ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 31, 2017

Serikali, wananchi wawajibike kwa bomoabomoa hii

Vilio vinavyotokana na makali ya bomoabomoa katika jiji la Dar es Salaam na machozi ya waathirika, vinajenga sababu ya kugawana lawama kati yao na Serikali.

Inawezekana ni kweli katika gharama ya kutafuta maendeleo, lazima wachache waumie ingawa pia kuna uwezekano wa kuchukua tahadhari mapema kupunguza makali kwa kutumia njia rafiki.

Unahitaji uvumilivu kusikiliza maelezo ya mzee Nicomed Leo anayeishi Kimara Stop Over, ambaye ni miongoni mwa waliokumbwa na bomoabomoa.

Kuna taarifa kuwa alizirai mara baada ya nyumba ya jirani yake kubomolewa. Mwenye alikuwa na nyumba nne zenye thamani ya 900 milioni ambazo nazo zimeshabolewa. Ni mwanachi anayedaiwa kujenga kwenye hifadhi ya barabara.

Gharama ya kutafuta maendeleo kwenye ubora wa miundombinu haikuliona hata zuio la mahakama kwa baadhi ya nyumba ambazo tayari zilikuwa na kinga kisheria.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika ni miongoni mwa viongozi walioshangazwa na hatua ya Wakala wa Barabara (Tanroads)kupuuza zuio hilo na kuendelea na bomoa bomoa.

Katika hili tusianze kuwalaumu wananchi kwa kuangalia tulipoangukia, bali turudi nyuma na kugawana lawama kwa kuangalia sababu za anguko hilo.

Maeneo yanayotajwa kuwa hifadhi za barabara, Serikali kupitia taasisi zake, iliboresha miundombinu ya maji na umeme na hivyo kuvutia shughuli za wananchi.

Kama watumiaji wa huduma hizo walizingatia taratibu zote, hakuna shaka kuwa Serikali inastahili lawama kwa kupata mavuno haramu kutoka kwa wananchi waliovamia hifadhi ya barabara.

Hatua ya Serikali kuvuna kodi kwenye maeneo yanayodaiwa kuvamiwa bila kuwaelimisha wananchi hatari iliyopo mbele yao ni kutowatendea haki.

Hii inaweza kufananishwa na ng’ombe aliyekamuliwa maziwa wakati wa kiangazi, ili kuboresha afya ya mgonjwa na baada ya hali yake kuimarika thamani ya mnyama huyo ikapungua.

Ilikuwa ni sawa na kuwahadaa kisaikolojia wananchi kuwa wako salama madamu Serikali imepeleka huduma ya maji na umeme na kupokea kodi ya nyumba.

Operesheni hii inaweza kuleta miundombinu bora ya barabara za kisasa kwenye Jiji la Dar es salaam. Lakini kwa upande wa pili, litaongeza matatizo ya kijamii yanayotokana na athari za kisaikolojia.

Tatizo la wataalamu wetu linaanzia hapa na wengi husubiri kushughulikia matokeo, badala ya kuwekeza nguvu kwenye kinga na elimu ili kuzuia madhara.

Itakuwa ni kujidanganya kuwa kazi ya kubomoa makazi ya watu katika jiji hilo haliwezi kuwa na mchango wa kuongezeka athari mbalimbali kwa viwango tofauti kwa siku zijazo.

Idadi ya nyumba zitakazobomolewa kutoka Kimara hadi Kiluvya ni takriban 1,300 na kuanzia hapo unaweza kupiga picha ya idadi ya vijana watakaopoteza mwelekeo na kuamua kutafuta njia mbadala.

Lipo kundi la wanafunzi watakaolazimika kuachana na masomo, kwa kuwa wazazi wao hawana makazi tena na watahitaji muda wa kuhangaikia makazi kuliko habari ya masomo ya watoto.

Pia, kundi hili litakalokosa malezi kutokana na athari bomoabomoa mbadala wake utakuwa ni kuelekea mitaani. Hasira za kundi la watoto zinajulikana na mara kadhaa wameunda magenge, kufunga mitaa na kufanya uporaji.

Watoto hawa wanaweza kusakwa kila kona ya jiji la Dar es salaam wakapigwa hata kuuawa kama wahalifu, lakini msingi wa tatizo utakuwa unaanzia kwenye athari za machungu ya kubomoa makazi ya wazazi wao.

Kama ambavyo hatutakiwi kufanya baadhi ya mambo hadharani mbele ya watoto, hata wanaposhuhudia nyumba walizoishi zinabomolewa na wao kulala nje, ni kuwajengea mbegu ya chuki na kuamua kujiunga mitaani na makundi yasiyofaa.

Katika hili wajibu wa wataalamu wa saikolojia hauonekani. Hawaonekani nyumba kwa nyumba kuwatuliza waathirika na kuwaandaa waikubali hali yao kabla ya kufikia hatua mbaya.

Waathirika wana haki ya kupata huduma ya kisaikolojia kwa kuwa sehemu ya mapato waliyovuna wakiwa kwenye maeneo wanayofukuzwa leo yalichukuliwa na Serikali yao.

Kama Serikali ingetimiza wajibu kwa kuchukua hatua mapema kwa kuacha kupeleka huduma za maji na umeme, tatizo lisingekuwa kubwa kiasi hiki hata kusababisha lawama kuelekezwa upande mmoja wa wananchi.

Serikali haiwezi kukwepa wajibu wake wa kuhakikisha kazi hii ya ubomoaji haileti madhara ya kisaikolojia, kiuchumi na kijamii. Hata ujenzi wa miji midogo unaoibuka kwa kasi kwenye maeneo ya barabara kuu, wajibu wa Serikali unaanza kwa elimu, maonyo na kuweka mipaka ili kupunguza ukubwa wa madhara hapo baadaye.

Phinias Bashaya ni mwandishi mkoani Kagera. 0767489094

MWANANCHI

No comments: