Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Bw. Tickson Nzunda akizungumza na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mkutano wa mwaka wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii na kuwaasa kuleta mabadiliko katika maeneo yao kwani wao ni wanajeshi wa maendeleo. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wana jukumu la kuhamasisha wananchi kubadili fikra zao ili wawe na mtazamo chanya unaowapa hamasa ya kushiriki kazi za kujitolea ili kujiletea maendeleo yao wenyewe na Taifa lao.
Hayo yamezungumzwa Mjini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu kutoka OR TAMISEMI Bw. Tickson Nzunda wakati wa Mkutano wa Mwaka kwa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii na kuwataka washiriki kufanya kazi zao kwa umahiri, kujenga uelewa kwa viongozi wa Halmashauri, kuchochea mabadiliko sehemu za mitaani na vijijini, kuelimisha jamii kubadili mitazamo na fikra, na hivyo kukuza ari ya wananchi kushiriki maendeleo ili kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Pamoja na mambo mengine, Naibu Katibu Mkuu amewataka Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kuratibu shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu ili kuhakikisha kuwa mashirika hayo yanakuwa na mchango unaokusudiwa katika kufanikisha mipango ya Halmashauri, Mikoa na Taifa ili kuboresha ustawi na maendeleo ya watu.
“Tunatarajia kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiseriklali yangehakikisha kuwa yanasaidia kutoa mchango katika kuwekeza kwenye uwekezaji wa vipaumbele vya kitaifa vilivyoainishwa ikiwemo kuboresha miundo mbinu ya elimu mashuleni ili kuwa na mazingira wezeshi ya kufundishia na kujifunzia, jambo ambalo halifanyiki ipasavyo” alisema Bw. Nzunda.
Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga amefafanua kuwa watumishi wa maendeleo ya jamii ndiyo washawishi na waragibishi wakuu katika kuamsha ari ya wananchi kushiriki mipango ya maendeleo kwa ajili ya mabadiliko ya watu wenyewe.
“Tutambue dhamana tuliyonayo lakini pia umahiri wenu utumike kusaidia watu masikini, wananchi wa vijijini na makundi maalumu katika kuwaongoza kupata haki na fursa sawa” alisema Bibi Sihaba.
Akizungumza katika mkutano huo Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Nyasa Bw. Protas Sule amesema kuwa wataalamu wa maendeleo ya jamii wanajukumu la kuhimiza wananchi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kusaidiana na Serikali na jamii kutatua matatizo haya bila kusubiri Serikali kutekeleza kila kitu.
“Afisa Maendeleo ya Jamii akifanikiwa kubuni mradi utatoa majawabu ya kero za vikundi vya vijana na wanawake atakuwa amefanya kazi kubwa ya kuaminisha jamii kwa Serikali na kuamsha ari yao kufanya kazi za maendeleo” alisema Bw. Sule
Maafisa Maendeleo ya Jamii wanatakiwa kuonesha utumishi uliotukuka katika kuhamashisha na kuamsha ari ya wananchi kushiriki shughuli za maendeleo yao bila kutegemea Serikali kuwafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment