Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari kuhusu Kaya zilizoondolewa kwenye Mpango wa kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya TASAF Tatu kwa kukosa sifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam kuhusu Kaya zilizoondolewa kwenye Mpango wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF), Awamu ya Tatu kwa kukosa sifa. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ikulu, Bw. Peter Ilomo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Susan Mlawi.
Serikali imeondoa kaya 55, 692 katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), Awamu ya tatu kutokana na sababu mbalimbali. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo jijini Dar es salaam.
“Sababu za kuondolewa kwa kaya hizo ni kifo, kuhama kijiji/mtaa ambapo mpango haujaanza kutekelezwa, kutojitokeza mara tatu mfulululizo kupokea ruzuku, mnufaika kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali za mpango, wastaafu, viongozi wa watumishi wa Umma.” Waziri Kairuki alisema na kuongeza hilo lilibainika baada ya uhakiki alioagiza kufanyika mwezi Februari, 2016.
Waziri Kairuki alisema katika uhakiki huo kaya zilizokuwa na mwanakaya aliyefariki au wote kufariki zilikuwa 13, 898, kaya zilizohama vijiji/mitaa ambapo mpango haujaanza kutekelezwa 6,228. Aliongeza kaya ambazo hazikujitokeza mara tatu mfululizo kupokea ruzuku zilikuwa 17,746, zilizothibitishwa kuwa sio masikini zilikuwa 13,468 na kaya zilizogundulika kuwa na baadhi ya wanakaya wajumbe wa kamati za usimamizi za Jamii, Halmashauri za Vijiji/Kamati za Mitaa, Viongozi na watendaji zilikuwa 4,352.
Mhe. Kairuki aliainisha kuwa kufuatia agizo lake alilotoa mwanzoni mwa mwaka huu hadi Septemba 2016 kiasi cha shilingi 6,427,110,309 kimeokolewa kwa kaya 42, 035 zilizoondolewa kwa kipindi hicho, na kusisitiza kiasi hicho kitaongezeka kwasababu zoezi hilo linaendelea.
Waziri Kairuki alifafanua kuwa ameshauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuwasimamisha waratibu wa TASAF Wilaya na uchunguzi kufanyika wa jinsi walivyojihusisha kuvuruga utekelezaji wa mpango kwa kuandikisha kaya zisizo na sifa.
Kufuatia hilo, Waziri Kairuki alimwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF kuwasimamisha kazi mara moja na kuendelea na hatua za kinidhamu kwa Maafisa Washauri na Ufuatiliaji 106 walioko kwenye Halmashauri walioshindwa kufuatilia na kusimamia mpango hivyo kusababisha kaya zisizostahili kuingizwa kwenye Mpango na kuendelea kulipwa isivyostahili.
Wengine alioelekeza kusimamishwa ni Maafisa watano wa TASAF Makao Makuu wanaosimamia mpango, pamoja na Mameneja Uratibu na Mkurugenzi wa Uratibu ambao ndio wasimamizi wakuu. Pamoja na hayo, Waziri Kairuki ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja ili kubaini ushiriki wa Maafisa hao na kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaothibitika kuhusika katika kuvuruga utaratibu wa utekelezaji wa mpango au kuwepo udhaifu katika usimamizi, ufuatiliaji na uwajibikaji.
Waziri Kairuki alielekeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya wahakikishe kuwa fedha zote zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa zinarejeshwa ili ziwanufaishe walengwa.
Waziri Kairuki alitoa rai kwa wananchi na wadau wote wa Mpango wa TASAF kutoa taarifa za watu wote ambao wananufaika lakini hawastahili kuwa kwenye Mpango ili malipo yasifanyike kwa wote wasiostahili.
Awamu ya Tatu ya TASAF ilianza mwaka 2012 ambapo Serikali inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini. Kaya zilizoandikishwa idadi yake ni 1,110,635, na kaya hizo huandikishwa baada ya hatua ya utambuzi ambayo jamii husika hushirikishwa katika mikutano ya pamoja kwa kuweka vigezo vya umasikini na baadaye kaya hizo hufanyiwa uhakiki kwa kutumia takwimu na viashiria vya umasikini. Takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania takribani 28.2% bado ni masikini sana, na serikali hadi sasa imeshatumia shilingi 391,835,484,755 zilizolipwa katika mikupuo nane kwa kaya 1,110,635
1 comment:
Hii TUtaisoma sana namba 0-9 kwani Tulishiba kula na kumywa sana hela hii ya TASAF! Dah hi balaah hatutakaasahau! Wengine tulikuwa na nyumba na madirisha!!
Post a Comment