Dar es Salaam. Maagizo yanayotolewa na baadhi ya wakuu wa wilaya ya kukamatwa kwa watu wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa na kuswekwa mahabusu kwa saa 48 imeelezwa kuwa yanakiuka baadhi ya taratibu.
Juzi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na kuwekwa mahabusu kwa saa 48 kwa kile alichodai alitoa kauli za kichochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
“Maneno yake ni ya kichochezi na hayakubaliki, hayafai kutolewa na kiongozi kama yeye hivyo namuagiza kamanda amkamate Mdee amuweke ndani kwa saa 48 ili ahojiwe (kwa) yale yote aliyoyaongea ili afikishwe kwenye vyombo vya usalama,” alisema Hapi alipotoa agizo hilo juzi mbele ya waandishi wa habari.
Hadi jana jioni, Mdee alikuwa mahabusu huku kukiwa hakuna taarifa zozote za kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria inayotoa mamlaka hayo.
Hata hivyo, mwezi uliopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene akiwa bungeni mjini Dodoma alionya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa vya kuwakamata watu pasipo na sababu za msingi kwa visingizio vya sheria.
Mbali na Mdee, mwezi uliopita Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alikamatwa wakati akiwa kwenye msafara na viongozi wengine wa Chadema na kuswekwa mahabusu kwa saa hizohizo 48 baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori kutoa agizo hilo kwa madai ya kufanya siasa kinyume na utaratibu.
Hata hivyo, meya huyo aliachiwa huru baada ya muda huo kwisha na hapakuwa na taarifa ya kufikishwa katika vyombo vya sheria kama sheria inavyotaka.
Sheria inasemaje?
Mamlaka hayo hutolewa chini ya Sheria ya Tawala za Mikoa namba 19 ya mwaka 1997.
Wakili wa kujitegemea, Juma Nassoro alisema sheria hiyo hutumika kwa ajili ya kutekeleza jukumu la kusimamia ulinzi na usalama na kwamba viongozi hao wanaweza kuagiza vyombo vya usalama kumkamata mtu yeyote anayeonekana kuhatarisha usalama wa eneo husika ili afikishwe mahakamani ndani ya saa 48.
Alifafanua kuwa kabla ya kutoa agizo hilo, kiongozi husika anatakiwa kuandika sababu za kwa nini mtu huyo akamatwe na kupeleka nakala yake kwa hakimu.
Pia, vifungu vya 7(9) na 15(9) vinatoa maelekezo kuwa endapo kiongozi husika atabainika kutumia vibaya madaraka yake, anaweza kushtakiwa chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai.
“Kiongozi hana mamlaka ya kumweka mtu ndani kama adhabu, bali anakamatwa ili afikishwe mahakamani ndani ya saa 48. Hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kumuadhibu mtu mwingine isipokuwa Mahakama pekee,” alisema Nassoro.
Kuhusu kukamatwa kwa Mdee, wakili huyo alisema mkuu wa wilaya alitekeleza wajibu wake chini ya sheria hiyo na huenda alifanya hivyo baada ya kuona vyombo vya usalama havikubaini suala hilo.
Bavicha wataka wateule wa Rais wapelekwe shule
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kukerwa na adhabu hizo dhidi ya viongozi wake, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limetaka wateule wa Rais wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya wapelekwe shule ili wajifunze mifumo na utendaji wa utumishi wa umma kwa madai kuwa wengi wao hutumia vibaya madaraka waliyopewa hali inayodhihirisha kutojua sheria zinazowaongoza.
Baraza hilo limeitaja Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 kwamba inatumiwa vibaya na wateule hao kwa kutoa matamko na kuwaweka kizuizini baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ilhali sheria hiyo imeeleza bayana jinsi taratibu zinavyopaswa kufuatwa.
Katibu mkuu wa baraza hilo, Julius Mwita alisema jana kuwa wengi wa wateule hao wamekuwa wakitoa amri za kukamatwa viongozi wa Chadema kwa kisingizio cha kulindwa na sheria hiyo.
Alisema wateule hao hawapaswi kutumia vibaya sheria hiyo kwa lengo la kutaka kuwaridhisha wateule wao.
“Ukiangalia sheria hii katika kipengele cha 15, utaona namna inavyoelekeza ni mazingira gani yanapaswa kufuatwa wakati mkuu wa mkoa au wilaya anapotoa amri ya mtu kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda wa saa 48, lakini wengi wa wateule hawa hawafuati kanuni zilizopo na ndiyo maana tunasema wapelekwe masomoni wakajifunze taratibu hizi,” alisema.
Katibu huyo alisema wengi wa wateule hao wanaonekana kulewa madaraka kiasi cha kutoa matamshi yanayokinzana na misingi iliyopo kwenye Katiba. “Hawa watu wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata kanuni za nchi na siyo kutoa matamko ya kutaka kumfurahisha mtu aliyewaweka hapo,” alisisitiza.
Alidai kuwa viongozi wa Chadema wamekuwa wakiandamwa na wateule hao na baadhi yao wamekuwa wakiwekwa kizuizini bila hata kuwa na makosa yoyote.
Kubenea mahakamani kwa kumshambulia Shonza
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kusomewa shtaka la kumshambulia Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Juliana Shonza kinyume na Kifungu cha 240 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 3 katika viwanja vya Bunge.
Hata hivyo, Kubenea ambaye anatetewa na mawakili watano; Jeremia Mtobesya, James Ole Millya, Fred Kalonga, Isack Mwaipopo na Dickson Matata alikana kosa hilo na Hakimu Karayemaha alisema dhamana yake ilikuwa wazi.Alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho, barua kutoka Serikali ya Mtaa na Sh1 milioni. Alitimiza masharti hayo.
Kutokana na upelelezi kutokamilika, kesi hiyo itatajwa tena Julai 26 na mtuhumiwa atatakiwa kuhudhuria bila kukosa isipokuwa kwa ugonjwa, kuuguliwa au msiba.
Imeandikwa na Cledo Michael, George Njogopa na Rachel Chibwete
No comments:
Post a Comment