Kampuni za utengenezaji filamu za Mashauri Studios na Novitech kwa kushirikiana na Clouds Plus pamoja na Shirikisho la Filamu Tanzania imezindua rasmi mfumo wa kutengeneza, kutangaza, kuonyesha na kusambaza filamu za kitanzania ujulikanao kama Bongohoodz.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwanzilishi mwenza wa Bongohoodz ambaye pia ni mtayarishaji wa filamu na Mkurugenzi wa Mashauri Studios, Paul Mashauri, mfanyabiashara ambaye katika miaka ya hivi karibuni alimua kuwekeza katika filamu alisema Bongohoodz inakuja kuwasaidia waandaaji wa filamu nchini kutatua tatizo la wizi wa kazi za sanaa hasa DVDs kutokana na usambazaji wa sinema feki unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Baada ya kutoa sinema kazaa sokoni ikiwa ni pamoja na One Month Date mwaka 2014, Maisha ni Siasa na Bongo na Fleva mwaka 2015 tumegundua kuwa wizi wa kazi za sanaa ‘piracy’ ni mkubwa sana. Lakini kupitia Bongohoodz, watayarishaji wa sinema nchini hawatahitaji tena kusubiri mapato yao au uwekezaji wao urudi kwa kuuza DVDs,
"Kimsingi hata katika nchi zilizopiga hatua katika sinema unazungumzia Hollywood (Marekani), Bollywood (India), China Film Industry (China) na Nollywood (Nigeria), mapato makubwa yanatokana na uonyeshaji wa sinema katika majumba ya sinema au ‘theaters’ wao wanaita ‘Box Office’.
Kwa sababu wizi wa kazi za sanaa upo dunia nzima," alisema Mashauri na kuongeza.
"Lakini mapato ya kwanza wanayopata waandaaji wa sinema au ‘production houses’ yanatoka ‘Box office’ au katika nyumba za kuonyesha sinema. Ndio maana sisi tutasema, kwanini tusionyeshe sinema hizi nchi nzima katika matamasha makubwa ambapo watanzania watapata kuona sinema zinazoburudisha na kufundisha kwa bei nafuu kabisa huku wakifurahia vyakula mbalimbali, muziki, kisha filamu?”
Mashauri alisema kuwa wameanza jitihada za makusudi za kutangaza sinema hizi ikiwa ni pamoja na kuwatangaza wasanii na wazalishaji wa sinema,“Dunia nzima waigizaji wenye majina makubwa ndio wanaovutia walaji au wanunuzi wa filamu, hata kwetu imezoeleka hivyo. Lakini ili muigizaji awe mkubwa lazima kazi yake ionekana,
"Kwa msingi huo na kwa ushirikiano wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na wadau wetu Clouds Plus, tumeanzisha ‘reality show’ ijulikanayo kama ‘The Producers’ inayoruka Clouds Plus kupitia king’amuzi cha Azam Tv kila siku jumatatu hadi ijumaa saa moja mpaka saa moja na nusu usiku na marudio siku ya jumapili kuanzia saa nne asubuhi ambapo watanzania wataweza kuona namna sinema zinavyotengenezwa na wasanii wanavyofanya kazi zao," alisema Mashauri.
Mashauri alisema kupitia kipiendi hicho watu mbalimbali ambao wanandoto za kuwa waigizaji watajua nini wa natakiwa kufanya kwani wataona fursa ziliziopo katika tasnia ya uigizaji na changamoto zinazowapata waandaji na waigizaji.
"Tunategemea kufanya kazi na waandaaji kumi kwa mzunguko wa miezi sita sita na kila Producer atatakiwa kuzalisha sinema ndani ya miezi sita na mchakato wa sinema yake utaonyeshwa katika reality show, sinema yake itatangazwa na kupelekwa sokoni," alisema Mashauri.
Naye Meneja wa Clouds Plus, Ramadhani Bukini, alisema Clouds Plus imeungana na Bongohoodz katika kufanikisha ukuaji wa soko la filamu nchini kwa kutoa fursa kwa wazalishaji wa sinema kuonyesha kazi zao na kuzipeleka sokoni kupitia matamasha.
“Tumeungana na Bongohoodz tukiamini kuwa lazima kuwe na mbinu mbadala za kuuza sinema. Dunia imebadilika sana na huwezi kutegemea chanzo kimoja cha mapato. Mfano, katika dunia ya leo, aina ya kompyuta zinazoongoza kwa kuuza duniani ni za Apple.
Watumiaji wa ‘computer’ hizi hawahamasiki kutumia DVDs. Inamaana tunakoelekea hata wenye deki za kuangalia DVDs ni
wachache,
"Watu wako kwenye simu za mikononi, ndio maana Clouds Plus ikaamua kuungana na Bongohoodz kuja na vyanzo vipya vya mapato kwa tasnia ya filamu Tanzania ikiwa ni pamoja na matamasha makubwa ya kuonyesha filamu. Kama imewezekana katika muziki tunaamini kabisa inawezekana katika filamu," alisema Bukini.
Naye mwanzilishi mwenza wa Bongohoodz ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Novitech ambayo inashirikiana na Mashauri Studios katika kutayarisha sinema, Mary Mgurusi alisema watanzania wasubirie kwa hamu kazi nzuri za filamu.
“Tumeandaa sinema nzuri za kitanzania zenye maudhui tofauti tofauti ambazo tunaamini zinaburudisha na kufundisha. Tayari sinema ya Tatu Chafu imekamilika na tunatarajia kuizindua tarehe 16/12/2017 Mlimani City pamoja na Dar Live Mbagala. Baada ya uzinduzi huo, tunatarajia kuonyesha sinema hii nchi nzima katika mikoa mbalimbali. Zaidi ya Tatu Chafu zipo sinema nyingi katika maandalizi, mfano Tajiri kutoka India, What is Marriage, Rashid Snake Boy Matumla na School Bus," alisema Mgurusi.
No comments:
Post a Comment