ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 20, 2018

Dkt. Kalemani aiagiza TANESCO kuondoa mita za umeme za zamani kabla ya mwezi Julai

 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa Tatu kushoto) akitia saini katika kitabu cha wageni mara alipowasili katika Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe  kwa lengo la kukagua mradi wa usambazaji umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III). Katikati ni Mkuu wa wilaya hiyo, Joseph Mkude, wa pili kushoto ni  Mbunge wa Ileje, Janet Mbene na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Haji Mnasi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Mapogoro wilayani Ileje wakati alipofika kijijini hapo kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini pamoja na kuzindua huduma ya upatikanaji wa umeme katika Kijiji hicho.



Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo kuhakikisha kuwa, mwisho wa kutumia mita za zamani, ambazo wateja hufanya malipo baada ya kutumia umeme (Conventional Meters), ni mwezi Juni mwaka huu.

Dkt.Kalemani aliyasema hayo wilayani Ileje mkoani Songwe wakati akizungumza na Mkuu wa wilaya hiyo, Joseph Mkude, Mbunge wa Ileje, Janet Mbene,  Watendaji wa TANESCO Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Wizara ya Nishati, na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kabla ya kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu katika Wilaya husika.

Alisema kuwa, jumla ya wateja Laki Tatu (300,000), katika nchi nzima hutumia mita hizo za zamani huku wateja 48,000 wakiwa wanatumia conventional meters ambazo muda wake umeisha.

" Kuendelea kutumia mita hizi ni kupoteza mapato ya Shirika, kwa mfano hawa wateja 48,000 wanatumia umeme bila sisi kujua wametumia kiasi gani, hivyo nawaagiza kuwa, mwisho wa kutumia mita hizi ni mwezi Juni na wateja wote wafungiwe mita mpya za umeme ili Serikali ikusanye mapato yake ipasavyo," alisema Dkt Kalemani.

Aidha, Dkt. Kalemani aliwaagiza Mameneja wa TANESCO nchini kuhakikisha kuwa kazi ya kufanya marekebisho mbalimbali katika miundombinu ya umeme ikiwemo uondoaji wa nguzo zilizochakaa  iwe imekamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu kwani fedha za kufanya kazi husika zilishatolewa.

Akizungumzia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III), Dkt. Kalemani alisema kuwa, mradi huo unaolenga kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini, utakamilika mwezi Juni mwaka 2021 ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wawe wameunganishwa na huduma ya umeme kufikia mwaka huo.

Waziri wa Nishati, pia aliwaagiza watendaji wa TANESCO, REA na Wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kuhakikisha kuwa vijiji vyote ambavyo vilipitiwa na miundombinu ya umeme lakini havina umeme, visambaziwe nishati hiyo kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaokamilika mwezi Juni, 2019.

Vilevile, alitoa wito kwa Halmashauri zote pamoja na Serikali za Vijiji nchini, kutenga fedha zitakazosaidia Taasisi za Serikali katika maeneo yao kama vile Shule na  Vituo vya Afya kuunganishwa na huduma ya umeme ili kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.

kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude, alisema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika wilaya hiyo inaridhisha kwani wanapata umeme kutoka gridi ya Taifa  na kwamba vijiji 31 kati ya 71 tayari vimeungwanisha nishati hiyo.


Aliongeza kuwa, katika mradi wa REA III mzunguko wa kwanza, vijiji 28 katika wilaya hiyo vitasambaziwa umeme ambapo shilingi Bilioni 34.6 zitatumika kwa kazi husika.

No comments: