ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 22, 2018

SHIDA YA UMEME KUSINI IMEKWISHA - MAJALIWA

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kufua Umeme kwa Gesi Asilia Mtwara, Mei 21, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kufua Umeme kwa Gesi Asilia Mtwara, Mei 21, 2018.  Watatu kulia ni  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na watatu kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditie , wanne kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Gelasius  Byakanwa na kulia ni Mbunge wa Mtwara Mjiji, Maftah. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia baada ya kuzindua Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kufua Umeme kwa Gesi Asilia Mtwara, Mei 21, 2018.  Watatu kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atshasta  Nditie, wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa na kulia ni Mbunge  wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo litakalotumika kupakuwa mafuta kutoka kwenye meli hadi kwenye matangi ya kuhifadhi mafuta katika bandari ya Mtwara, Mei 21, 2018. Wapili kulia ni  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Tanzania, Deusdediti Kakoko.
 Majenereta mawili ya kuzalisha umeme yaliyonunuliwa serikali na kufungwa kwenye eneo la TANESCO lenye mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi asilia katika Manispaa ya Mtwara ili kupanua uzalishaji umeme wa gesi asilia Mtwara .  Majenereta hayo yalizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mei 21, 2018 . 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema shida ya umeme iliyokuwa inaikabili mikoa ya Lindi na Mtwara hivi sasa imekwisha.

"Kuunganishwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye gridi ya Taifa, kumeondoa tatizo la umeme lililokuwa likiikabili mikoa hii, na mitambo ya jenerata iliyokuwepo, itabakia kuwa ya akiba endapo dharura yoyote itatokea," alisema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei 21, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Mtwara kwenye viwanja vya bandarini mjini humo.

Alisema pengo lililokuwepo la kukatikakatika kwa umeme, limezibwa kwa kupata umeme wa kutoka Somanga hadi Lindi. “Umeme huu umeanzia kituo chetu cha Mbagala, umekuja Mkuranga, Muhoro, Lindi na hatimaye umefika pale Mahumbika. Na mchana wakati nikiwa Mahumbika, niliwasha kwa kompyuta kuashiria umeme wa gridi kuingia mikoa yetu ya Lindi na Mtwara,” alisema.

Akiwa Mtwara mjini, Waziri Mkuu alikagua na kisha kuzindua mradi wa upanuzi wa kituo cha kufua umeme wa gesi asilia wenye uwezo wa kuzalisha megawati nne.

Kabla ya kuzindua mradi huo, alipita bandarini kukagua ukarabati wa mitambo ya kupokelea mafuta ya dizeli na petroli ambako alielezwa kuwa kampuni mbili za GM na OILCOM zimeanza ukarabati na kwamba mwezi ujao, bandari hiyo itaanza kupokea meli za kubeba mafuta.

“Bandari ya Mtwara hivi sasa itaanza kupokea meli kubwa za mafuta, jambo ambalo halijafanyika tangu mwaka 2014. Mwezi ujao, wakati wowote, wataanza kupakua mafuta. Kwa hiyo mji utaanza kuchangamka.”

“Kuanza kupakuliwa kwa mafuta katika bandari hii, kutasaidia kushusha bei ya mafuta kwenye mikoa hii na pia kiasi kitakachobakia, tutakipeleka nchi za jirani za Msumbiji na Malawi,” alisema.

Alisema matengenezo hayo yakikamilika yatafanya bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zote ziwe na uwezo wa kupokea mafuta. Pia aliitaka Mamlaka ya Bandari (TPA) iondoe urasimu na Mkurugenzi Mkuu wake awatumie vizuri watendaji waliopo chini yake.

Mapema, walipopewa nafasi ya kusalimia wananchi, wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) walitumia fursa hiyo kuelezea kufurahishwa kwao na hatua za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kusini, Bw. Selemani Said Bungara alisema aliamua kutoka Chama cha Mapinduzi kwa sababu aliamini kwamba mtu hawezi kusukuma gari akiwa ndani, ni lazima atoke.

“Tumetoka ndani ya gari ya gari na sasa tunalisukuma na linakwenda kwa kasi. Hebu angalia, ndani ya miaka miwili tu, mambo yanavyokwenda kwa kasi. Kama tungebakia ndani, gari lingeenda?” alihoji.

Hoja yake ilijibiwa na Mbunge wa Nanyamba, Bw. Abdallah Dadi Chikota ambaye alisema gari analolizungumzia mbunge huyo liko imara na wala halihitaji kusukumwa. “Gari letu halihitaji kusukumwa hata kidogo, liko imara, matairi yako imara, na dereva wetu yuko makini. Tena gari letu hata muda wake wa service haujafika,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi waliokuwa wakimsikiliza Waziri Mkuu.

Naye Bw. Zuberi Mohammed Kuchauka (Liwale) aliwataka wananchi wa mikoa ya Kusini wachangamkie fursa zinazopatikana kutokana na maendeleo yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano. “Kusini hivi sasa imeamka na imetoka gizani, sasa wananchi tuchangamkie fursa,” alisema.

Naye Mbunge wa Nachingwea, Bw. Hassan Elias Masala, alitumia fursa hiyo kuomba barabara ya kutoka Nachingwea iwekewe lami ili wakazi wake waweze kutumia fursa ya kusafirisha korosho zao hadi kwenye bandari ya Mtwara.

Naye Bw. Maftaha Abdallah Nachuma (Mtwara Mjini) pia aliomba barabara ya kutoka Mtwara hadi Mingoyo ikamilishwe matengenezo yake kwani kwa hali ya sasa siyo rahisi kusafirisha mizigo. Pia aliomba apelekewe umeme maeneo ya Mbawalachini na Mkunjanguo. “Maendeleo hayana chama, kabila wala itikadi,” alisema.

Wabunge wengine waliofuatana na Waziri Mkuu kwenye ziara hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Bibi Hawa Ghasia na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Bi. Hamida Mohammed Abdallah (Viti Maalum).

No comments: