Moshi. Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia amehoji uhalali wa Chadema kutaka kuwaadhibu madiwani wake sita waliompigia kura mgombea wa NCCR-Mageuzi.
Mbatia ameenda mbali na kuhoji kama kitendo cha madiwani hao kinatafsiriwa na Chadema ni usaliti, ilikuaje wenzao wa Chadema walimpigia kura mwenyekiti wa kamati kutoka CCM.
Juzi, uongozi wa Chadema Wilaya ya Moshi Vijijini uliwaandikia barua madiwani hao ukiwapa wiki mbili kujieleza kwa nini wasiadhibiwe kwa kumpigia kura mgombea wa NCCR-Mageuzi, Filbert Shayo.
Katika uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Shayo aliibuka na ushindi baada ya kumbwaga Deogratius Mushi wa Chadema licha ya chama hicho kuwa na wingi wa madiwani.
Matokeo hayo yalionyesha kuwa Shayo alishinda kwa kupata kura 27 dhidi ya 19 alizopata Mushi, wakati katika baraza hilo Chadema ina madiwani 27 na CCM na NCCR-Mageuzi 19.
Madiwani walioandikiwa barua ni Michael Kilawila (Kindi), Rogers Mmari (Arusha Chini), Exaud Mamuya (Marangu Mashariki), Focus Shio (Kirima) na Haika Lyatuu na Rose Msack wa Viti Maalumu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbatia alisema anashangazwa na uamuzi huo wa Chadema kuwaandikia barua madiwani hao, akihoji njia waliyotumia kuwabaini wakati kura zilikuwa ni siri.
“Hata kama NCCR na CCM waliotupigia kura zote basi kura nane zilikuwa za Chadema na siyo sita. Mbona baraza kivuli la Upinzani bungeni ni la vyama vyote washirika wa Ukawa, kulikoni?” alihoji Mbatia na kuongeza:
“Siamini wala haiingi akilini kwamba huu ni msimamo wa Chadema Taifa. Mama yangu Philomena alinionya kamwe Kichaka kilichokuhifadhi usikitie moto.”
Chadema yajibu
Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alikiri kuwa kitendo cha madiwani wa Chadema kuchagua mgombea wa CCM badala ya Ukawa ni dhambi kubwa zaidi.
“Msimamo wa chama ulikuwa ni kwamba madiwani wetu ambao ni wengi wamchague makamu mwenyekiti kutoka Chadema, lakini kulikuwa na usaliti walienda tofauti,” alisema Lema na kuongeza:
“Lakini kwa hili la madiwani kuchagua mwenyekiti wa kamati kutoka CCM na kumuacha mgombea wa Ukawa (wa NCCR-Mageuzi) ni dhambi kubwa zaidi. Kwa hili naungana na Mbatia.”
No comments:
Post a Comment