Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka amelipa faini ya Sh35 milioni hivyo kukwepa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka sita jela.
Adhabu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jumatano wiki hii baada ya Mattaka na mwenzake kutiwa hatiani katika mashtaka sita yaliyokuwa yakiwakabili yakiwemo ya kununua magari 26 chakavu kinyume cha sheria.
Mwingine aliyehukumiwa adhabu kama hiyo ni Elisafi Ikomba, aliyekuwa kaimu mkuu wa kitengo cha fedha ATCL.
Ikomba ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Pentekoste Motomoto alilipa faini ya Sh35 milioni Septemba 13 muda mfupi baada ya hukumu kusomwa.
Mshtakiwa mwingine, William Hajji aliyekuwa mkaguzi wa ndani wa ATCL, aliachiwa huru na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Hakimu Nongwa licha ya adhabu ya kulipa faini au kutumikia kifungo, pia amewaamuru Mattaka na Ikomba ndani ya mwezi mmoja wawe wamelipa Dola 143,442.75 za Marekani wanazodaiwa kuisababishia hasara Serikali.
Mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 14 wa upande wa mashtaka na wa utetezi.
Mattaka na Ikomba walitiwa hatiani katika shtaka la kula njama, mashtaka manne ya matumizi mabaya ya madaraka na moja la kusababisha hasara.
Hakimu Nongwa katika shtaka la kula njama aliamuru kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika mashtaka manne ya matumizi mabaya ya madaraka, kila mshtakiwa aliamriwa kulipa faini ya Sh5 milioni kwa kila kosa au katika kila kosa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika shtaka la kusababisha hasara, Hakimu Nongwa aliamuru kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh10 milioni au kutumikia kifungo cha miaka sita jela.
Hakimu Nongwa aliamuru vifungo kutumikiwa kwa pamoja, hivyo iwapo kila mmoja angeshindwa kulipa jumla ya Sh35 milioni, angetumikia kifungo cha miaka sita jela. Pia, alisema wana haki ya kukata rufaa.
Kabla ya hukumu kutolewa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa alisema hawakuwa na kumbukumbu za makosa mengine dhidi ya washtakiwa bali aliomba adhabu stahiki itolewe kulingana na makosa yao.
Mattaka aliiomba Mahakama impunguzie adhabu akisema magari yanayodaiwa kuwa yalinunuliwa yakiwa chakavu yanaendelea kutumika hadi sasa ATCL na hawajawahi kununua mengine.
Alidai upatikanaji wa magari hayo ulikuwa wa dharura na alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kulinusuru shirika, hivyo aliomba mahakama izingatie kuwa yeye ni binadamu na alikuwa akifanya uamuzi akiwa mkurugenzi mtendaji.
Alisema ana umri wa miaka 66 akikaribia 67, kiafya ana matatizo ya ugonjwa wa shinikizo la damu, ana mke na watoto wanaomtegemea na anamlea mzazi wake mwenye miaka 85, hivyo aliomba hayo yazingatiwe katika kutolea uamuzi.
Francis Mgale, wakili aliyemwakilisha Ikomba alisema mteja wake ni askofu mwenye kundi kubwa la watu wanaomtegemea kwenye neno la Mungu na anahubiri amani.
“Mahakama ifikiri mtu wa aina gani anapewa adhabu kiasi gani kwa sababu ni askofu, hakutenda kosa hilo kwa makusudi alifanya kutokana na mazingira aliyoamini anaitendea haki ATCL,” alisema Mgale.
Ikomba aliomba msamaha akisema, “Naomba msamaha wa hukumu itakayonifanya kuanzia sasa nishindwe kuhubiri Injili ya Yesu Kristo na mimi ni baba ninayetegemewa, nina mke na watoto watatu, watoto wawili yatima na wengine watatu ninaowalea, pia nina mama yangu mzazi ambaye mumewe alifariki miaka 22 iliyopita.”
Hakimu Nongwa alisema mahakama inachukua kigezo cha kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na maombi kama ni muhubiri au mazingira ya shirika lilikuwa katika hali mbaya si kigezo.
Washtakiwa wametiwa hatiani kwa matumizi mabaya ya madaraka na ununuzi wa magari chakavu kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004. Makosa hayo wanadaiwa kuyatenda mwaka 2007 jijini Dar es Salaam.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment