ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 5, 2017

WATUHUMIWA 4,809 WA DAWA ZA KULEVYA WAKAMATWA

Waziri Mkuu, Mh. Kassim Majaliwa

*Heroine, Cocaine, bangi, mirungi na kemikali bashirifu vyakamatwa
* Mashamba ya bangi ekari 569.25 na mirungi ekari 64.5 yateketezwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miezi minne, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imewakamata watuhumiwa 4,809 na kufungua majalada ya kesi 3,222.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.

“Katika kipindi kifupi tangu Februari, 2017 Mamlaka hii ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu 327.173); cocaine (kilo 26.977); bangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini,” amesema.

Amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.


“Dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Amesema azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio. “Tuungeni mkono kwenye mapambano haya, ili tutokomeze kabisa mtandao huo,” amesisitiza.

No comments: