ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 16, 2018

MPINA AMUAGIZA KATIBU MKUU UVUVI, KUHARAKISHA MCHAKATO WA KUTAIFISHA MELI YA KAMPUNI YA BUAH NAGA ONE.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga (mwenye kofia) akinyanyua samaki aina ya Jodari mara baada ya kukagua Meli ya Uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China iliyotia nanga katika bandari ya Dar eS Salaam kwa ajili ya ukaguzi. Meli hii ilipewa leseni ya kuvua samaki aina ya Jodari na inavua kwa kutumia mishipi. (Picha na John Mapepele).
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga (mwenye kofia) akipima samaki aina ya Jodari mara baada ya kukagua Meli ya Uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China iliyotia nanga katika bandari ya Dar eS Salaam kwa ajili ya ukaguzi. Meli hii ilipewa leseni ya kuvua samaki aina ya Jodari na inavua kwa kutumia mishipi. (Picha na John Mapepele)
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga (mwenye Kofia) na Katibu Mkuu wa Uvuvi Dkt. Yohana Budeba wakikagua Meli ya Uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China iliyotia nanga katika bandari ya Dar eS Salaam kwa ajili ya ukaguzi. Meli hii ilipewa leseni ya kuvua samaki aina ya Jodari na inavua kwa kutumia mishipi (Picha na John Mapepele)


Na John Mapepele
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi, Dk. Yohana Budeba kuharakisha mchakato wa kuomba kibali cha Mahakama ili kutaifisha meli ya Kampuni ya Buah Naga One ya nchini Malaysia baada ya mmiliki wa meli hiyo kukaidi amri halali ya Serikali iliyomtaka kulipa faini ya Dola za Kimarekani 350,000 sawa na sh milioni 770 ndani ya siku saba baada ya kubainika kukiuka Kanuni ya 66 ya Kanuni za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007.

Mpina amesema, Januari 25 mwaka huu meli hiyo ilikutwa na makosa mawili ambayo ni kukutwa na mapezi na mikia ya samaki aina ya papa 30 bila kuwepo miili yake na Kapteni wa meli hiyo Han Ming Chuan raia wa Malaysia kukutwa na bastola aina ya Bereta na risasi kumi ambayo alikuwa anaimiliki kinyume cha sheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kukagua Meli ya Uvuvi ya Kampuni ya XISHIJI 37 ya nchini China kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya ukaguzi ambapo aliipongeza kwa kufuata taratibu za kimataifa za ukaguzi, Waziri Mpina aliagiza vyombo vya dola kuisaka na kuichukulia hatua kali za kisheria meli ya Kampuni ya Tai Hong No. 1 ambayo pia ilikaguliwa na kukutwa na mikia ya papa 44 bila kuwa na miili yake kinyume cha sheria za uvuvi.

Waziri Mpina alisema meli hiyo ilitoweka katika mazingira ya kutatanisha na kuagiza vyombo vya dola kufuatilia ili ikamatwe na hatimaye ifikishwe katika vyombo vya sheria.

“Tutahakikisha meli hii tunaikamata ili sheria ichukue mkondo wake kwa kuwa bahari ya Tanzania siyo shamba la bibi” alisisitiza Mpina

Katika hatua nyingine Waziri Mpina amevitaka vyombo vya dola kuzisaka hadi kuzipata meli nyingine 16 zilizopewa leseni ya kuvua katika bahari ya Tanzania ambazo zilitoroshwa na wenye meli kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu mara baada ya kuanza kwa operesheni Jodari aliyoiunda hivi karibuni iliyojumuisha vyombo mbalimbali vya Serikali kudhibiti uvuvi haramu.

Waziri Mpina alisema doria hiyo pia inalenga kudhibiti utoroshaji wa samaki na mazao yake, kudhibiti biashara haramu ya madawa ya kulevya, biashara ya binadamu, usafirishaji wa silaha na magendo, utupaji wa taka hatarishi kutoka katika meli na uhalifu wowote unaoweza kujitokeza katika maji ya nchi yetu.

Aidha Mpina alisema jumla ya meli 24 zilipewa leseni ya uvuvi wa bahari kuu ambapo hadi sasa ni meli 8 tu ndizo zilizokaguliwa huku 16 zikitoroshwa.

Waziri Mpina aliyataja baadhi ya maeneo manne ambayo Serikali imeyafanyia maboresho katika marekebisho ya Kanuni za uvuvi za mwaka 2009 na kuweka vifungu vipya ambavyo vitasaidia Serikali kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi kuwa ni pamoja na;

Kufanya ukaguzi wa meli zote zinazokuja kuvua nchini kabla ya kuanza kuvua na baada ya kumaliza kuvua ili kubaini idadi halisi ya kiasi cha raslimali za uvuvi inayovunwa na kutozwa kodi halisi ili kuinua pato la taifa.

Kupakia asilimia 10 ya mabaharia wazawa katika kila meli inayokuja kuvua katika maji ya Tanzania ili kuwajengea uwezo na na kuwapatia ajira.

Kushusha samaki waliovuliwa bila kutarajiwa na kukabidhi katika kwa Serikali kwa vile ni mali ya serikali ili wauziwe wananchi kwa taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kupigwa mnada.

Pia kutoza mrabaha wa dola za kimarekani 0.4 kwa kila kilo ya samaki walengwa(targeted species) kuongeza pato la nchi.

Wakala wa meli ya XISHIJI 37 nchini Abdulkarim Karia Maina kutoka kampuni ya Scaforth Gereral Agencies ya jijini Dar es Salaam amesifu juhudi zinazofanywa na Waziri Mpina katika kudhibiti meli zilizokuwa zinalihujumu taifa kwa kutofuata taratibu na kusema kuwa zinapashwa kuigwa na watumishi wote katika Wizara yake.

“Mageuzi yanaofanywa na Mheshimiwa Mpina katika kudhibiti uvuvi haramu nchini yataleta mapinduzi makubwa katika sekta katika siku za hivi karibuni na kuliingizia taifa mapato makubwa” alisisitiza Maina

Naye Katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba alisifu miongozo inayotolewa na Waziri Mpina kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kuahidi kusimamia kikamilifu maelekezo yote ili sekta iweze kuchangia inavyositahili kwenye uchumi wa nchi yetu.

Kwa upande wake, Bw. Wankyo Simon ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Dawati linalohusiana na Makosa ya Mazingira, amesisitiza kuwa Tanzania imejizatiti kuhakikisha kwamba Sheria zinachukua mkondo wake ili kudhibiti uhalifu wowote unaotokea katika bahari ya Tanzania.

No comments: