ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 2, 2018

WATUMISHI WA SERIKALI ZA MITAA, ASKARI WA MBELE VITANI - WAZIRI JAFO

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Arusha Dc wakati wa ziara yake katika Halmashauri hiyo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(kushoto) pamoja na kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Iddi Kimanta kwenye kikao na watumishi wa Halmashauri ya Arusha Dc.
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha Dc Dr.Wilson Mahera Charles akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi Mhe.Selemani Jafo(hayupo pichani) na watumishi wa Halmashauri hiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Arusha Dc wakifuatilia Kikao wakati Waziri wa Nchi Mhe.Selemani Jafo alipowatembelea na kufanya kikao na watumishi  wa Halmashauri hiyo.

Nteghenjwa Hosseah, Arusha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo  amesema watumishi wa Mamlaka hii ndio askari wa mbele katika harakati za maendeleo na kuleta mabadiliko kwa wananchi wa Nchi hii.

Waziri Jafo amesema shida zote za wananchi zitapata ufumbuzi wa kina endapo watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wataacha kufanya kazi kwa mazoea na kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Arusha Dc kwenye ziara yake ya Siku moja katika Halmashauri hiyo na kuzungumza na watumishi, kukutana na wananchi na kuskiliza kero zao sambamba na kukagua miradi ya maendeleo.

Amesema "Ili kufikia agenda ya mabadiliko katika Nchi hii lazima sisi tunaohudumu katika Ofisi hii tuongee lugha moja, tujitume, tuwajibe kwa moyo katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu.

Aliongeza kuwa Upimaji wa utendaji kazi wetu usiwe ule wa kujaza Opras kama mazoea  ila uwe ni Mkataba wa Makubaliano ya kazi na mpimane kulingana na yale mliokubaliana kwa mujibu wa Mkataba.

Aliupongeza Mkoa huu kwa kuanzisha mpango wa kupima wanafunzi wa Sekondari na kushauri kuboresha mpango huo kwa kuanzisha Kampeni ya Kuondoa Zero katika Mkoa wa Arusha.

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akimkaribiha Waziri wa Nchi amesema watumishi waliopo katika Halmashauri ndio Timu ya Ushindi ya Mkoa wa Arusha hivyo wakurugenzi wote wanatakiwa kuwasimamia na kuwaongoza kwa Weledi ili waweze kufikia malengo.

Pia alikumbushia maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao wanaanza masomo wiki ijayo na kuwaelekeza wakurugenzi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaaza masomo kwa wakati huku miundombinu ikiwa imekamilika na walimu kujiandaa kwa mapokezi  hayo.

Akielezea mpango wa Mkoa wa Arusha wa kusimamia  ubora wa Elimu kwa wanafunzi wa Sekondari kwa kuanzisha Mtihani  Maalumu wa kupima uwezo wa mwanafunzi katika kila kidato amesema ili kuweka uelewa wa pamoja katika shule zote za Sekondari Mkoa umeamua kusimamia mpango huu  na maandalizi ya uratibu wa mtihani huo yameshakamilika na yako chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Iddi Kimanta  amesema wamefurahi kuwa watumishi wa kwanza kwa mwaka huu kutembelewa na Waziri wa Nchi Sambamba na viongozi wa juu wa Mkoa na bika shaka ari waliyoipata leo itaendelea kujidhihirisha katika maeneo yao ya Utendaji katika kipindi cha mwaka Mzima.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe.Selemani Jafo ameanza ziara ya kwanza ya kikazi kwa mwaka 2018 na ataendelea na ziara hii katika Mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es salaam, Iringa, Mbeya, Mtwara na Lindi.

No comments: