SERIKALI imekubali kulifanyia kazi ombi la Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy la kutaka taasisi za umma ziwe
zinanunua mafuta ya kampuni hiyo yenye ubia wa asilimia 50 kwa 50 na Serikali ili faida inayopatikana itumike kwenye
kutatua changamoto za Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa Mjini Dodoma jana baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Dk Ben Moshi kutoa ombi
hilo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango wakati wa tukio la kampuni hiyo kutoa gawio la Sh bilioni 7
kwa Serikali ambayo ni faida iliyopatikana kutokana na biashara ya mafuta.
Akikubali ombi hilo Dk.Mpango alisema kuwa watalifanyia kazi ombi hilo hasa kwa kutambua hata mchango wa
kampuni ambazo zimewekeza nchini na zina ubia na Serikali huku akitoa angalizo kuwa pamoja na ombi hilo
kufanyiwa kazi hakuna sababu ya Puma kubweteka kwani lazima ushindani uwepo ili kupatikana kwa bidhaa bora.
"Serikali tumefurahi kwa gawio hili ambalo mmelitoa kwani fedha hizi zitakwenda kuhudumia Watanzania masikini
ambao wanahitaji kupata huduma muhimu.Hivyo niwahakikishie Puma ombi lenu nimelisikia na tunalifanyia kazi lazima
tuendelee kushirikiana ili kuwa na uwekezaji wenye tija kwa nchi yetu,"alisema Dk.Mpango.
Pia alitumia nafasi hiyo kuitaka kampuni ya Puma kuendelea kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi ili mwaka ujao wa
fedha gawio liongezeke zaidi na kuwahakikisha Serikali inalo jicho lake ambalo linaangalia kwa kampuni zote na
mashirika ambayo wana ubia nayo.
Awali kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya Sh bilioni 7 kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mwenyekiti wa Bodi ya
Puma Dk. Mosha alisema kuwa wanatambua majukumu yao kwenye kufanyabiashara ya mafuta na ndio kampuni
ambayo inaongoza kwenye soko lakini ombi lao kwa Serikali ni kwamba itoe maelekezo kwa taasisi na mashirika ya
umma kununua mafuta kutoka kwao.
Alisema wanaamini ombi hilo likifanikiwa wataongeza mapato na faida kwa kampuni hiyo ambayo kwa sehemu kubwa
ni kama ya Serikali na hivyo gawio litaongezeka zaidi ya lilitolewa jana huku akisisitiza jukumu lililopo mbele yao ni
kuhakikisha wanaendelea kuwa bora katika utoaji wa huduma ya mafuta nchini.
"Kampuni yetu ina ubia na Serikali, hivyo tunaomba kama Waziri utaona inafaa mtoe maelekezo maalumu ili kuzifanya
taasisi za umma kununua mafuta kwetu.Hii itatuwezesha kupata fedha nyingi na hivyo kuongeza gawio kwa Serikali
.Tunatamani kuona tukija tena mwakani tunatoa fedha nyingi zaidi ya hizi Sh bilioni 7,"alisisitiza.
Wakati huo huo, Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania Limited Philippe Corsaletti, alisema kuwa uongozi wa
kampuni hiyo unapongeza juhudi za Rais John Magufuli ya kuhakikisha Serikali inatekeleza mikakati yake ya kukusanya
kodi na kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje na ndani.
Pia alisema kuwa ufanisi wa kibiashara wa kampuni hiyo kwa mwaka 2016 ulikua mzuri kwa pande zote za mauzo
pamoja na mapato. "Ufanisi wetu mkubwa unatokana zaidi na biashara ya mafuta ya ndege ambako kwa sasa sisi ndio
tunaongoza katika soko."
Alisisitiza wakati wakitoa gawio hilo la Sh bilioni 7 kwa Serikali, jambo kubwa ambalo linawapa faraja ni juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais ,Dk.John Magufuli ambaye pamoja na mambo mengine ya kuleta
maendeleo ameimarisha mfumo wa kukusanya kodi na kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje na ndani kama
ilivyooneshwa kwenye bajeti ya 2017/2018.
"Puma imekuwa ikifuatilia kwa karibu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya tano, na kuridhishwa na utendaji wake,
hivyo uongozi wa Puma Energy utaendelea kutoa ushrikiano kama ambavyo wamekua wakishirikiana siku zote.
"Pia tunafurahishwa na hatua ambazo Rais wetu anachukua katika kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinawanufaisha
Watanzania wote, hivyo Puma tutaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano,"alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu gawio ambalo wamelitoa kwa Serikali Meneja huyo wa Puma alisema kufikia mwisho wa
mwaka ulioishia Desemba 31 mwaka 2016 kampuni hiyo ilitengeneza faida kabla ya kodi ya jumla ya
Sh bilioni 35.5 na kufafanua Puma Energy iliwekeza kwa nguvu katika kipindi cha mwaka 2016 ili kuboresha
miundombinu yake ya ndani na rasilimali zake.
"Lengo letu lilikuwa ni kuimarisha uwepo wake sehemu mbalimbali na kukuza biashara yake. Hivyo kutokana na
mazingira mazuri ya biashara bodi ya wakurugenzi imependekeza gawio la Sh.bilioni kwa mwaka ulioishia 2016 iweze
kulipwa kwa Serikali kutokana na utendaji mzuri wa kampuni.Mwaka 2015 gawio lilikua Sh bilioni 4.5 bilioni na hivyo
hiyo inawakilisha ongezeko la asilimia 56 ukilinganisha na mwaka jana na hii ni sambamba kabisa na mkakati wa
kampuni,"aliongeza.
Alitumia nafasi hiyo kuelezea majukumu ya kampuni hiyo ni masoko na usambazaji wa bidhaa za petroli ndani ya
Tanzania na kufafanua wanao uwezo wa kuhifadhi lita za mafuta milioni 94, vituo 47 vya mafuta maeneo mbalimbali
nchini na inahudumia viwanja vinane vya ndege.
Mwisho
No comments:
Post a Comment