Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani( wa pili kushoto)akikagua kituo cha kupokea na kupooza umeme cha Ilala wakati wa ziara yake ya kukagua Mradi wa kuimarisha miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Dar es salaam, kushoto ni Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ilala, Mhandisi Atanasius Nangali ambaye ndiye msimamizi wa kituo cha cha Ilala na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) Mhandisi Titus Mwinuka( kulia).
Moja ya Transfoma mpya zilizofungwa katika vituo vya Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya umeme kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Sehemu ya mitambo ya kupokea na kupoza umeme katika vituo vya Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya umeme kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Sehemu nyaya zilizotandazwa chini ya ardhi zinazotoka na kuingia katika Vituo vya Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya umeme kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Na Zuena Msuya
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani amesema kuanzia sasa ni marufuku nishati ya umeme kukatika katika jiji la Dar es salaam, kwa kuwa Mradi wa kuimarisha miundombinu ya nishati hiyo imekamilika.
Dkt. Kalemani alisema hayo Octoba 2, 2017 wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi huo, uliojengwa na Serikali kwa msaada wa Serikali ya Japani kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa ajili ya kuimarisha huduma ya upatikanaji umeme katika jiji la Dar es salaam, ikiwemo maeneo ya hospitali, biashara, viwanda na makazi ya watu.
Dkt. Kalemani alisema kuwa mradi huyo ulijengwa mahususi kwa mkoa wa Dar es salaam, kwakuwa kwa sasa ni jiji hilo ni la kibiashara hivyo matumizi ya nishati ya umeme yanaongezeka kwa kasi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Aidha aliweka wazi kwamba, ameridhishwa na kufurahishwa na kasi ya ujenzi ya utekelezaji wa mradi huo, uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 66.4 za kitanzania, ambao umejengwa kwa kipindi cha miaka miwili na nusu badala ya mitatu kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Akizungumzia utunzaji wa vituo hivyo, Dkt. Kalemani aliwataka Mameneja na wasimamizi wa vituo hivyo kufanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa, na kuhakikisha kuwa ukarabati wa mara kwa mara unafanyika ili viweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani alitembelea vituo vitano vya kupooza umeme vilivyojengwa ambavyo ni pamoja na kituo cha Muhimbili, ambapo pamoja na mambo mengine aliagiza kutokukatika kwa umeme katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete,(JKCI) na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili( MUHASI).
Alitoa agizo hilo kwa kuwa kito hicho kinauwezo wa kutoa umeme wa megwati 12 na mahitaji halisi ya umeme katika maeneo hayo ni megawati 4 tu mpaka sasa.
“Mradi wa kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa jiji la Dar es salaam, umekamilika kabla ya wakati uliopangwa , hongereni sana, sitarajii kusikia kwamba umeme umekatika katika jiji hili wala katika hospitali zote za Mkoa wa Dar es salaam, na endapo itatokea aliyehusika atawajibika” alisisitiza Dkt. Kalemani
Pia, alitembelea kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Ilala ambacho baada ya ukarabati wa miundombinu yake, kwa sasa kinauwezo wa kuhudumia wateja zaidi ya laki moja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kilikuwa kinahudumia wateja 40 Elfu.
Pamoja na kituo hicho, njia mpaya ya umeme wa Kv 132 kutoka Ubungo imejengwa, hivyo kuimarisha upatikanaji wa uhakika na wa kutosha wa umeme katika Hospitali ya Amana , Maeneo ya biashara, na Makazi ya watu.
Sambamba na hilo, Dkt. Kalemani pia alitembelea kituo cha Mwanyamala ambacho kinauwezo wa kutoa umeme wa megawati 12, na mahitaji halisi kwa sasa ni megawati 6 tu.
Aidha alitembelea vituo vya Jangwani na Masaki ambavyo pia vinauwezo wa kutoa megawati 12 za umeme, hivyo kuagiza kuwa ni marufuku kukatika kwa umeme katika maeneo yote yanayozunguka vituo hivyo zikiwemo hoteli kumbwa na makazi ya watu.
No comments:
Post a Comment