Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na madereva wa Bodaboda na Bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga katika uwanja wa Nelson Mandela.
Baadhi ya Bajaji zikiwa zimepaki katika uwanja ulipofanyikia Mkutano wa madereva wa Bajaji na Bodaboda na Mkuu wa Mkoa.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa ACP George Kyando akitoa elimu ya usalama barabarani na kujibu baadhi ya kero zilizotolewa na madereva wa Bodaboda na bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya bodaboda zikiwa zimepaki uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa George Kyando kuwaweka pembeni Mkuu wa Usalama barabarani wa Wilaya Inspector Suleiman Africanus pamoja na Msaidizi wa Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa Inspector Michael Mwakasungula ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yao.
Agizo hilo amelitoa wakati akijibu kero za madereva wa bajaji na bodaboda wapatao 4352 kwa mkoa mzima waliowakilishwa na wenzao wa mjini Sumbawanga baada ya kukutana nao na kusikiliza vilio vyao katika Mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Madereva 13 walipata nafasi ya kumuelezea Mh. Wangabo kero wanazopata wakiwa barabarani huku miongoni mwa kero hizo ambazo ni pamoja na kupokea rushwa, uonevu usio wa lazima barabarani na kuwaweka mahabusu kwa visingizio mbalimbali zilielekezwa kwa maafisa hao wa usalama barabarani.
“Hawa wawili hawa na tuhuma mlizozitoa huenda zina ukweli, RPC nakuagiza nenda kazichunguze hizi tuhuma zote zilizotolewa hapa kwa kina na nyinyi muwe mashahidi kwenda polisi kutoa shuhuda zenu, halafu uchukue hatua stahiki, lakini wakati huo huo unapozichunguza hizi tuhuma wao uwaweke pembeni, uwape kazi nyingine,”
Amesema kuwa hakuna mtendaji wa serikali ambaye amepangiwa sehemu akae milele na milele na kuwa mtumishi asijidanyanye kwamba bila ya yeye kazi za serikali haziwezi kwenda huku akijitolea mfano kuwa yeye ni Mkuu wa Mkoa wa 15 tangu kuanzishwa kwa Mkoa huu mwaka 1974, wote walionitangulia wamepiga kazi wameondoka nae ataondoka.
Aidha, Mh. Wangabo amewasisitiza madereva hao kusomea sheria za barabarani na kupata leseni ilikupunguza ajali za barabarani katika Mkoa wa Rukwa huku akiwapongeza kwa takwimu zinzoonyesha kupungua kwa ajali hizi ukilinganisha na mwaka 2016.
Katika kulisisitiza hilo Mh. Wangabo alimualika mwalimu wa mafunzo ya usalama barabarani ili kutoa mafunzo hayo ya siku 3 bure kwa madereva hao kwa lengo la kutokuwa na ajali katika Mkoa wa Rukwa.huku akimpa miezi 7 kamanda wa polisi mkoa kuhakikisha bodaboda wote 4352 wanakuwa na leseni na vitambulisho.
Kwa upande wake kamanda wa polisi Mkoa ACP George Kyando ameeleza kuwa kwa ajali za bajaji na bodaboda mwaka 2016 kulikuwa na ajali 18 huku 11 zikisababisha vifo vya watu 20 wakati mwaka 2017 kuemtokea ajali 9 huku 5 zikisababisha vifo vya watu 7.
Yona Mwangoka ni mmoja wa madereva wa bodaboda aliyedai kuwa na ushahidi wa video unaoonyesha ukusanyaji wa shilingi 40,000 kuwapa polisi ili kuachiwa kwa makosa mbalimbali huku risiti zao zikionesha shilingi 30,000, fedha ambazo zilikusanywa na kiongozi wa boda boda baada ya boda boda hao kukamatwa kwa kosa la kumpiga askari wa usalama barabarani tukio lililotokea siku mbili kabla ya Mkutano huo.
No comments:
Post a Comment