Tuesday, February 6, 2018

MAHAKAMA YAAGIZA NABII TITTO APIME UPYA AKILI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Dodoma imeagiza mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma Tito Machibya, maarufu kama ‘Nabii Tito’ (45) kupimwa akili upya katika Taasisi ya Afya ya Akili ya Mirembe Isanga mkoani Dodoma ili kuriridhisha kama ana matatizo ya akili.


Licha ya kuagizwa mtuhumiwa huyo kufanyiwa vipimo upya, mahakama pia imetaka kuwasilishwa kwa vielelezo kama kweli ana tatizo hilo kama alivyoieleza mahakama.



Nabii Tito anashtakiwa kwa kosa la kujaribu kujiua kwa kutumia wembe.



Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, alisema jana kuwa kutokana na mshtakiwa kuieleza mahakama kuwa ana matatizo ya akili na alifanya tukio hilo kutokana na kusikia vitu ambavyo vilikuwa vinamwamuru akate, mahakama itabidi  ipate vielelezo ambavyo vitathibitisha anachokisema.



Karayemaha alisema kutokana na kifungu namba 219 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, kama mshtakiwa atabainika kweli ana matatizo ya afya ya akili, mahakama itaamua kuwa alivyofanya tukio hilo hakuwa na akili timamu, hivyo hana hatia.



“Mshitakiwa anadai kuwa ana matatizo ya akili na amekuwa akitibiwa katika hospitali mbalimbli ikiwemo ya Maweni.  Mahakama hii inaagiza vielelezo vyake vyote viletwe hapa lakini pia apelekwe kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya ya akili Mirembe Isanga,” alisema Karayemaha.

           
NABII TITO ALIVYOKAMATWA NA JESHI LA POLISI MKOANI DODOMA
Pia alisema kama mshtakiwa atabainika kuwa hana tatizo lolote la afya ya akili kwa mujibu wa vielelezo vyake pamoja na vipimo atakavyofanyiwa, atakuwa na kesi ya kujibu.


“Kutokana na hili aliloiambia mahakama kuwa ana matatizo ya akili hata suala la dhamana tunaliweka pembeni kwanza kwa sababu hawezi kujieleza lakini kama itabainika kuwa hana matatizo ya akili kutokana na vielelezo vitakavyoletwa pamoja na vipimo vitakavyofanyika, suala la dhamana litafanyiwa kazi,”alisema.



Hata hivyo alisema mshtakiwa huyo anarudi rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa  Februari 19,  mwaka huu.



Wakati kesi itakapotajwa vielelezo vyote pamoja na vipimo vinatakiwa kuwa tayari vimeshawasilishwa mbele ya mahakama hiyo.



Nabii Tito anashtakiwa kwa tuhuma za kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu, katika mtaa huo wa Ng’ong’ona alipokuwa akikaguliwa na polisi.



CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake