Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Tamasha la Uelimishaji na
Upimaji Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na
vijana kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi Kinyerezi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala akihutubia wakati wa Tamasha la Uelimishaji na Upimaji Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasioambukiza kwa watoto na vijana lililofanyika kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi Kinyerezi, mgeni rasmi kwenye Tamasha hilo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Watoto wakionesha umahiri wao katika kucheza ngoma za asili.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimu watoto waliotoka kupata chanjo.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka
wananchi kote nchi kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto
kijinsia ili waweze kukamatwa na kuchukua hatua za kisheria kama hatua ya
kukomesha vitendo hivyo ambayo vimeanza kushamiri katika baadhi ya jamii
nchini.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo
hilo katika hotuba yake ya kuhitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ambayo ilitoa huduma bure za vipimo na matibabu kwa watoto na vijana
zaidi ya 1500 kampeni ambayo iliambatana na maadhimisho ya siku ya mtoto wa
Afrika katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi mkoani Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema kuwa watenda maovu hao
lazima vifichuliwe na wananchi, walezi pamoja na wazazi kwa kuwa watu
wanaofanya vitendo hivyo vya udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii.
Katika
kukabiliana na hali hiyo, Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya dola kutofumbua
macho vitendo hivyo bali pindi wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji
wa watoto wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki
watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya.
Makamu wa
Rais pia ametoa wito maalum kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote
nchini waache kuwaficha watu wanaotendea vitendo hivyo vibaya bali wawapatie
taarifa walimu wao na polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.
Amesema kwa
kufanya hivyo watoto watakuwa salama katika mazingira ya nyumbani na wakiwa
mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo watawajibishwa kulingana
na matendo maovu waliyokuwa wanawafanyia watoto hao.
“Mtoto anaweza kufaidika na fursa
sawa iwapo tu atalindwa kwa kuwezeshwa kuwa afya bora”, Amesisitiza Makamu wa Rais.
Kuhusu
kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameendelea kuua watu kwa kasi
katika nchi zinazoendelea Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.
Amesema ipo
haja ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na tatizo hilo kwa ushirikiano wa
wadau wote kwani janga hilo linagharimu taifa na wananchi wake wakiwemo watu
wazima, watoto na vijana.
“Magonjwa yasiyo ya
kuambukiza yasipodhibitiwa yatapunguza uzalishaji mali,ufanisi mahali pa kazi
na hata shughuli za ulinzi na usalama nchini mwetu na hivyo pato la taifa
litapungua na taifa kuwa watu maskini kutokana na magonjwa hayo”, Alifafanua Makamu wa Rais.
Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo
ya kuambukiza Serikali imeweza kupanua maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa
saratani nchini kwa kujenga jengo jipya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean
Road na kuongeza majengo mapya ya huduma za saratani kwenye Hospitali za Rufaa
ya kanda ya Bugando mkoani Mwanza.
Amesema
Serikali pia imejenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo ni taasisi ya
mfano ya kutibu maradhi ya moyo ambapo kutokana na kujengwa kwa taasisi hiyo
Serikali imefanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambayo yangetumika kuwagharamia
wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt
Hamisi Kingwangala amemhakikishia Makamu wa Raia kuwa Wizara hiyo itaendelea
kuweka mipango na mikakati imara ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza nchini.
Dkt Kingwangala
ameomba wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kidini na wadau wengine
kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuongeza kasi ya kukabiliana na magonjwa
hayo ili yasiendelee kuteketeza maisha ya watu nchini.
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
No comments:
Post a Comment