ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 7, 2017

Serikali yamtega tena Mbowe, kigingi kingine chanyemelea uwekezaji wake

“Mimi sijapata hizo taarifa lakini tuna tatizo
By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Hai. Serikali imetoa siku 30 kwa wawekezaji 50 waliopewa maeneo ya kujenga viwanda na kushindwa kuvijenga, kuwasilisha mipango ya ujenzi vinginevyo watanyang’anywa.

Serikali imetoa orodha ya watu hao na taasisi zilizopewa maeneo katika eneo la Weruweru karibu na kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools, akiwamo mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe.

Katika orodha hiyo, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Taifa wa Chadema anaonekana kumiliki viwanja viwili; kimoja kikiwa na ukubwa wa hekta 1.88 na kingine na hekta 2.17.

Akizungumzia uamuzi huo mpya wa Serikali na sababu za kushindwa kuendeleza eneo hilo kwa miaka 13 tangu yeye na wenzake walipomilikishwa mwaka 2004, Mbowe alisema alikuwa hajapata taarifa hizo, lakini kwa vile yuko njiani kuelekea mkoani Kilimanjaro akifika atafuatilia.

Ataja sababu

Mwanasiasa huyo alisema Serikali inapaswa kulaumiwa kwa kutofikisha miundombinu muhimu katika eneo hilo ikiwamo umeme na badala kutarajia wawekezaji wabebe gharama hizo.

Aliongeza kuwa ni vigumu wawekezaji kufanya hivyo na ni lazima soko lijulikane kwanza na pawepo na mazingira rafiki ya uwekezaji ndipo wawekeze.

“Huwezi tu kukurupuka kujenga kiwanda, ni lazima ujue utazalisha bidhaa gani na soko liko wapi. Serikali bado haijalinda viwanda vya ndani na kusababisha ushindani usio sawa wa bidhaa kutoka nje,” alisema mbunge huyo ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni.

Mbowe aliongeza kuwa ni lazima ufanyike utafiti wa kina hasa katika kipindi hiki ambacho uwezo wa wananchi kununua bidhaa unazidi kushuka siku hadi siku.

“Miundombinu hilo eneo hakuna, kuna ushindani usio sawa na bidhaa za nje, masoko na pia uhakika wa umeme. Zote hizi ni changamoto zinazohitaji utatuzi wa Serikali. Unajengaje kiwanda katikati ya changamoto hizo?” alihoji.

Agizo la DC

Akizungumza na baadhi ya wawekezaji hao juzi, mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa alisema mipango ya ujenzi wa viwanda katika eneo hilo iwe imemfikia kabla ya Agosti 10.

“Mlikuja kuomba mkisema ninyi ni wawekezaji wa viwanda ambao pengine mliidhinishwa na TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania). Kuanzia mwaka 2004 mpaka leo 2017 kwa nini hatuvioni viwanda pale?” alihoji na kuongeza;

“Nimeamua kuwaita si jukumu la kisheria kwamba nitawaita watu wanaomiliki maeneo na kuwauliza kwa nini hamyaendelezi. Si jukumu langu ningeweza kuchukua hatua.”

“Hamjaonyesha nia ya kujenga viwanda. Nataka niwatangazie wawekezaji wengine kuwa Hai lipo eneo la kujenga viwanda ila liko mikononi mwa watu ambao hawapo tayari kujenga viwanda.”

Mkuu huyo wa wilaya alisema ndani ya muda wa mwezi mmoja kuanzia juzi, wawekezaji hao wawe wamewasilisha mipango ya kujenga viwanda, vinginevyo watanyang’anywa maeneo hayo.

“Msipofanya hivyo, tutamuomba mheshimiwa Rais (John Magufuli) abatilishe miliki zenu wapewe watu wengine watakaokuja kujenga viwanda ili Hai nayo iwe ya viwanda,” alisema Byakanwa.

Alisema, “Wamiliki wengi wa viwanja hawasomi masharti ya umilikaji. Wengi waliomilikishwa viwanja miaka ya 1980 kwa sasa hawana ardhi wana makaratasi tu, umiliki wao ulishamalizika na hawajahuisha.”

Mmoja wa wawekezaji katika kikao hicho, Peter Naya alisema alikwama kujenga kiwanda kutokana na gharama za kuvuta umeme kuwa juu na kwamba aliambiwa ni zaidi ya Sh56 milioni.

“Niliwasiliana na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) wakasema lile eneo halina kipaumbele tugharamie wenyewe. Nimetafuta gharama inaenda hadi Sh50 milioni,” alisema mwekezaji huyo.

Kwa mujibu wa mwekezaji huyo, ili kuweza kukusanya mtaji wa kujenga kiwanda cha kati inachukua kati ya miaka mitano na 10, na kusisitiza kuwa changamoto kubwa ni umeme na upatikanaji wa mtaji.

Misukosuko ya Mbowe

Endapo Mbowe atashindwa kuwasilisha mipango ya ujenzi wa viwanda katika eneo hilo na Serikali kumnyang’anya litakuwa ni pigo lake la nne tangu awamu ya tano iingie madarakani.

Pigo la kwanza lilikuwa la kunyang’anywa jengo la Club Billicanas jijini Dar es Salaam ambalo alilitumia kama ukumbi wa starehe na baadaye lilivunjwa.

Kubomolewa kwa jengo hilo lililokuwapo katika barabara ya Mkwepu na Indira Gandhi kulitokana na mgogoro wa umiliki kati yake na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Mbali na tukio hilo, Januari 21, Serikali wilayani Hai ilimpa siku 14 kulipa Sh13.5 milioni alizokuwa akidaiwa kama kodi ya huduma ya hoteli yake ya Aishi Protea.

Ukiacha misukosuko hiyo, mwezi Februari alikuwa miongoni mwa watu waliotajwa kujihusisha na dawa za kulevya na kutakiwa kuripoti kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam.

Haikuishia hapo, ila mwezi Juni, Serikali iling’oa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba lake la kilimo cha kisasa cha umwagiliaji (green house) lililopo Machame wilayani Hai, kwa madai ya kuharibu mazingira.

Mbali na kung’oa miundombinu hiyo, pia Mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), ilimtoza faini ya Sh18 kwa kuendesha kilimo ndani ya mita 60 kutoka kilipo chanzo cha maji.

No comments: