ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 9, 2017

MHE MWANJELWA: UZALISHAJI WA MAZAO YA CHAKULA NA BIASHARA UMEONGEZEKA KWA KASI

Na Mathias Canal, Dodoma

Serikali imesema kuwa utekelezaji wa mpango wa Kilimo Kwanza umekuwa na mafanikio katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini ambapo uzalishaji wa jumla wa mazao ya biashara katika msimu wa mwaka 2016/2017 umeongezeka kufikia Tani 881,583 ukilinganisha na Tani 796,562 katika msimu wa mwaka 2015/2016.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa amebainisha hayo Leo Novemba 7, 2017 Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Mkoani Singida Mhe Yahaya Omary Masare aliyetaka kufahamu Kuna mafanikio kiasi gani kwa mazao ya biashara na chakula kwani Katika mpango wa kilimo Kwanza serikali ilihamasisha watanzania kuongeza uzalishaji katika kilimo ili serikali itoe mikopo ya matrekta.

Mhe Mwanjelwa alisema kuwa mafanikio ya mpango huo ni makubwa kwani Katika Wilaya ya Manyoni uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kufikia Tani 42,554 katika msimu wa mwaka 2015/2016 ambapo uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka Tani 1342 mwaka 2011/2012 hadi kufikia Tani 6212 mwaka 2015/2016.

Alisema kwa upande wa Zao la Alizeti uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 4464 mwaka 2010/2011 hadi kufikia Tani 21,871 mwaka 2016/2017 wakati huo huo zao la Ufuta uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 2285 mwaka 2010/2011 hadi kufikia Tani 8874 katika msimu wa mwaka 2015/2016.

Aliongeza kuwa katika Mkoa wa Singida uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka Tani 453,297 mwaka 2013/2014 hadi Tani 481,452 mwaka 2015/2016.

Uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka Tani 184,066 mwaka 2012/2013 hadi kufikia Tani 293,873 katika msimu wa mwaka 2015/2016.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe Mary Mwanjelwa alisema kuwa Jumla ya Matreka yanayofanya kazi nchini ni 18,774 ambapo kati yake Matrekta makubwa ni 11,500 na matrekta madogo ya mkono ni 7274.

Alisema kuwa Wilaya ya Manyoni pekee ina jumla ya matrekta makubwa 32 Matrekta madogo ya Mkono 39 na wanyamakazi 14784 yanayotumika katika kuongeza ufanisi wa kilimo ambapo pia kilimo cha kutumia Maksai ni maarufu katika Wilaya hiyo.

Alisema kuwa pamoja na jitihada za serikali kuu katika kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za Kilimo Halmashauri za Wilaya kote nchini zimelekezwa kuhamasisha wakulima kujiunga au kuanzisha vyama vya akiba na Mikopo (SACCOS) ambavyo vitakopesha wanachama wake au kuwadhamini kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za fedha kwa ajili ya kununua Zana hizo bora za Kilimo ikiwemo Matrekta.

Akijibu swali la Nyongeza la Mbunge Masare aliyetaka kufahamu namna ya kupatiwa mikopo kwa wananchi ambao hawajajiunga na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa alisema kuwa sifa ya wananchi kukopeshwa ni pamoja na kujiunga na Vyama Vya Ushirika lakini pia Wizara ya Kilimo kupitia Mfuko wake wa Taifa wa pembejeo za kilimo ataruhusiwa mkulima mmoja mmoja kukopa jinsi atakavyo kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

MWISHO

No comments: