Naibu Mkurugenzi Rasilimali Watu wa Mamlaka hiyo, Bw. Ulimbakisya
Masomelu akiwaeleza Waajiriwa wapya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) juu ya kuwa waadilifu na kutekeleza majukumu yao kikamilifu
wakati wa Semina Elekezi ya Siku Kumi iliyoanza leo 08 Novemba, 2017
katika Chuo cha Kodi (ITA) Kilichopo Jijini Dar es Salaam.
Waajiriwa wapya 400 walioajiriwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wakipokea elimu ya Semina Elekezi toka kwa Maafisa Utumishi wa TRA
kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao kwa weledi wakati wa
ufunguzi wa Semina hiyo ya Siku Kumi iliyoanza leo katika Chuo cha Kodi
(ITA) kilichopo Jijini Dar es Salaam, 08 Novemba, 2017.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA,TRA).
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kutoa Semina elekezi ya siku
10 kwa Waajiriwa wapya 400 waliopata fursa ya kupata ajira katika
Mamlaka hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao wakati
wanapoenda kuanza majukumu ya kukusanya mapato kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo
cha Kodi cha TRA (ITA), Profesa Isaya Jairo na yanatarajiwa kukamilika
baada ya siku kumi na kuwawezesha waajiriwa hao kumudu majukumu ya
kukusanya mapato nchini kwa uadilifu.
Akiongea wakati wa Semina hiyo, Naibu Mkurugenzi Rasilimali Watu wa
Mamlaka hiyo, Bw. Ulimbakisya Masomelu alisema kwamba, lengo la
kubwa la kuwapatia mafunzo waajiriwa hao ni kuhakikisha kwamba TRA
inakuwa na nguvu kazi kubwa ya rasilimali watu katika kutekeleza
majukumu yake.
Bwana Masomelu ameeleza kwamba, TRA ina majukumu makubwa ya
kukusanya mapato nchi nzima na huo ni utaratibu wake wa kuwapatia
mafunzo waajiriwa wake kwani mafunzo hayo yanawawezesha waajiriwa
hao kuijua mamlaka hiyo jinsi inavyofanya kazi, ikiwemo mgawanyo wa
majukumu (Organization Structure) pamoja na maadili ya utumishi.
“Lengo la kuwapatia semina hii elekezi waajiriwa wetu wapya ni
kuwawezesha waweze kutambua dhima kubwa ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania ambayo ni kukusanya mapato, waweze kutambua pia maadili ya
utumishi ili wanapoenda kutekeleza majukumu yao waweze kutekeleza
kulingana na maadili ya kiutumishi, lakini pia waweze kujua mgawanyo
wa majukumu ya TRA katika vitengo vyao”, alisema, Masomelu.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mafunzo wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania, Bi. Pendo Mandia amesema kwamba, waajiriwa hao katika
muda wao wote wa mafunzo ya siku kumi watapitishwa katika maeneo
mbalimbali ili waweze kuyajua vizuri majukumu yao, ambapo baadhi ya
mambo watayofanya ni pamoja na kufahamishwa juu ya muundo wa
vitengo vyao, Sheria za Mamlaka ya Mapato, kufahamu Mkataba wa
Huduma kwa Mlipakodi, kufahamu maadili na mwenendo wa utumishi wa
umma.
Ameongeza kuwa, pamoja na hayo yote, waajiriwa hao wapya mara
baada ya kukamilisha taratibu zote za ajira katika mamlaka hiyo watakula
kiapo cha uadilifu kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wao baadhi ya waajiriwa hao wapya wameonyesha nyuso za
furaha ya kupata ajira TRA na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa
pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi.
No comments:
Post a Comment