Serikali ya Tanzania na Ufaransa zimezindua mkakati wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa ambao lengo lake ni kuimarisha utafiti lakini pia kuangalia namna vyuo hivyo vinaweza kushirikiana. Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mkakati huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha alisema ushirikiano huo ni muhimu kwa vyuo vya Tanzania kwani vitakuwa vikipata fedha ambazo zitawasaidia kufanya tafiti. Alisema ni vyema wanafunzi Watanzania wakatumia vyema ushirikiano huo ili kujifunza Kifaransa, lakini pia wanaweza kupata nafasi ya kwenda kusoma Ufaransa kwani kwa sasa changamoto kubwa ni wengi wao kutokujua kuzungumza Kifaransa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza kuhusu mkakati wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa. (Picha zote na Rabi Hume, MO Dewji Blog)
"Sisi kama Tanzania tunaona ni ushirikiano mzuri sana ambao utavisaidia vyuo vyetu kupata fedha kwa ajili ya tafiti, lakini unafungua ukurasa mpya kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka Tanzania kwenda kusoma kwenye vyuo vya Ufaransa, Ufaransa ni moja ya nchi duniani zenye mfumo mzuri sana wa elimu. "Kwa bahati mbaya sana (Watanzania) hawajanufaika na elimu ya Ufaransa kwa sababu pamoja na mambo mengine tatizo ni lugha, kwamba kile kinachotumika kule ni Kifaransa. Lakini pia ushirikiano huu utaumika kuimarisha mazingira ili wanafunzi wetu waweze kusoma Kifaransa lakini iwe ni rahisi kwao kuingia kwenye vyuo vya Ufaransa," alisema Ole Nasha.
Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier akizungumza kuhusu mkakati wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa.
Nae Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier alisema ushirikiano huo utaboresha uhusiano uliopo sasa kati ya mataifa hayo mawili na muhimu zaidi ni kutoa elimu ambayo itawasaidia wanafunzi Watanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati. Alisema Ufaransa imekuwa ikipokea wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali duniani ambao wanakwenda kusoma katika vyuo vikuu vya nchi hiyo na hivyo kuwataka Watanzania kutumia vyema ushirikiano huo ili waweze kusoma katika vyuo vya nchi hiyo na kupata fursa ya kufanya kazi katika mataifa zaidi ya 80 ambayo yanazungumza Kifaransa. "Ndoto imetia ya kuwepo kwa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika elimu ya juu, kwa serikali yetu ni jambo muhimu sababu nchi zetu zinataka vijana kupata ujuzi ili kwenda mbele zaidi," alisema Clavier na kuongeza. "Ushirikiano huu utawezesha wanafunzi wa Tanzania kufahamu fursa zilizopo Ufaransa na kujua namna wanaweza kuzitumia, kwa sisi tayari tunao Wafaransa ambao wanajifunza Kiswahili katika vyuo mbalimbali hapa nchini." Na Rabi Hume, MO Dewji Blog
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier wakizindua mkakati wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier wakipongezana baada ya kuzindua mkakati wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa.
Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mkakati wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa.
No comments:
Post a Comment