ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 9, 2017

PROFESA TIBAIJUKA ATANGAZA KUNG’ATUKA UBUNGE 2020

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka, ametangaza kung’atuka nafasi ya ubunge kwa kutogombea tena kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Prof. Tibaijuka alitangaza msimamo huo jana mkoani Kagera, wakati wakizungumzia miaka miwili ya serikali ya Rais John Magufuli ambaye hivi sasa yuko mkoani humo kwa ziara za kikazi.

Jumatatu ya wiki iliyopita, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitangaza kujiuzulu ubunge na pia kujivua uanachama wa CCM kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.

Baadaye Nyalandu alionekana akikaribishwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kisheria, kuhama chama humpotezea mbunge sifa ya kuendelea kuwa mwakilishi wa jimbo lake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huandaa uchaguzi mwingine mdogo kwa ajili ya kumpata mbunge mwingine kwenye jimbo husika.

Wakati akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kutogombea tena ubunge mwaka 2020, Tibaijuka aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, aliiambia Televisheni ya Taifa (TBC), kuwa ameamua kujing’atua ili kutoa nafasi kwa vijana.

“Sisi ni watu wazima… kizazi chetu tumeshamaliza kazi. Tumeshastaafu na mimi nikimaliza ubunge muhula huu nastaafu, nakwenda Muleba,” alisema Tibaijuka na kuongeza:

“Na kuaga nimeshaaga na wananchi wameniamini. Napenda tuwape nafasi vijana. Kuzeeka haimaanishi kwamba maarifa yangu yaondoke kwa sababu nimestaafu, tunawapa nafasi vijana washike nchi.

“Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema tung’atuke… na mimi nang’atuka ili maarifa yetu yaweze kutumika kushauri, jamani tufanye hivi ili tuende mbele.”

Akizungumzia utendaji wa serikali ya Rais Magufuli katika kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, Tibaijuka alisema amefanya mengi mazuri na lazima Watanzania waendelee kumuamini.

“Hii nchi ilikuwa inasubiri kiongozi si Rais. Rais lazima awe pia kiongozi… sasa tujifunze kujua tofauti, mtu anaweza kukalia nafasi, lakini anaongoza? Anaonyesha njia? Ni jasiri? Kwa maana ujasiri unatokana na ukweli,” alisema.

Tibaijuka aliondolewa katika nafasi ya uwaziri kwenye serikali ya awamu ya nne ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete wakati baadhi ya wabunge walipomhusisha na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT).

No comments: