ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 7, 2017

Sheria mpya yaanza kuwachemsha wawekezaji sekta ya madini nchini



By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kutafuta njia za kudhibiti kikamilifu rasilimali za nchi baada ya kupitisha sheria mpya ya maboresho ya Sheria ya Madini iliyopendekeza mambo kadhaa, wawekezaji katika sekta hiyo wameanza kutishika na kuanza kujiondoa.

Baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, tayari mwekezaji mmoja kutoka Australia, Ian Middlemas kupitia kampuni yake ya Cradle Resources, amekosa dili la dola 55 milioni za Marekani (Sh121 bilioni) kupitia mradi wa uchimbaji wa madini ya niobium Panda Hill, uliopo nchini.

Kufuatia hatua hiyo, wataalamu kadhaa wa masuala ya uchumi wamesema ni lazima sheria hizo zitakuwa zimewashtua wawekezaji.

Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Dk Abel Kinyondo alisema watakimbia kwa muda mfupi tu.

Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kutaibuka baadhi ya kampuni ambazo zitafanya hivyo ili kutishia Serikali ili ichanganyikiwe na kubadilisha uamuzi wake.

Kampuni kadhaa katika soko la hisa la Australia, pia zimeripotiwa kusitisha shughuli za utafutaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji nchini, kwa madai kuwa zinatafakari athari ya sheria hizo mpya.

Wiki hii, Bunge lilipitisha mabadiliko ya sheria ambayo pamoja na mambo mengine, imependekeza mambo sita yatakayoleta mapinduzi ya kusimamia katika sekta ya madini nchini ikiwamo kurejesha madini yote chini ya miliki ya nchi na pia, kuweka vipengele vya kupitia upya mikataba ya madini na kuweka ulazima wa Serikali kuwa na hisa katika kampuni ya uchimbaji madini ya aina mbalimbali.

Kwa mujibu wa gazeti moja la Australia, Cradle Resources, ilishauriwa kwamba wasitishe dili hilo lililokuwa litekelezwe kwa ushirikiano na kampuni binafsi ya Tremont Investment.

Tremont ilikuwa iwekeze dau hilo kwenye mradi wa Panda Hill uliopo Tanzania, lakini baada ya mabadiliko ya sheria yaliyofanyika wiki hii bungeni kuhusu sekta ya madini, imeukacha mradi huo.

Mabadiliko hayo yanairuhusu Serikali kutia mkono katika mikataba ya kampuni zote za madini zilizopo nchini.

Katika mabadiliko hayo, inapendekeza Serikali ya Tanzania kuwa na asilimia 16 kutoka katika kila kampuni ya uchimbaji wa madini pamoja na kuwapa mamlaka ya kuwa na hisa mpaka asilimia 50.

Kutokana na mabadiliko hayo, Cradle Resources ilisema endapo sheria hizo zitaachwa kama zilivyo, basi mradi wake huo wa Panda Hill utaathirika.

Soko la hisa la Australia la Jumatatu hii, limetaka kampuni katika soko hilo kusitisha shughuli zao mpaka hapo watakapopata usahihi wa mabadiliko hayo ya sheria yana maana gani. Soko hilo limetaja kampuni nyingine za Tanga Resources and Peak Resources kwamba yote yametolewa katika soko lao la hisa wakati wakiendelea kuchunguza mabadiliko hayo yatakuwa na maana gani.

Baadhi ya kampuni za madini za Australia zikiwamo Kibaran Resources, Volt Resources, Strandline Resources and Magnis Resources, nazo zimesitisha kuuza hisa katika soko hilo ili kuona athari ya sheria hiyo mpya.

No comments: