ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 17, 2017

WABUNGE WARARUANA SAKATA LA MAKINIKIA


Na KULWA MZEE-DODOMA

BUNGE limeingia siku ya nne jana kujadili Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2017/18, huku wabunge kadhaa wakiraruana kuhusu ripoti ya pili ya kamati iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli, kuhusu mchanga wa dhahabau (makinikia) pamoja na mikataba ya madini.

Ripoti ya kamati hiyo pamoja na watu wengine iliwataja baadhi ya vigogo wa Serikali kuhusika moja kwa moja katika kusaini mikataba mbalimbali ya madini na kupendekeza vyombo vya dola viwachunguze.

Waliotajwa na ripoti hiyo ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja katika Serikali ya awamu ya nne kuanzia 2008 hadi 2012.

Mwingine ni aliyewahi kushika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, kuanzia mwaka 1993 hadi 2005 na Dk. Dalaly Kafumu aliyepata kuwa Kamishina wa Madini katika wizara ya Nishati na Madini kati ya mwaka 2006 na 2011.

Aliyekuwa wakwanza kuchafua hali ya hewa bungeni ni Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga (Chadema), aliyemkatisha Ngeleja wakati akichangia bajeti hiyo aliyewataka wabunge wanyanyuke kwenye viti vyao ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono Rais Dk. Magufuli katika kupambana na wizi wa rasilimali za taifa.

Wakati Ngeleja akichangia, Haonga alisimama na kuomba kumpa taarifa Ngeleja ambapo alisema. “Naomba kutoa taarifa, mheshimiwa Ngeleja yeye ni miongoni mwa wabunge waliotajwa katika kashfa hii ya makinikia, anapokuwa anachangia atuambie uhusika wake katika hili”.

Kabla Ngeleja hajasimama kujibu hilo, Mwenyekiti wa Bunge aliyekuwa akiongoza kikao hicho jana asubuhi, Mussa Zungu, alisema hiyo siyo taarifa na hivyo kumtaka Ngeleja kuendelea na mchango wake.

Hata hivyo Ngeleja kabla ya kuendelea alisema: “Haonga mdogo wangu anajua kutuhumiwa si kupatikana na hatia, maisha yanaendelea.

“Sisi Bunge tumetoa pongezi kwa rais kwa kazi kubwa aliyofanya, tumpongeze mheshimiwa rais, kwa hali tuliyofikia tunahitaji usimamizi wa sera, nimekuwa waziri kwa miaka mitano, tungeanza utaratibu wa kawaida kuboresha mikataba ya madini ingetuchukua miaka mingi kufikia hapa,” alisema.

Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM), akichangia bajeti hiyo alipigilia msumari wa moto kwa kusema waliohusika wote wakamatwe kabla ya kuhojiwa.

“Nampongeza Rais na Profesa (Nehemiah Osoro- Mwenyekiti wa Kamati ya pili ya makinikia), aliwataja watu waliosababisha matatizo, wengine wako CCM, tusema ukweli tuache mzaha.

“Wengine wanaweka katika twitter eti sihojiwi mpaka mahakamani, wengine tunawaheshimu, mzee wetu humu ndani anatwitt eti hawezi kuhojiwa hadi mahakamani, kila mwaka, kila tuhuma anatajwa kwani yeye ni nani?

“Kama kuna uwezekano wakamatwe washtakiwe, wanaotusumbua humu ni hao hao waliotajwa….. katajwa Ngeleja, katajwa Chenge, katajwa Kafumu” alisema Msukuma na kuendelea:

“Nimefuatilia taarifa zote hata Rais Magufuli alipomtumbua aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,..sijui kama yumo humu….nina hamu naye.

“Rais Magufuli alisema aliyaamini ma – vyeti, tuangalie uwezo wa mtu ikiwezekana mawaziri wafanyiwe usaili kabla ya kupata nafasi.

“Tunaamini madigrii mwisho wa siku tunakuta wezi, tufanye kitu cha msingi, tusiamini haya madigrii, kuamini haya madigrii kunatuletea matatizo, zile Phd zimerudi kwetu,”alisema Musukuma.

Alisema watu wengi hawana vyeti, hawana elimu, Katiba inasema ukitaka cheo fulani inataka elimu kubwa sasa wamefoji hayo madigrii, uwezo ni mdogo makaratasi makubwa.

Kubenea

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), alisema wabunge wa CCM wamezungumza mengi kwamba wapinzani hawaungi mkono hoja ya kukomboa rasilimali.

Alisema wapinzani hawapaswi kuingia kwenye lawama hizo kwakuwa hawahusiki katika mikataba yote kwani hawajawahi kuingia katika Serikali na kwamba kazi hiyo ni ya CCM.

“Sisi hatuhusiki katika mikataba yote iliyofungwa, hatujawahi kuingia katika Serikali, hii ni kazi ya CCM…ni dudu lao wameliamsha wahangaike nalo.

“Imekuwepo hoja ya msingi kwamba eti tumeibiwa katika rasilimali zetu, tumeibiwa na watu waliokuja kuwekeza, mikataba ilifungwa kwa sheria zilizopo, walifunga mikataba… bahati mmoja wao kazungumza hakamatiki.

“Rais alikaa na aliyemwita mwizi jana, mlango wa Ikulu jana ulifunguliwa ukawa wazi mwizi akaingia Ikulu,” alisema.

Kafulila, Zitto waombwe radhi

Akichangia mjadala huo wa bajeti, Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida (CUF) alisema wabunge warudi majimboni wakaombe radhi wananchi kwani wao ndiyo walipitisha sheria za madini.

“Tuliapa kwa kushika kurani na biblia, kurani na biblia ni vitabu vya Mwenyezi Mungu havitakiwi kudanganya, huwezi kuapa kisha ukazungumza uongo, unashika kurani ama biblia alafu ukaja kubadilisha ukazungumza mengine, kila siku tunasema tumerogwa na nani, tumerogwa na kurani na biblia.

“Mara nyingi ukiwa mkweli hukubaliki, kuna wakereketwa na wanaharakati walionesha hali ya madini ngumu, Dk. Hamisi Kigwangala ubunge wake ulikuwa wataabu kwa sababu alisimamia na kupinga madini haya yasiibwe hayachakachuliwi, alipigwa mabomu, aombwe radhi.

“David Kafulila ambaye alikuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) akaitwa tumbili, Zitto Kabwe alikuja na hoja nzito mwisho wa siku hapana ikawa ndio”alisema mbunge huyo.

MTANZANIA

No comments: