Shirika la Umoja wa Mataifa nchini limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Wahanga wa Maangamizi Makuu ya Moto dhidi ya Wayahudi kwa kuwakutanisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Dar es Salaam na kuwapa elimu kuhusu maangamizi hayo. Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Stella Vuzo alisema ni jambo jema kwa wanafunzi hao kupata elimu kuhusu maangamizi ambayo yalifanywa na kiongozi wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler kwani hata wao wanaweza kuja kuwa viongozi kwa miaka ijayo hivyo kama watapatiwa elimu mapema watajifunza ni mambo gani kiongozi anapaswa kufanya na yapi hapaswi kwa faida ya kila mmoja. “Kwa nyie kama wanafunzi ambao kwa miaka ya baadae wengine mtakuwa viongozi mnapaswa kujifunza kwa jambo kama hili ambalo alifanya Hitler kuwa sio jambo jema, kila binadamu ana haki sawa hakuna ambaye anamshinda mwenzake na huo ndiyo msimamo wa Umoja wa Mataifa,” alisema Vuzo.
Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Stella Vuzo akizungumza na wanafunzi kutoka shule ya Chang'ombe, Kibasila, Jitegemee, Kigamboni, Dar es Salaam, Gerezani, Airwing na vijana kutoka Temeke Youth Development Network (TEYODEN) kuhusu Siku ya Kimataifa ya Kuadhimisha na Kuwakumbuka Wahanga wa Maangamizi Makuu ya Moto ambapo watu mil. 55 wanakadiriwa kuwa walipoteza maisha. (Picha na Rabi Hume - MO Dewji Blog)
Aidha Afisa Habari huyo alizungumza kuhusu siku mauaji ambayo yalifanywa na Hitler wakati akiwa kiongozi wa Ujerumani katika kipindi cha mwaka 1933 hadi 1939, “Alikuwa akichagua watu ambao wanaonekana kuwa tofauti na kuwaondoa katika jamii ya Wajerumani, anawapeleka katika kambi maalumu na anawaua wengine wanawekwa katika kambi maalumu wanafanyishwa kazi ngumu bila malipo na waliokuwa wanashindwa na wao wanauawa kwa kuchomwa moto hadi kufa, Vuzo aliongeza kwa kusema kuwa, “Mauaji ya moto ni mauaji hatari kuwahi kutokea duniani, ilikuwa ni dhana ya Adolf Hitler kutaka Wanazi kuwa ni watu ambao wamenyoka lakini kumbe ilitakiwa aishi na watu wote katika jamii lakini alipinga hilo,” “Lakini pia alikuwa hawapendi Wayahudi, walikuwa wafanyabiashara wazuri lakini yeye aliwapinga na hata akawa anawambia wananchi wake kuwa Wayahudi kuwa hawafai katika jamii na wasinunue kitu chochote kutoka kwao.”
Afisa Habari wa Ubalozi wa Ujerumani nchini, Susann Keller akizungumza kuhusu Siku ya Kimataifa ya Kuadhimisha na Kuwakumbuka Wahanga wa Maangamizi Makuu ya Moto.
Kwa upande wa Afisa Habari wa Ubalozi wa Ujerumani nchini, Susann Keller alisema kitendo ambacho kilifanywa na Hitler hakikubaliki na ni jambo ambalo Wajerumani wamekuwa wakijutia kila muda kutokana na vitendo vya kikatili ambavyo vilifanyika vilivyosababisha watu wanaokadiriwa kufikia milioni 55 na kati yao milioni sita wakiwa ni Wayahudi kupoteza maisha. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Elimu kwa ajili ya maisha Bora ya Baadae.” Na Rabi Hume, MO Dewji Blog
Wanafunzi kutoka shule ya Chang'ombe, Kibasila, Jitegemee, Kigamboni, Dar es Salaam, Gerezani, Airwing na vijana kutoka Temeke Youth Development Network (TEYODEN) wakiangalia video inayoelezea historia ya Adolf Hitler na mauaji ambayo alikuwa akiyafanya.
Baadhi ya wanafunzi wakitoa maoni na kuuliza maswali.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja.
No comments:
Post a Comment