawazo mengi, karibu kila mfanyakazi niliyemwangalia usoni alionekana kuwa na sura ya ‘SIJUI ITAKUWAJE?” Hakuna mtu aliyekuwa akiniambia chochote.
 Saleh Ally, Mhariri Kiongozi Magazeti ya Michezo ni rafiki yangu, huwa yuko wazi sana kuongea na mimi chochote, lakini siku hiyo alikuwa akiniangalia kwa jicho la kwenye kona, hataki kukutanisha macho na mimi, moyoni nikatambua kwamba karibu watu wote ofisini walikuwa na hofu kubwa  sana na hatima yangu na yao.
Saa nne hivi asubuhi, nikiwa nimesimama nje ya ofisi, simu yangu iliita, nilipoangalia kwenye kioo niliona maandishi “SG”, moyo wangu ukadunda, maana nilifahamu kabisa mtu aliyekuwa akipiga simu ile kwa namna moja au nyingine alikuwa amechukia kwa uamuzi wangu wa kuzungumza ukweli, pengine alikuwa na hasira na angeweza kunitamkia maneno ya kuniumiza zaidi, nikasita kuipokea simu lakini baadaye nikajipa moyo.
“Shikamoo baba!”
“Marahaba hujambo Eric?”
“Sijambo.”
“Sasa wewe mwanangu umefanya nini tena?” aliniuliza.
Akaendelea kunisema kwamba kitendo ninachokifanya kilikuwa kibaya, nakumbuka nilichokisema peke yake kwake ni kwamba “Sikuwa na jinsi baba, hali yangu ni mbaya sana na hakuna mtu anayeonekana kujali.”
“Uko wapi?”
“Niko ofisini!”
“Hebu njoo haraka hapa Lumumba.” Ilikuwa ni sauti ya Katibu Mkuu wa CCM, mzee Kinana ambaye kwenye simu yangu nimeitunza namba yake kwa jina la “SG”
Moyo wangu ukinidunda, nikijua huko CCM Lumumba nilikokuwa naitwa kulikuwa na matatizo makubwa kwa sababu nimewaudhi viongozi wakubwa wa chama, nilimwita dereva wangu, Nyange na kumwambia: “Kimbia haraka sana kuelekea ofisi za CCM Lumumba!”
Dakika arobaini na tano baadaye tuliegesha mbele ya Jengo la CCM Lumumba, nikashuka na kuingia ndani, nikasaini kitabu cha wageni na kupandisha hadi ofisini kwa mzee Kinana, Katibu wake aliniambia: “Ingia mzee anakusubiri” mara moja nikaingia ndani na kumkuta mzee Kinana ameketi akiwa na Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Rajab Luhwavi.
Tofauti kabisa na matarajio yangu nilipokelewa kwa tabasamu, shinikizo langu la damu ambalo nahisi lilikuwa limekaribia mia mbili, kidogo likaanza kutulia! “Keti kwenye kiti Eric” alisema Luhwavi akiniangalia kwa jicho la huruma, nilipoketi mzee Kinana akaanza kunieleza kwamba hisia zangu zilikuwa zimeniondolea uvumilivu na kunituma kufanya maamuzi mabaya, muda wote huo nilikuwa kimya, nimemwacha mzee ambaye kwangu mimi ni mzazi aongee, ndivyo nilivyolelewa, kwetu sisi huwa hatufungui midomo kuongea wazazi wakiwa wanasema.
“Eric, mimi sikuwepo hapa nchini, nilikuwa nimempeleka nduguyo kutibiwa huko India, ndiyo maana ulikuwa hunipati kwenye simu, si kwamba nilifanya dharau!” aliongea mzee Kinana kwa upole tofauti kabisa na nilivyotarajia  na kuugusa moyo wangu.
“Kwa hilo naomba unisamehe baba, ningejua umepeleka mgonjwa nje ya nchi wala nisingezungumza maneno hayo, machungu niliyonayo moyoni ni makubwa, niko hatarini kupoteza mali za watoto wangu, nihurumieni!”
Muda mfupi baadaye mlango ulifunguliwa, akaingia mama Zakia Meghji akiongozana na Mohamed Seif Khatibu, niliwaamkia wote, timu nzima ikaanza kunisihi nitulie, nisifanye maamuzi yasiyo sahihi! Kifua changu kilikuwa kimejaa, sikuweza hata kuongea vizuri.
Baadaye mama Meghji na Khatibu waliondoka ofisini kwenda kwenye chumba cha kusubiria wakituacha sisi watatu; Mzee Kinana, Luhwavi na mimi tukiongea juu ya namna ya kulimaliza tatizo, wakakiri chama hakikuwa na fedha wakati huo lakini wangejitahidi kadiri ya uwezo wao kupunguza deni kidogokidogo mpaka limalizike, tukakubaliana kuwa na mawasiliano ya karibu badala ya kukaa kimya.
Niliondoka ofisini kwa mzee Kinana moyo wangu ukiwa umetulia kabisa, matumaini yakiwa yamerejea moyoni mwangu kwamba nisingepoteza haki yangu na watoto wangu! Tangu siku hiyo mpaka ninavyoandika kumbukumbu hizi, nina amani mno moyoni mwangu, ingawa sijalipwa, najua ipo siku ambayo haipo mbali nitalipwa nami nimalizane na wanaonidai.
Kuhusu suala la CCM na deni ninalodai hapo ndipo lilipofikia, sina maelezo zaidi ya hapo, nabaki kuwa mwanachama muaminifu wa Chama Cha Mapinduzi, kada aliye tayari kupigana usiku na mchana kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kustawi, nilichofanya ni kutumia uhuru wa kujieleza ambao upo ndani ya Chama Cha Mapinduzi na katiba ya nchi yetu.
Kitu kimoja nataka kuwaeleza Watanzania wenzangu  ni kwamba, wakati umefika wa watu kuachana na hofu nyingi iliyoligubika taifa na kuanza kuzungumza ukweli, badala ya unafiki na kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa hali ambayo inaendelea sana katika nchi yetu.
Hatuwezi kulisaidia taifa hili kama hatutazungumza ukweli, hatuwezi kutengeneza taifa la vijana waoga tu, ambao hawawezi kusimama na kuzungumzia yanayowaumiza, eti kwa sababu watapoteza kazi, watapoteza biashara, watawaudhi watu, la hasha! Kuzungumza ukweli ndiko kuliwafanya wazee wetu wa mwanzo wafanikiwe kuwaondoa Wakoloni katika nchi yetu, leo hii tuko huru kwa sababu walihatarisha maisha yao kwa ajili yetu.
Lazima tuzungumze pale tunapoona mambo hayaendi sawa, lazima tupaze sauti pale tunapohisi tunaonewa! Katika taifa hili watu wamechagua kukaa kimya, hata viongozi wa dini waliotarajiwa kuwa watu wa kwanza kukemea mambo maovu, sasa wanaogopa kusema kwa sababu tu hawataki kuwaudhi watu! Wakati umefika wa kila  mtu kusimama katika sehemu yake na kuzungumza ukweli, kama kweli tunayo nia ya dhati ya kulisaidia taifa letu, vinginevyo tutazama pamoja, hakuna atakayebaki salama.
Silaha ya mnyonge ni kelele, pazeni sauti zetu, Wakristo wanajua, Biblia inamtaja mtu mmoja aitwaye Batimayo, huyu alikuwa kipofu aliketi kando ya njia, akasikia kundi kubwa la watu linapita, alikuwa ni Yesu mponyaji ambaye Batimayo alishasikia habari zake.
“Nani anapita?” Batimayo alimuuliza rafiki yake.
“Yesu Mnazareti!”
Bila kupoteza wakati Batimayo alinyanyuka na kuanza kupaza sauti: “Yesu! Yesu! Nihurumie!” Yesu aliyekuwa amekwishapita eneo hilo alisikia sauti ya Batimayo, akageuka na kutembea mpaka mahali alipokuwa na kumuuliza: “Nikufanyie nini?”
“Ninataka kuona.”
Yesu akamponya Batimayo upofu wake! Sisi pia tukipaza sauti zetu, pamoja na unyonge tulionao tutapata uponyaji kiuchumi, kiafya, kielimu, nk.  Badala ya kuendelea kubaki kimya kama vile hatuumii, huo ni unafiki ambao hakika hautatusaidia chochote, STAND UP AND SPEAK.
Mwisho wa mjadala…
GPL

2 comments:

Anonymous said...

1) Seems to YOU as a good motive, however "PROVEBS 3:7a" is talking to you
2) According to MATTHEW 6:24 and HEBREW 10:34 raise doubt on your TRUE stance in CHRIST

However, you could have listened to your 'father' (“SILENCE IS WISDOM” yaani kubaki kimya ni busara) and the SG words (“Sasa wewe mwanangu umefanya nini tena?” aliniuliza.) means, in the face of the ELDERS you became UNWISE

In the face of GOD (“Sikuwa na jinsi baba, hali yangu ni mbaya sana na hakuna mtu anayeonekana kujali.”)****((mtu anayeonekana kujali)) YOU COULD HAVE PUT YOUR FAITH MORE IN GOD and not (mtu anayeonekana kujali) - JEREMIAH 17:5-8

POLE SANA NA BWANA YESU AKUPE NEEMA YAKE KUENENDA KWA HEKIMA NA KWELI, HASWA PALE UNAPOLITAJA NA KULITUMIA JINA LAKE KATIKA MAKALA ZAKO NA MANENO YAKO

Anonymous said...

Eric. Baada ya kupaza sauti ukasikika imebakia kusubiri haki yako endelea kusubiri na kusali sana mkuu apitishe hiyo vocha!