ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 30, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AFANYA ZIARA KATIKA HIFADHI YA SAADANI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Vitalis Kuluka huku akishirikiana kuonesha eneo hilo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo,Erica Yigella ( wa pili kulia) mahali kilipo Kitongoji cha Uvinje ambapo wakazi wa eneo hilo wamegoma kuhama ndani ya hifadhi hiyo na wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana. Wa kwanza kulia ni Afisa Wanyamapori, Godfrey Maro na Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Stephano Msumi na pande wa kulia nyuma ya Katibu Tawala ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( wa pili kulia ) akizungumza na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi ( katikati) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili . Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Erica Yigella, Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Vitalis Kuluka, wa tatu kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza jana na Wananchi wa Kitongoji cha Uvinje ambao wamegoma kuhama ndani ya hifadhi hiyo, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kwa ajili ya kuzungumza nao ili kujua ukubwa tatizo la mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa .
Bango lililopo katika geti la Gama linalokuelekeza sheria na taratibu ukiwa unaingia katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( kushoto ) akipatiwa maelezo na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi ( katikati) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili .Wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa, Vitalis Kuluka, nyuma ya Mhifadhi wa Saadani ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( mbele ) akiwa na baadhi ya viongozi wa Hifadhi za Taifa pamoja kamati ya ulinzi na usalama kutoka Wilayani Bagamoyo akiongoza kwenda kuangalia sehemu kunakofanyika utalii wa boti katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili .
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kulia) akipatiwa maelezo na Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu ( wali kushoto) kuhusiana na sehemu kunakofanyika utalii wa boti katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani . Wengine ni baadhi ya viongozi wa Hifadhi za Taifa pamoja na kamati ya ulinzi kutoka Wilayani Bagamoyo .  Picha na Lusungu Helela

Wananchi wa Kitongoji cha Uvinje kilichomo ndani Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoani wa Pwani wamesema hawapo tayari kuhama wala kulipwa fidia ili kupisha hifadhi hiyo.

Kitongoji hicho, ambacho ni kati ya vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005 baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.


Akizungumza mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakati alipofanya ziara jana katika kijiji hicho aliwambia wananchi hao kuwa lengo la ziara yake ni kutaka kuwasikiliza juu mgogoro huo na sio kuwahamisha.

‘Mimi ni mgeni kidogo kwenye Wizara hii, Nimekuja kuangalia sio kuwahamisha kwa kuwa sijui eneo hili lina ukubwa kiasi na lina kaya ngapi lakini nimekuja kutembelea hifadhi na maeneo yote yenye changamoto. ‘’ alisema.Alisema amefika kwa ajili ya kuwasikiliza ili aweze kujua jinsi mgogoro ulivyo kwa sababu hakutaka kusikia upande mmoja wa TANAPA pekee.

Naye , Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hassan Akida alisema wakazi wa eneo hilo hawapo tayari kuhama na wala kulipwa fidia kwa vile ni ardhi yao tokea enzi za mababu zao.’‘Tumesema hapa ndo kwetu mnataka kutuhamisha mtupeleke wapi wakati sisi tumezoea maisha yetu hapa’’ alisema Akida.

Aliongeza kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila shida hadi pale pori hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa.“Wakati hili ni pori la akiba tuliishi vizuri tu na wazazi wetu walikuwa ni wafanyakazi wa pori. Lakini tangu iwe hifadhi imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati tumezaliwa hapa na wazazi wetu wamezikwa hapa hapa,” anasema Hassan Akida.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Saadani, Adam Mwandosi alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na umekuwa ukileta chuki kati ya Serikali na wananchi.



Amesema wananchi wa eneo hilo muda mwingine wamekuwa wakimuona hata yeye Mwenyekiti wao kama anawasaliti kwa vile tokea mgogoro huo ulipoanza viongozi wengi wamekuwa wakifika hapo lakini wamekuwa hawana majibu ya kumaliza mgogoro huo.


Mhifadhi Mkuu wa Saadani, Stepahano Msumi amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.

“Kwa ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote la kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.

Anasema katika makubaliano, iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu lakini hata hivyo licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea mbali ya wachache kujitokeza.

Ikumbukwe kuwa, Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa nchini na Afrika Mashariki yenye fukwe za bahari na inayotazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake zinakutana na uoto wa asili wa nchi kavu.

Inapatikana katika mikoa ya Tanga na Pwani. Uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba la Saadani, ranchi ya Mkwaja na sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa asili wa Zaraninge.

No comments: